3
Mwishowe hatukuweza kuvumilia zaidi. Basi, tuliamua kubaki kule Athene peke yetu, na kumtuma kwenu ndugu yetu Timotheo, ambaye ni mfanyakazi mwenzetu kwa ajili ya Mungu katika kuhubiri Habari Njema ya Kristo. Tulimtuma ili awaimarisheni na kuwafarijini, kusudi imani ya mtu yeyote miongoni mwenu isije ikafifia kwa sababu ya taabu hizo. Ninyi mnajua kwamba tunapaswa kupata mateso. Maana, tulipokuwa pamoja nanyi, tuliwaambieni kwamba tutateswa; na kama mjuavyo ndivyo ilivyotukia. Ndio maana nilimtuma Timotheo kwenu. Sikuweza kungoja zaidi, na hivyo nilimtuma nipate habari za imani yenu. Isije ikawa labda Mshawishi aliwajaribuni na kazi yote tuliyofanya miongoni mwenu imepotea bure! Sasa Timotheo amekwisha rudi, naye ametupa habari za kufurahisha kuhusu imani na upendo wenu. Ametuarifu kwamba mnatukumbuka daima, na kwamba mna hamu ya kutuona sisi kama nasi tulivyo na hamu ya kuwaoneni. Basi, habari za imani yenu zimetutia moyo katika taabu na mateso yetu yote, kwani sasa tunaishi kweli ikiwa ninyi mnasimama imara katika kuungana na Bwana. Sasa twaweza kumshukuru Mungu wetu kwa ajili yenu. Tunamshukuru kwa furaha tuliyo nayo mbele yake kwa sababu yenu. 10 Tunazidi kumwomba Mungu usiku na mchana kwa moyo wetu wote ili atupatie fursa ya kuwaoneni uso kwa uso ili tuweze kurekebisha chochote kilichopungua katika imani yenu. 11 Tunamwomba Mungu, Baba yetu mwenyewe, na Bwana wetu Yesu atutayarishie njia ya kuja kwenu. 12 Bwana awawezeshe ninyi kupendana na kuwapenda watu wote zaidi na zaidi, kama vile sisi tunavyowapenda ninyi. 13 Hivyo ataiimarisha mioyo yenu, nanyi mtakuwa wakamilifu na watakatifu mbele ya Mungu na Baba yetu wakati Bwana wetu Yesu atakapokuja pamoja na wote walio wake.