7
Melkisedeki alikuwa mfalme wa Salemu, na kuhani wa Mungu Mkuu. Abrahamu alipokuwa anarudi kutoka vitani ambako aliwaua wafalme, Melkisedeki alikutana naye akambariki, naye Abrahamu akampa sehemu ya kumi ya vitu vyote alivyokuwa navyo. (Maana ya kwanza ya jina hili Melkisedeki ni “Mfalme wa Uadilifu”; na, kwa vile yeye alikuwa mfalme wa Salemu, jina lake pia lina maana ya “Mfalme wa Amani.”) Baba yake na mama yake hawatajwi, wala ukoo wake hautajwi; haisemwi alizaliwa lini au alikufa lini. Anafanana na Mwana wa Mungu, na anaendelea kuwa kuhani daima. Basi, mwaona jinsi mtu huyu alivyokuwa maarufu. Baba Abrahamu alimpa sehemu moja ya kumi ya vitu vyote alivyoteka vitani. Tunajua vilevile kwamba kufuatana na Sheria, wana wa Lawi ambao ni makuhani, wanayo haki ya kuchukua sehemu ya kumi kutoka kwa watu, yaani ndugu zao, ingawaje nao ni watoto wa Abrahamu. Lakini huyo Melkisedeki hakuwa wa ukoo wa Lawi, hata hivyo alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu; tena akambariki yeye ambaye alikuwa amepewa ahadi ya Mungu. Hakuna mashaka hata kidogo kwamba anayebariki ni mkuu zaidi kuliko yule anayebarikiwa. Tena, hao makuhani wanaopokea sehemu ya kumi, ni watu ambao hufa; lakini hapa anayepokea sehemu ya kumi, yaani Melkisedeki, anasemekana kwamba hafi. Twaweza, basi, kusema kwamba Abrahamu alipotoa sehemu moja ya kumi, Lawi (ambaye watoto wake hupokea sehemu moja ya kumi) alitoa sehemu moja ya kumi pia. 10 Maana Lawi hakuwa amezaliwa bado, bali ni kama alikuwa katika mwili wa baba yake, Abrahamu, wakati Melkisedeki alipokutana naye. 11 Kutokana na ukuhani wa Walawi, watu wa Israeli walipewa Sheria. Sasa, kama huduma ya Walawi ingalikuwa kamilifu hapangekuwa tena na haja ya kutokea ukuhani mwingine tofauti, ukuhani ambao umefuata utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki, na si ule wa Aroni. 12 Maana ukuhani ukibadilika ni lazima Sheria nayo ibadilike. 13 Naye Bwana wetu ambaye mambo hayo yote yanasemwa juu yake, alikuwa wa kabila lingine, na wala hakuna hata mmoja wa kabila lake aliyepata kutumikia madhabahuni akiwa kuhani. 14 Inafahamika wazi kwamba yeye alizaliwa katika kabila la Yuda ambalo Mose hakulitaja alipokuwa anasema juu ya makuhani. 15 Tena jambo hili ni dhahiri zaidi: kuhani mwingine anayefanana na Melkisedeki amekwisha tokea. 16 Yeye hakufanywa kuwa kuhani kwa sheria na maagizo ya kibinadamu, bali kwa nguvu ya uhai ambao hauna mwisho. 17 Maana Maandiko yasema: “Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.” 18 Basi, ile amri ya zamani ilifutwa kwa sababu ilikuwa hafifu na isiyofaa kitu. 19 Maana Sheria ya Mose haikuweza kukamilisha jambo lolote. Lakini sasa, mahali pake pamewekwa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo tunaweza kumkaribia Mungu. 20 Zaidi ya hayo hapa pana kiapo cha Mungu. Wakati wale wengine walipofanywa makuhani hapakuwako kiapo. 21 Lakini Yesu alifanywa kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia: “Bwana ameapa, wala hataigeuza nia yake: Wewe ni kuhani milele.” 22 Basi, kutokana na tofauti hii, Yesu amekuwa mdhamini wa agano lililo bora zaidi. 23 Kuna tofauti nyingine pia: hao makuhani wengine walikuwa wengi kwa sababu walikufa na hawakuweza kuendelea na kazi yao. 24 Lakini Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. 25 Hivyo, yeye anaweza daima kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa Mungu. 26 Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi na ameinuliwa mpaka juu mbinguni. 27 Yeye si kama wale makuhani wakuu wengine; hana haja ya kutoa dhabihu kila siku, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alifanya hivyo mara moja tu wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote. 28 Sheria ya Mose huwateua watu waliokuwa dhaifu kuwa makuhani wakuu; lakini ahadi ya Mungu aliyoifanya kwa kiapo na ambayo imefika baada ya sheria imemteua Mwana ambaye amefanywa mkamilifu milele.