16
1 “Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.
2 Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
3 Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.
4 Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. “Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
5 Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: Unakwenda wapi?
6 Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.
7 Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.
8 Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
9 Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;
10 kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;
11 kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
12 “Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.
13 Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
14 Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
16 “Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!”
17 Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, “Ana maana gani anapotwambia: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona? Tena anasema: Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!”
18 Basi, wakawa wanaulizana, “Ana maana gani anaposema: Bado kitambo kidogo? Hatuelewi anaongelea nini.”
19 Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, “Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?
20 Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.
22 Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
23 Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.
24 Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.
25 “Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.
26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu;
27 maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
28 Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba.”
29 Basi, wanafunzi wake wakamwambia, “Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.
30 Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu.”
31 Yesu akawajibu, “Je, mnaamini sasa?
32 Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.
33 Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!”