17
1 Kisha, Yesu akawaambia wanafunzi wake, “Haiwezekani kabisa kusitokee vikwazo vinavyosababisha dhambi; lakini ole wake mtu yule atakayevisababisha.
2 Ingekuwa afadhali kwake kufungiwa shingoni jiwe kubwa la kusagia na kutoswa baharini, kuliko kumkwaza mmoja wa wadogo hawa.
3 Jihadharini! Kama ndugu yako akikukosea, mwonye; akitubu, msamehe.
4 Na kama akikukosea mara saba kwa siku, na kila mara akarudi kwako akisema Nimetubu, lazima umsamehe.”
5 Mitume wakamwambia Bwana, “Utuongezee imani.”
6 Naye Bwana akajibu, “Kama imani yenu ingekuwa ndogo hata kama chembe ndogo ya haradali, mngeweza kuuambia mti huu wa mkuyu: Ng'oka ukajipandikize baharini, nao ungewatii.
7 “Tuseme mmoja wenu ana mtumishi ambaye analima shambani au anachunga kondoo. Je, anaporudi kutoka shambani, atamwambia: Haraka, njoo ule chakula?
8 La! Atamwambia: Nitayarishie chakula, ujifunge tayari kunitumikia mpaka nitakapomaliza kula na kunywa, ndipo nawe ule na unywe.
9 Je utamshukuru huyo mtumishi kwa sababu ametimiza aliyoamriwa?
10 Hali kadhalika na ninyi mkisha fanya yote mliyoamriwa, semeni: Sisi ni watumishi tusio na faida, tumetimiza tu yale tuliyotakiwa kufanya.”
11 Yesu akiwa safarini kwenda Yerusalemu alipitia mipakani mwa Samaria na Galilaya.
12 Alipokuwa anaingia katika kijiji kimoja, watu kumi wenye ukoma walikutana naye, wakasimama kwa mbali.
13 Wakapaza sauti wakisema, “Yesu Mwalimu, tuonee huruma!”
14 Alipowaona akawaambia, “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Basi, ikawa walipokuwa wanakwenda, wakatakasika.
15 Mmoja wao alipoona kwamba ameponywa alirudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa.
16 Akajitupa chini mbele ya miguu ya Yesu huku akimshukuru. Huyo alikuwa Msamaria.
17 Hapo Yesu akasema, “Je, si watu kumi walitakaswa? Wale tisa wako wapi?
18 Hakupatikana mwingine aliyerudi kumtukuza Mungu ila tu huyu mgeni?”
19 Halafu akamwambia huyo mtu, “Simama, uende zako; imani yako imekuponya.”
20 Wakati mmoja, Mafarisayo walimwuliza Yesu, “Ufalme wa Mungu utakuja lini?” Naye akawajibu, “Ufalme wa Mungu hauji kwa namna itakayoweza kuonekana.
21 Wala hakuna atakayeweza kusema, Uko hapa, au Uko pale. Kwa kweli Ufalme wa Mungu uko kati yenu.”
22 Halafu akawaambia wanafunzi wake, “Siku zinakuja ambapo mtatamani kuona mojawapo ya siku za Mwana wa Mtu, lakini hamtaiona.
23 Na watu watawaambieni: Tazameni yuko hapa; ninyi msitoke wala msiwafuate.
24 Kwa maana kama vile umeme unavyotokea ghafla na kuangaza anga upande mmoja hadi mwingine, ndivyo Mwana wa Mtu atakavyokuwa siku yake.
25 Lakini kabla ya hayo, itambidi ateseke sana na kukataliwa na kizazi hiki.
26 Kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa katika siku za Mwana wa Mtu.
27 Watu waliendelea kula na kunywa, kuoa na kuolewa mpaka wakati ule Noa alipoingia katika safina. Gharika ikatokea na kuwaangamiza wote.
28 Itakuwa kama ilivyotokea wakati wa Loti. Watu waliendelea kula na kunywa, kununua na kuuza, kupanda mbegu na kujenga.
29 Lakini siku ile Loti alipoondoka Sodoma, moto na kiberiti vikanyesha kama mvua kutoka mbinguni na kuwaangamiza wote.
30 Ndivyo itakavyokuwa siku ile Mwana wa Mtu atakapofunuliwa.
31 “Siku hiyo, yeyote atakayekuwa juu ya paa asishuke nyumbani kuchukua mali yake. Kadhalika, naye atakayekuwa shambani asirudi nyuma.
32 Kumbukeni yaliyompata mke wa Loti.
33 Yeyote anayetaka kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na yeyote anayeipoteza, ataiokoa.
34 Nawaambieni, siku ile usiku watu wawili watakuwa wanalala pamoja, mmoja atachukuliwa na yule mwingine ataachwa.
35 Wanawake wawili watakuwa wakisaga nafaka pamoja; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.”
36 Watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.
37 Hapo wakamwuliza, “Ni wapi Bwana?” Naye akawaambia, “Ulipo mzoga, ndipo tai watakapokusanyikia.”