Danieli
1
Mafunzo Ya Danieli Huko Babeli
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, Nebukadneza mfalme wa Babeli alikuja akazingira Yerusalemu kwa jeshi. Bwana akamtia Yehoyakimu mfalme wa Yuda mkononi mwa Nebukadneza, pamoja na baadhi ya vyombo kutoka Hekalu la Mungu. Hivi akavichukua hadi kwenye hekalu la mungu wake huko Shinari, naye akaviweka nyumbani ya hazina ya mungu wake.
Kisha mfalme akamwagiza Ashpenazi, mkuu wa maafisa wa mfalme, kumletea baadhi ya Waisraeli kutoka jamaa ya mfalme na kutoka jamaa kuu, vijana wanaume wasio na dosari mwilini, wenye sura nzuri, wanaoonyesha kipaji katika kila aina ya elimu, wenye ufahamu mzuri, wepesi kuelewa, na waliofuzu kuhudumu katika jumba la kifalme. Alikuwa awafundishe lugha na maandiko ya Wakaldayo. Mfalme akawaagizia kiasi cha chakula na divai ya kila siku kutoka meza ya mfalme. Walikuwa wafundishwe kwa miaka mitatu, na hatimaye waingie kwenye utumishi wa mfalme.
Baadhi ya hawa vijana walitoka Yuda: nao ni Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Mkuu wa maafisa akawapa majina mapya: Danieli akamwita Belteshaza, Hanania akamwita Shadraki, Mishaeli akamwita Meshaki, na Azaria akamwita Abednego.
Lakini Danieli alikusudia kuwa hatajitia unajisi kwa chakula cha mfalme na divai, naye akamwomba mkuu wa maafisa ruhusa ili asijinajisi kwa njia hii. Basi Mungu alikuwa amemfanya huyo mkuu wa maafisa kuonyesha upendeleo na huruma kwa Danieli, 10 lakini huyo mkuu wa maafisa akamwambia Danieli, “Ninamwogopa bwana wangu mfalme, aliyeagizia chakula na kinywaji chenu. Kwa nini aone nyuso zenu zikiwa mbaya kuliko za vijana wengine wa rika lenu? Mfalme atakata kichwa changu kwa sababu yenu.”
11 Ndipo Danieli akamwambia mlinzi aliyeteuliwa na huyo mkuu wa maafisa kuwasimamia Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria, 12 “Tafadhali wajaribu watumishi wako kwa siku kumi. Usitupe chochote ila nafaka na mboga za majani* tule, na maji ya kunywa. 13 Baadaye ulinganishe sura zetu na vijana wanaokula chakula cha mfalme, ukawatendee watumishi wako kulingana na unachoona.” 14 Basi akakubali jambo hili, akawajaribu kwa siku kumi.
15 Mwisho wa zile siku kumi, walionekana kuwa na afya na kunawiri zaidi kuliko yeyote kati ya wale vijana waliokula chakula cha mfalme. 16 Hivyo mlinzi wao akaondoa chakula chao na divai yao waliopangiwa kula na kunywa, akawapa nafaka na mboga za majani badala yake.
17 Mungu akawapa hawa vijana wanne maarifa na ufahamu wa kila aina ya maandiko na elimu. Naye Danieli aliweza kufahamu maono na aina zote za ndoto.
18 Mwisho wa muda uliowekwa na mfalme kuwaingiza kwake, mkuu wa maafisa akawaleta mbele ya Mfalme Nebukadneza. 19 Mfalme akazungumza nao, akaona hakuna aliyelingana na Danieli, Hanania, Mishaeli na Azaria. Hivyo wakaingia katika utumishi wa mfalme. 20 Katika kila jambo la hekima na ufahamu kuhusu kile mfalme alichowauliza, aliwaona bora mara kumi zaidi kuliko waganga na wasihiri wote katika ufalme wake wote.
21 Naye Danieli akabaki huko mpaka mwaka wa kwanza wa utawala wa Mfalme Koreshi.
* 1:12 Nafaka na mboga za majani, yaani zeroimu kwa Kiebrania, ina maana ya aina za ngano na shayiri, na jamii ya kunde kama maharagwe, dengu, choroko, n.k.