10
Maono Ya Danieli Kuhusu Mtu
Katika mwaka wa tatu wa utawala wa Koreshi mfalme wa Uajemi, Danieli (ambaye aliitwa Belteshaza) alipewa ufunuo. Ujumbe wake ulikuwa kweli, nao ulihusu vita vikubwa. Ufahamu wa ujumbe ulimjia katika maono.
Wakati huo, mimi Danieli nikaomboleza kwa majuma matatu. Sikula chakula kizuri; nyama wala divai havikugusa midomo yangu; nami sikujipaka mafuta kamwe mpaka majuma matatu yalipotimia.
Kwenye siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa nimesimama kwenye ukingo wa mto mkubwa Hidekeli,* nikatazama juu, na mbele yangu alikuwepo mtu aliyevaa mavazi ya kitani na mshipi wa dhahabu safi kutoka ufazi kiunoni mwake. Mwili wake ulikuwa kama kito cha zabarajadi safi, uso wake kama umeme wa radi, macho yake kama mwali wa moto, mikono yake na miguu yake kama mngʼao wa shaba iliyosuguliwa sana, nayo sauti yake kama ya umati mkubwa wa watu.
Mimi Danieli, ni mimi peke yangu niliyeona hayo maono; watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona, lakini waligubikwa na hofu kuu, hata wakakimbia na kujificha. Kwa hiyo niliachwa peke yangu, nikikodolea macho maono hayo makubwa; sikubakiwa na nguvu, na rangi ya uso wangu ikabadilika kama aliyekufa, nikakosa nguvu. Kisha nikamsikia akisema, nami nilipokuwa nikimsikiliza, nikalala kifudifudi, nikapatwa na usingizi mzito.
10 Mkono ulinigusa, ukaninyanyua, na kuniweka nikipiga magoti na mikono yangu ikashika chini, huku nikiwa bado ninatetemeka. 11 Akasema, “Danieli, wewe mtu upendwaye sana, fikiri kwa makini maneno ninayokwenda kunena nawe sasa; simama wima, kwa maana sasa nimetumwa kwako.” Naye aliponiambia haya, nikasimama nikitetemeka.
12 Ndipo akaendelea kusema, “Danieli, usiogope. Tangu siku ya kwanza ulipotia moyo wako ili kupata ufahamu na kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yalisikiwa, nami nimekuja ili kujibu maneno yako. 13 Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga kwa siku ishirini na moja. Ndipo Mikaeli, mmoja wa malaika wakuu, alikuja kunisaidia, kwa sababu nilikuwa nimezuiliwa huko na mfalme wa Uajemi. 14 Sasa nimekuja kukuelezea mambo yatakayowatokea watu wako wakati ujao, kwa maana maono hayo yanahusu wakati ambao haujaja bado.”
15 Alipokuwa akinielezea haya, nilisujudu uso wangu ukiwa umeelekea chini, nikawa bubu. 16 Ndipo mmoja aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa midomo yangu, nami nikafungua kinywa changu, nikaanza kunena. Nikamwambia yule aliyesimama mbele yangu, “Nimepatwa na huzuni kubwa kwa sababu ya maono haya, bwana wangu, nami nimeishiwa nguvu. 17 Bwana wangu, mimi mtumishi wako nitawezaje kuzungumza na wewe? Nguvu zangu zimeniishia hata ninashindwa kupumua.”
18 Tena yule aliyeonekana kama mwanadamu akanigusa na kunitia nguvu. 19 Akasema, “Ee mtu upendwaye sana, usiogope. Amani iwe kwako! Uwe na nguvu sasa; jipe nguvu.”
Alipozungumza nami, nilipata nguvu, nikasema, “Nena, bwana wangu, kwa kuwa umenipa nguvu.”
20 Kwa hiyo akasema, “Je, unajua kwa nini nimekujia? Sasa hivi nitarudi kupigana dhidi ya mkuu wa Uajemi, nami nikienda, mkuu wa Uyunani atakuja. 21 Lakini kwanza nitakuambia kile kilichoandikwa katika Kitabu cha Kweli. (Hakuna hata mmoja anayenisaidia dhidi yao isipokuwa Mikaeli, mkuu wenu.
* 10:4 Hedekeli ndio Mto Tigrisi.