3
Sanamu Ya Dhahabu Na Moto Mkali
Mfalme Nebukadneza alitengeneza sanamu ya dhahabu, yenye kimo cha dhiraa sitini,* na upana wa dhiraa sita, akaisimamisha kwenye tambarare ya Dura katika jimbo la nchi ya Babeli. Kisha mfalme akaita wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wote wa jimbo kuja kuizindua sanamu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha. Basi wakuu, wasimamizi, watawala, washauri, watunza hazina, waamuzi, mahakimu na maafisa wengine wa jimbo walikusanyika ili kuizindua sanamu ile Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha, nao wakasimama mbele ya hiyo sanamu.
Ndipo mpiga mbiu akatangaza kwa sauti kubwa, “Enyi watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha, hili ndilo mnaloamriwa kulifanya: Mara mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za sauti za ala za uimbaji, lazima mwanguke chini na kuabudu sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza ameisimamisha. Mtu yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu sanamu hiyo, atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto.”
Kwa hiyo, mara waliposikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda na aina zote za ala za uimbaji, watu wa kabila zote, mataifa na watu wa kila lugha wakaanguka chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu ambayo Mfalme Nebukadneza alikuwa ameisimamisha.
Wakati huo baadhi ya Wakaldayo walijitokeza na kuwashtaki Wayahudi. Wakamwambia Mfalme Nebukadneza, “Ee mfalme, uishi milele! 10 Ee mfalme, umetoa amri kwamba kila mmoja atakayesikia sauti ya baragumu, filimbi, kinubi, zeze, kinanda, zumari na aina zote za ala za uimbaji lazima aanguke chini na kuiabudu ile sanamu ya dhahabu, 11 na kwamba yeyote ambaye hataanguka chini na kuiabudu atatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. 12 Lakini wako baadhi ya Wayahudi ambao umewaweka juu ya mambo ya jimbo la Babeli: yaani, Shadraki, Meshaki na Abednego, ambao hawakujali wewe, ee mfalme. Hawaitumikii miungu yako wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
13 Mfalme Nebukadneza, akiwa amekasirika na mwenye ghadhabu kali, akawaita Shadraki, Meshaki na Abednego. Hivyo watu hawa wakaletwa mbele ya mfalme, 14 naye Nebukadneza akawauliza, “Je, ni kweli kwamba ninyi Shadraki, Meshaki na Abednego hamuitumikii miungu yangu wala kuiabudu sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha? 15 Basi wakati mtakaposikia sauti ya baragumu, filimbi, marimba, zeze, kinubi, zumari na aina zote za ala za uimbaji, kama mtakuwa tayari kusujudu na kuiabudu hiyo sanamu niliyoitengeneza, vyema sana. Lakini kama hamtaiabudu, mtatupwa saa iyo hiyo ndani ya tanuru iwakayo moto. Naye ni mungu yupi atakayeweza kuwaokoa ninyi, kutoka mkono wangu?”
16 Shadraki, Meshaki na Abednego wakamjibu mfalme, “Ee Nebukadneza, hatuhitaji kujitetea mbele zako kuhusu jambo hili. 17 Ikiwa tutatupwa ndani ya tanuru iwakayo moto, Mungu tunayemtumikia anaweza kutuokoa na moto, naye atatuokoa kutoka mkononi mwako, ee mfalme. 18 Lakini hata ikiwa hatatuokoa, ee mfalme, tunataka ufahamu kwamba, hatutaitumikia miungu yako wala kuiabudu sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”
19 Ndipo Nebukadneza akawa na ghadhabu kali sana kwa Shadraki, Meshaki na Abednego, nayo nia yake ikabadilika kwao. Akaagiza tanuru ichochewe moto mara saba kuliko kawaida yake 20 na kuwaamuru baadhi ya askari wake wenye nguvu zaidi katika jeshi lake kuwafunga Shadraki, Meshaki na Abednego na kuwatupa ndani ya tanuru iwakayo moto. 21 Hivyo watu hawa, walifungwa na kutupwa ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamevaa majoho yao, suruali, vilemba na nguo zao nyingine. 22 Amri ya mfalme ilikuwa ya haraka sana na tanuru ilikuwa na moto mkali kiasi kwamba miali ya moto iliwaua wale askari waliowapeleka Shadraki, Meshaki na Abednego. 23 Watu hawa watatu walianguka ndani ya tanuru iwakayo moto wakiwa wamefungwa kwa uthabiti sana.
24 Ndipo Mfalme Nebukadneza akashangaa, akainuka kwa haraka na kuwauliza washauri wake, “Je, hawakuwa watu watatu ambao tuliwafunga na kuwatupa ndani ya moto?”
Washauri wakajibu, “Hakika, ee mfalme.”
25 Mfalme akasema, “Tazama! Naona watu wanne wakitembeatembea ndani ya moto, hawajafungwa wala kudhurika, naye mtu yule wa nne anaonekana kama mwana wa miungu.”
26 Ndipo Nebukadneza akaukaribia mdomo wa ile tanuru iwakayo moto na kupaza sauti, “Shadraki, Meshaki na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, tokeni! Njooni hapa!”
Ndipo Shadraki, Meshaki na Abednego wakatoka ndani ya moto. 27 Nao maliwali, wasimamizi, watawala na washauri wa mfalme wakakusanyika kuwazunguka. Waliona kwamba moto haukudhuru miili yao, wala unywele wa vichwa vyao haukuungua, majoho yao hayakuungua, wala hapakuwepo na harufu ya moto kwenye miili yao.
28 Ndipo Nebukadneza akasema, “Ahimidiwe Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego, ambaye amemtuma malaika wake na kuwaokoa watumishi wake. Walimtumaini na kukaidi amri ya mfalme, nao wakawa tayari kufa kuliko kutumikia au kuabudu mungu mwingine yeyote isipokuwa Mungu wao. 29 Kwa hiyo ninaamuru kwamba watu wa taifa lolote au lugha yoyote watakaosema kitu chochote dhidi ya Mungu wa Shadraki, Meshaki na Abednego wakatwe vipande vipande na nyumba zao zifanywe kuwa malundo ya kokoto, kwa maana hakuna mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.”
30 Kisha mfalme akawapandisha vyeo Shadraki, Meshaki na Abednego katika jimbo la Babeli.
* 3:1 Dhiraa sitini ni sawa na mita 27. 3:1 Dhiraa sita ni sawa na mita 2.7.