12
Mahali Pekee Pa Kuabudia
Hizi ndizo amri na sheria ambazo ni lazima mwe waangalifu kuzifuata katika nchi ambayo Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa kumiliki, kwa muda wote mtakaoishi katika nchi. Haribuni kabisa kila mahali pao pa kuabudia kwenye milima mirefu, vilima na chini ya kila mti mkubwa ambamo mataifa haya mnayokwenda kuchukua ardhi yao huabudia miungu yao. Bomoeni madhabahu zao, vunjeni yale mawe wanayoabudu, chomeni moto nguzo zao za Ashera; katilieni mbali sanamu za miungu yao na mfute majina yao mahali hapo.
Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kama wanavyoabudu wao. Bali mtatafuta mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua katika makabila yenu yote ili aliweke jina lake huko kuwa makao yake. Mahali hapo ndipo iwapasapo kwenda; hapo ndipo mtakapoleta sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo zenu, kile ulichoweka nadhiri kutoa, sadaka zenu za hiari na malimbuko ya makundi yenu ya ngʼombe pamoja na mbuzi na kondoo. Hapo, katika uwepo wa Bwana Mungu wenu, ninyi pamoja na jamaa zenu, mtakula na kufurahia kila kitu ambacho mmegusa kwa mikono yenu, kwa sababu Bwana Mungu wenu amewabariki.
Msifanye kama tunavyofanya hapa leo, kila mtu anavyopenda mwenyewe, kwa kuwa bado hamjafikia mahali pa mapumziko na urithi ambao Bwana Mungu wenu anawapa. 10 Lakini mtavuka Yordani na kuishi katika nchi Bwana Mungu wenu anayowapa kama urithi, naye atawapa pumziko kutokana na adui zenu wote wanaowazunguka ili ninyi mpate kuishi kwa salama. 11 Kisha kuhusu mahali Bwana Mungu wenu atakapopachagua kuwa mahali pa makao ya Jina lake, hapo ndipo inapowapasa kuleta kila kitu ninachowaamuru: sadaka zenu za kuteketezwa na dhabihu, zaka zenu na changizo, pamoja na vitu vyote vyenye thamani ambavyo mmeweka nadhiri kumtolea Bwana. 12 Hapo furahini mbele za Bwana Mungu wenu, ninyi, wana wenu na binti zenu, watumishi wenu wa kiume na wa kike, pamoja na Walawi kutoka miji yenu ambao hawana mgawo wala urithi wao wenyewe. 13 Kuweni waangalifu, msitoe dhabihu zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopapenda. 14 Mtazitoa tu mahali pale ambapo Bwana atachagua katika mojawapo ya makabila yenu, nanyi hapo zingatieni kila jambo ninalowaamuru.
15 Hata hivyo, mnaweza kuwachinja wanyama wenu katika miji yenu yoyote ile na kula nyama nyingi mpendavyo kama vile mmemchinja paa au kulungu, kulingana na baraka mtakazojaliwa na Bwana Mungu wenu. Watu walio najisi au walio safi wanaweza kula. 16 Lakini kamwe usinywe damu; imwage juu ya ardhi kama maji. 17 Hamruhusiwi kula katika miji yenu zaka yenu ya nafaka, ya divai mpya na ya mafuta, au mzaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ngʼombe na makundi yenu ya mbuzi na kondoo, wala chochote ambacho mmeweka nadhiri kukitoa, au sadaka zako za hiari, wala matoleo maalum. 18 Badala yake, mtakula vitu hivyo katika uwepo wa Bwana Mungu wenu mahali ambapo Bwana Mungu wenu atapachagua: wewe, wana wako na binti zako, watumishi wako wa kiume na wa kike, na Walawi kutoka miji yenu. Mnatakiwa mfurahi mbele za Bwana Mungu wenu kwa kula kitu mtakachoweka mikono yenu. 19 Mwe waangalifu msiwapuuze Walawi kwa muda wote mnaoishi katika nchi yenu.
20 Bwana Mungu wenu atakapokuwa ameongeza nchi yenu kama alivyowaahidi, nanyi mkitamani nyama na mkisema, “Ningependa nyama,” hapo unaweza kula nyingi upendavyo. 21 Kama mahali ambapo Bwana Mungu wenu atapachagua kuweka Jina lake ni mbali sana kutoka kwenu, unaweza kuchinja wanyama kutoka makundi yenu ya ngʼombe, ya mbuzi na ya kondoo ambayo Bwana amewapa, kama nilivyokuamuru, na mkiwa katika miji yenu wenyewe mnaweza kula nyingi mtakavyo. 22 Mle kama vile mngekula paa na kulungu. Wote walio najisi kiibada na walio safi mwaweza kula. 23 Lakini hakikisheni kwamba hamkunywa damu, kwa sababu damu ni uhai, kamwe msile uhai pamoja na nyama. 24 Hamruhusiwi kamwe kunywa damu; imwageni juu ya ardhi kama maji. 25 Msinywe damu, ili mweze kufanikiwa ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo haki machoni pa Bwana.
26 Lakini vichukueni vitu vyenu vilivyowekwa wakfu pamoja na vile mlivyoweka nadhiri, mwende mahali pale Bwana atakapopachagua. 27 Leteni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, vyote nyama na damu. Damu ya dhabihu zenu lazima imiminwe kando ya madhabahu ya Bwana Mungu wenu, lakini nyama mnaweza kula. 28 Mwe waangalifu kutii masharti haya yote ninayowapa, ili kwamba siku zote mweze kufanikiwa, ninyi pamoja na watoto wenu baada yenu, kwa sababu mtakuwa mkifanya lililo jema na sahihi mbele za macho ya Bwana Mungu wenu.
29 Bwana Mungu wenu atayakatilia mbali mbele yenu mataifa ambayo punde kidogo mtayavamia na kuyaondoa. Lakini mtakapokuwa mmeyafukuza na kuishi katika nchi yao, 30 na baada ya kuangamizwa mbele yenu, mwe waangalifu msijiingize katika tanzi kwa kuuliza habari za miungu yao, mkisema, “Je, mataifa haya hutumikiaje miungu yao? Nasi tutafanya vivyo hivyo.” 31 Kamwe msimwabudu Bwana Mungu wenu kwa njia wanayoabudu miungu yao, kwa sababu katika kuabudu miungu yao, wanafanya aina zote za machukizo anayoyachukia Bwana. Hata huwateketeza wana wao na binti zao kwa moto kama kafara kwa miungu yao.
32 Angalieni kwamba mnafanya yote niliyowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.