12
1 Mkumbuke Muumba wako
siku za ujana wako,
kabla hazijaja siku za taabu,
wala haijakaribia miaka utakaposema,
“Mimi sifurahii hiyo”:
2 kabla jua na nuru,
nao mwezi na nyota havijatiwa giza,
kabla ya kurudi mawingu baada ya mvua;
3 siku ile walinzi wa nyumba watakapotetemeka,
nao watu wenye nguvu watakapojiinamisha,
wakati wasagao watakapokoma kwa sababu ya uchache,
nao wachunguliao madirishani kutiwa giza;
4 wakati milango ya kuingia barabarani itakapofungwa
na sauti ya kusaga kufifia;
wakati watu wataamshwa kwa sauti ya ndege,
lakini nyimbo zao zote zikififia;
5 wakati watu watakapoogopa kilichoinuka juu
na hatari zitakazokuwepo barabarani;
wakati mlozi utakapochanua maua
na panzi kujikokota
nawe usiwe na shauku ya kitu chochote.
Ndipo mwanadamu aiendea nyumba yake ya milele
nao waombolezaji wakizunguka barabarani.
6 Mkumbuke Muumba wako: kabla haijakatika kamba ya fedha,
au bakuli la dhahabu halijavunjika;
kabla mtungi kuvunjika kwenye chemchemi,
au gurudumu kuvunjika kisimani,
7 nayo mavumbi kurudi ardhini yalikotoka,
na roho kurudi kwa Mungu aliyeitoa.
8 Mhubiri asema, “Ubatili! Ubatili!
Kila kitu ni ubatili!”
Hitimisho La Mambo
9 Mhubiri hakuwa tu na hekima, bali aliwagawia watu maarifa pia. Alitafakari na kutafiti na akaweka katika utaratibu mithali nyingi.
10 Mhubiri alitafiti ili kupata maneno sahihi na kila alichoandika kilikuwa sawa na kweli.
11 Maneno ya wenye hekima ni kama mchokoro, mithali zao zilizokusanywa pamoja ni kama misumari iliyogongomewa ikawa imara, yaliyotolewa na Mchungaji mmoja.
12 Tena zaidi ya hayo, mwanangu, kubali maonyo, hakuna mwisho wa kutunga vitabu vingi, nako kusoma sana huuchosha mwili.
13 Hii ndiyo jumla ya maneno;
yote yamekwisha sikiwa:
Mche Mungu, nawe uzishike amri zake,
maana kwa jumla ndiyo impasayo mtu.
14 Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi,
pamoja na kila neno la siri,
likiwa jema au baya.