9
Ushindi Wa Wayahudi
1 Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia.
2 Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa.
3 Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai.
4 Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi.
5 Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia.
6 Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume 500.
7 Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha,
8 Poratha, Adalia, Ardatha,
9 Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha,
10 wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara.
11 Mfalme aliarifiwa siku iyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani.
12 Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume 500 na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utafanyiwa.”
13 Esta akajibu, “Ikimpendeza mfalme, uwape ruhusa Wayahudi walioko Shushani warudie amri ya leo kesho pia, na wana wa Hamani kumi wanyongwe mahali pa kunyongea watu.”
14 Basi mfalme akaamuru kwamba hili litendeke. Amri ilitolewa huko Shushani, nao wakawanyonga wana kumi wa Hamani.
15 Wayahudi huko Shushani wakakusanyika pamoja siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, nao wakawaua wanaume 300 huko Shushani, lakini hawakuchukua nyara zao.
16 Wakati ule ule, Wayahudi wengine waliokuwa kwenye majimbo ya mfalme, wakakusanyika kujilinda nao wakapata nafuu kutokana na adui zao. Waliua adui zao wapatao 75,000 lakini hawakugusa nyara zao.
17 Hili lilitendeka siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari na siku ya kumi na nne walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
Kusherehekea Purimu
18 Wayahudi huko Shushani, hata hivyo, walikuwa wamekusanyika siku ya kumi na tatu na ya kumi na nne, pia siku ya kumi na tano walipumzika na kuifanya siku ya karamu na furaha.
19 Ndiyo sababu Wayahudi wanaokaa vijijini na katika miji midogo huadhimisha siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari kama siku ya furaha na karamu, siku ambayo wao hupeana zawadi mmoja kwa mwingine.
20 Mordekai aliandika matukio haya, naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote walioko katika majimbo ya Mfalme Ahasuero, majimbo yaliyo mbali na karibu,
21 akiwataka kila mwaka washerehekee siku ya kumi na nne na ya kumi na tano ya mwezi wa Adari
22 kama wakati ambao Wayahudi walipata nafuu kutoka kwa adui zao na kama mwezi ambao huzuni yao iligeuzwa kuwa furaha na kuomboleza kwao kuwa siku ya kusherehekea. Aliwaandikia kushika siku hizo kama siku za karamu na za furaha na kupeana zawadi za vyakula wao kwa wao na zawadi kwa maskini.
23 Hivyo Wayahudi walikubali kuendeleza sherehe walizokuwa wamezianza, wakifanya lile Mordekai alilokuwa amewaandikia.
24 Kwa maana Hamani mwana wa Hamedatha Mwagagi, adui wa Wayahudi wote, alikuwa amepanga hila dhidi ya Wayahudi ili kuwaangamiza, na alikuwa amepiga puri (yaani kura) kwa ajili ya maangamizi na uharibifu wao.
25 Lakini wakati shauri hilo baya lilipoarifiwa kwa mfalme, alitoa amri iliyoandikwa kwamba mipango mibaya ambayo Hamani ameipanga dhidi ya Wayahudi inapasa imrudie juu ya kichwa chake mwenyewe, na kwamba yeye na wanawe waangikwe mahali pa kunyongea watu.
26 (Kwa hiyo siku hizi ziliitwa Purimu, kutokana na neno puri.) Kwa sababu ya kila kitu kilichoandikwa kwenye barua hii na kwa sababu ya yale waliyoyaona na yale yaliyowatokea,
27 Wayahudi wakachukua na kuifanya desturi kwamba wao na wazao wao na wote ambao walijiunga nao wangefanya bila kuacha kushika siku hizi mbili kila mwaka, kwa njia ilivyoelekezwa na kwa wakati wake.
28 Siku hizi zinapasa zikumbukwe na kuadhimishwa katika kila kizazi, kila jamaa na katika kila jimbo na kila jiji. Nazo siku hizi za Purimu kamwe zisikome kusherehekewa na Wayahudi, wala kumbukumbu zake zisipotee miongoni mwa wazao wake.
29 Basi Malkia Esta binti Abihaili, pamoja na Mordekai, Myahudi, waliandika kwa mamlaka yote kuthibitisha barua hii ya pili kuhusu Purimu.
30 Naye Mordekai akatuma barua kwa Wayahudi wote katika majimbo 127 ya ufalme wa Ahasuero, barua zenye maneno ya amani na matumaini,
31 ili kuimarisha siku hizi za Purimu katika majira yake yaliyowekwa, kama Mordekai, Myahudi na Malkia Esta walivyowaamuru, na walivyojiimarisha wenyewe na wazao wao kuhusu nyakati za kufunga na kuomboleza.
32 Amri ya Esta ilithibitisha taratibu hizi kuhusu Purimu, nayo ikaandikwa katika kumbukumbu.