23
Sheria Za Haki Na Rehema
“Usieneze habari za uongo. Usimsaidie mtu mwovu kwa kuwa shahidi mwenye nia ya kudhuru wengine.
“Usifuate umati wa watu katika kutenda mabaya. Unapotoa ushahidi kwenye mashtaka, usipotoshe haki ukijumuika na umati wa watu, nawe usimpendelee mtu maskini katika mashtaka yake.
“Kama ukikutana na maksai au punda wa adui yako anapotea, hakikisha umemrudisha kwake. Ukiona punda wa mtu anayekuchukia ameanguka na mzigo wake, usimwache hapo alipoangukia; hakikisha kuwa umemsaidia.
“Usiwanyime haki watu wako walio maskini katika mashtaka yao. Ujiepushe na mashtaka ya uongo, wala usimuue mtu asiye na hatia au mtu mwaminifu, kwa maana sitamhesabia hana hatia yeye aliye na hatia.
“Usipokee rushwa, kwa kuwa rushwa hupofusha wale waonao, na kupinda maneno ya wenye haki.
“Usimwonee mgeni; ninyi wenyewe mnajua jinsi mgeni anavyojisikia, kwa sababu mlikuwa wageni Misri.
Sheria Za Sabato
10 “Kwa muda wa miaka sita mtapanda mashamba yenu na kuvuna mazao, 11 lakini katika mwaka wa saba usiilime ardhi wala kuitumia, ili watu walio maskini miongoni mwenu waweze kupata chakula kutoka kwenye hayo mashamba, nao wanyama pori wapate chakula kwa yale mabaki watakayobakiza. Utafanya hivyo katika shamba lako la mizabibu na la mizeituni.
12 “Kwa siku sita fanya kazi zako, lakini siku ya saba usifanye kazi, ili maksai wako na punda wako wapate kupumzika, naye mtumwa aliyezaliwa nyumbani mwako, pamoja na mgeni, wapate kustarehe.
13 “Uzingatie kutenda kila kitu nilichokuambia. Usiombe kwa majina ya miungu mingine, wala usiyaruhusu kusikika kinywani mwako.
Sikukuu Tatu Za Mwaka
(Kutoka 34:18-26; Kumbukumbu 16:1-17)
14 “Mara tatu kwa mwaka utanifanyia sikukuu.
15 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu; kwa siku saba utakula mikate isiyotiwa chachu kama nilivyokuagiza. Fanya jambo hili kwa wakati uliopangwa katika mwezi wa Abibu, ndio mwezi wa nne, kwa sababu katika mwezi huo ulitoka Misri.
“Mtu yeyote asije mbele yangu mikono mitupu.
16 “Utaadhimisha Sikukuu ya Mavuno kwa malimbuko ya mazao yako uliyopanda katika shamba lako.
“Utaadhimisha Sikukuu ya Kukusanya mavuno mwishoni mwa mwaka, unapokusanya mavuno yako toka shambani.
17 “Mara tatu kwa mwaka wanaume wote watakuja mbele za Bwana Mwenyezi.
18 “Msitoe damu ya dhabihu kwangu pamoja na kitu chochote kilicho na chachu.
“Mafuta ya mnyama wa sadaka ya sikukuu yangu yasibakizwe mpaka asubuhi.
19 “Utaleta malimbuko bora ya ardhi yako katika nyumba ya Bwana Mungu wako.
“Usimchemshe mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Malaika Wa Mungu Kuandaa Njia
20 “Tazama, ninamtuma malaika akutangulie mbele yako akulinde njiani na kukuleta mpaka mahali nilipoandaa. 21 Mtamtii na kusikiliza kile anachokisema. Usiasi dhidi yake; hatakusamehe uasi wako, kwa maana Jina langu limo ndani yake. 22 Kama ukitii kweli kweli kile asemacho na kufanya yote nisemayo, nitakuwa adui wa adui zako, na nitawapinga wale wakupingao. 23 Malaika wangu atatangulia mbele yako na kukuleta katika nchi ya Waamori, Wahiti, Waperizi, Wakanaani, Wahivi na Wayebusi, nami nitawafutilia mbali. 24 Usiisujudie miungu yao, au kuiabudu, wala kufuata desturi yao. Utayabomoa kabisa na kuvunjavunja mawe yao ya ibada vipande vipande. 25 Utamwabudu Bwana Mungu wako, na baraka zake zitakuwa juu ya vyakula vyako na maji yako. Nami nitaondoa maradhi miongoni mwako, 26 na hakuna atakayeharibu mimba wala atakayekuwa tasa katika nchi yako. Nami nitakupa maisha makamilifu.
27 “Nitapeleka utisho wangu mbele yako na kufadhaisha kila taifa utakalolifikia. Nitafanya adui zako wote wakupe kisogo na kukimbia. 28 Nitatanguliza manyigu mbele yako kuwafukuza Wahivi, Wakanaani na Wahiti waondoke njiani mwako. 29 Lakini sitawafukuza kwa mara moja, kwa sababu nchi itabaki ukiwa na wanyama pori watakuwa wengi mno kwako. 30 Nitawafukuza kidogo kidogo mbele yako, mpaka uwe umeongezeka kiasi cha kutosha kuimiliki nchi.
31 “Nitaweka mipaka ya nchi yako kuanzia Bahari ya Shamu hadi Bahari ya Wafilisti, na kuanzia jangwani hadi Mto Frati. Nitawatia watu wanaoishi katika nchi hizo mikononi mwako, nawe utawafukuza watoke mbele yako. 32 Usifanye agano lolote nao wala na miungu yao. 33 Usiwaache waishi katika nchi yako, la sivyo watakusababisha utende dhambi dhidi yangu, kwa sababu ibada ya miungu yao hakika itakuwa mtego kwako.”