9
Pigo La Tano: Vifo Vya Mifugo
1 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo Bwana, Mungu wa Waebrania asemalo: “Waachie watu wangu waende ili wapate kuniabudu.”
2 Kama ukikataa kuwaachia waende, nawe ukiendelea kuwashikilia,
3 mkono wa Bwana utaleta pigo baya kwa mifugo yako, juu ya farasi wako, punda, ngamia, ngʼombe wako, kondoo na mbuzi.
4 Lakini Bwana ataweka tofauti kati ya mifugo ya Israeli na ile ya Misri, kwamba hakuna mnyama wa Mwisraeli atakayekufa.’ ”
5 Bwana akaweka wakati na kusema, “Kesho Bwana atalitenda hili katika nchi.”
6 Siku iliyofuata Bwana akalitenda: Mifugo yote ya Wamisri ikafa, lakini hakuna hata mnyama mmoja wa wana wa Israeli aliyekufa.
7 Farao akatuma watu kuchunguza, nao wakakuta kuwa hakuna hata mnyama mmoja wa Waisraeli aliyekufa. Lakini moyo wa Farao haukukubali kuwaachia watu waende.
Pigo La Sita: Majipu
8 Kisha Bwana akamwambia Mose na Aroni, “Chukueni majivu ya tanuru, naye Mose ayarushe angani mbele ya Farao.
9 Yatakuwa vumbi jepesi juu ya nchi yote ya Misri, pia yatatokea majipu yenye kufura juu ya watu na wanyama katika nchi yote.”
10 Basi wakachukua majivu kwenye tanuru na kusimama mbele ya Farao. Mose akayarusha hewani, nayo majipu yenye kufura yakatokea miilini mwa watu na wanyama.
11 Waganga hawakuweza kusimama mbele ya Mose kwa sababu ya majipu yale yaliyokuwa miilini mwao na juu ya miili ya Wamisri wote.
12 Lakini Bwana akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, naye hakuwasikiliza Mose na Aroni, sawasawa kama vile Bwana alivyokuwa amemwambia Mose.
Pigo La Saba: Mvua Ya Mawe
13 Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi, usimame mbele ya Farao, umwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Waebrania: Waachie watu wangu waende, ili kwamba waweze kuniabudu,
14 au wakati huu nitaleta mapigo yangu yenye nguvu dhidi yako, maafisa wako na watu wako, ili upate kujua kuwa hakuna mwingine kama Mimi katika dunia yote.
15 Kwa kuwa mpaka sasa ningelikuwa nimenyoosha mkono wangu na kukupiga wewe na watu wako kwa pigo ambalo lingekufutilia mbali juu ya nchi.
16 Lakini nimekuinua wewe kwa kusudi hili hasa, ili nipate kukuonyesha uwezo wangu, na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani yote.
17 Bado unaendelea kujiinua juu ya watu wangu, wala hutaki kuwaachia waende.
18 Kwa hiyo, kesho wakati kama huu nitaleta mvua mbaya sana ya mawe ambayo haijapata kunyesha katika nchi ya Misri, tangu siku ilipoumbwa mpaka leo.
19 Sasa toa amri urudishe wanyama wote watoke malishoni na chochote ambacho kipo mashambani waje mpaka mahali pa usalama, kwa sababu mvua ya mawe itanyesha juu ya kila mtu na kila mnyama ambaye hajaletwa ndani ambao bado wako nje mashambani, nao watakufa.’ ”
20 Wale maafisa wa Farao ambao waliliogopa neno la Bwana wakafanya haraka kuwaleta watumwa wao na mifugo yao ndani.
21 Lakini wale waliopuuza neno la Bwana wakawaacha watumwa wao na mifugo yao shambani.
22 Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nyoosha mkono wako kuelekea angani ili kwamba mvua ya mawe inyeshe juu ya Misri yote, juu ya watu, wanyama na juu ya kila kitu kiotacho katika mashamba ya Misri.”
23 Mose alipoinyoosha fimbo yake kuelekea angani, Bwana akatuma ngurumo na mvua ya mawe, umeme wa radi ulimulika hadi nchi. Kwa hiyo Bwana akaifanya mvua ya mawe kunyesha juu ya nchi ya Misri,
24 mvua ya mawe ikanyesha na radi ikamulika pote. Ikawa dhoruba ya kutisha ambayo haijakuwako katika nchi ya Misri, tangu nchi hiyo iwe taifa.
25 Mvua ya mawe ikaharibu kila kitu katika nchi ya Misri kilichokuwa katika mashamba, watu na wanyama, ikaharibu kila kitu kinachoota mashambani na kuvunja kila mti.
26 Mahali pekee ambapo mvua ya mawe haikunyesha ni nchi ya Gosheni, ambako Waisraeli waliishi.
27 Ndipo Farao akawaita Mose na Aroni akawaambia, “Wakati huu nimetenda dhambi. Bwana ni mwenye haki, mimi na watu wangu ni wakosaji.
28 Mwombeni Bwana, kwa kuwa tumepata ngurumo na mvua za mawe za kututosha. Nitawaachia mwondoke; hamtahitaji kungoja zaidi.”
29 Mose akamjibu, “Nitakapokuwa nimetoka nje ya mji, nitanyoosha mikono yangu juu kumwomba Bwana. Ngurumo zitakoma na hapatakuwepo mvua ya mawe tena, ili upate kujua kuwa, nchi ni mali ya Bwana.
30 Lakini ninajua kuwa wewe na maafisa wako bado hammwogopi Bwana Mungu.”
31 (Kitani na shayiri viliharibiwa, kwa kuwa shayiri ilikuwa na masuke, na kitani ilikuwa katika kutoa maua.
32 Hata hivyo, ngano na jamii nyingine ya ngano hazikuharibiwa kwa sababu zilikuwa hazijakomaa bado.)
33 Kisha Mose akaondoka kwa Farao akaenda nje ya mji. Mose akanyoosha mikono yake kuelekea kwa Bwana, ngurumo na mvua ya mawe vikakoma, mvua haikuendelea tena kunyesha nchini.
34 Farao alipoona kwamba mvua ya mawe na ngurumo zimekoma, akafanya dhambi tena. Yeye na maafisa wake wakafanya mioyo yao kuwa migumu.
35 Kwa hiyo moyo wa Farao ukawa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waende, kama vile Bwana alivyokuwa amesema kupitia Mose.