Isaya
1
Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.
 
Taifa Asi
Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!
Kwa maana Bwana amesema:
“Nimewalisha watoto na kuwalea,
lakini wameniasi mimi.
Ngʼombe anamjua bwana wake,
naye punda anajua hori la mmiliki wake,
lakini Israeli hajui,
watu wangu hawaelewi.”
 
Lo! Taifa lenye dhambi,
watu waliolemewa na uovu,
uzao wa watenda mabaya,
watoto waliozoelea upotovu!
Wamemwacha Bwana,
Wamemkataa kwa dharau
yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli
na kumgeuzia kisogo.
 
Kwa nini mzidi kupigwa?
Kwa nini kudumu katika uasi?
Kichwa chako chote kimejeruhiwa,
moyo wako wote ni mgonjwa.
Kutoka wayo wako wa mguu hadi kwenye utosi wa kichwa chako
hakuna uzima:
ni majeraha matupu na makovu
na vidonda vitokavyo damu,
havikusafishwa au kufungwa
wala kulainishwa kwa mafuta.
 
Nchi yenu imekuwa ukiwa,
miji yenu imeteketezwa kwa moto;
nchi yenu imeachwa tupu na wageni
mbele ya macho yenu,
imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.
Binti Sayuni ameachwa kama kipenu
katika shamba la mizabibu,
kama kibanda katika shamba la matikitimaji,
kama mji uliohusuriwa.
Kama Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote*
asingelituachia walionusurika,
tungelikuwa kama Sodoma,
tungelifanana na Gomora.
 
10 Sikieni neno la Bwana,
ninyi watawala wa Sodoma;
sikilizeni sheria ya Mungu wetu,
enyi watu wa Gomora!
11 Bwana anasema, “Wingi wa sadaka zenu,
ni kitu gani kwangu?
Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,
za kondoo dume na mafuta ya wanyama walionona.
Sipendezwi na damu za mafahali
wala za wana-kondoo na mbuzi.
12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,
ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,
huku kuzikanyaga nyua zangu?
13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!
Uvumba wenu ni chukizo kwangu.
Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.
14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi, na sikukuu zenu zilizoamriwa:
moyo wangu unazichukia.
Zimekuwa mzigo kwangu,
nimechoka kuzivumilia.
15 Mnaponyoosha mikono yenu katika maombi,
nitaficha macho yangu nisiwaone;
hata mkiomba maombi mengi
sitasikiliza.
Mikono yenu imejaa damu;
16 jiosheni na mkajitakase.
Yaondoeni matendo yenu maovu
mbele zangu!
Acheni kutenda mabaya,
17 jifunzeni kutenda mema!
Tafuteni haki,
watieni moyo walioonewa.
Teteeni shauri la yatima,
wateteeni wajane.
 
18 “Njooni basi tuhojiane,”
asema Bwana.
“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,
zitakuwa nyeupe kama theluji;
ingawa ni nyekundu sana kama damu,
zitakuwa nyeupe kama sufu.
19 Kama mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi,
20 lakini kama mkikataa na kuasi,
mtaangamizwa kwa upanga.”
Kwa kuwa kinywa cha Bwana kimenena.
 
21 Tazama jinsi mji uliokuwa mwaminifu
umekuwa kahaba!
Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,
haki ilikuwa inakaa ndani yake,
lakini sasa ni wauaji!
22 Fedha yenu imekuwa takataka,
divai yenu nzuri imechanganywa na maji.
23 Watawala wenu ni waasi,
rafiki wa wevi,
wote wanapenda rushwa
na kukimbilia hongo.
Hawatetei yatima,
shauri la mjane haliletwi mbele yao lisikilizwe.
24 Kwa hiyo Bwana, Bwana Mwenye Nguvu Zote,
Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:
“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu
na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.
25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,
nitawasafisha takataka zenu zote
na kuwaondolea unajisi wenu wote.
26 Nitawarudishia waamuzi wenu kama ilivyokuwa siku za zamani,
nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.
Baadaye utaitwa,
Mji wa Haki,
Mji Mwaminifu.”
27 Sayuni itakombolewa kwa haki,
wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.
28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,
nao wanaomwacha Bwana wataangamia.
 
29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni
ambayo mlifurahia,
mtafadhaika kwa sababu ya bustani
mlizozichagua.
30 Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,
kama bustani isiyokuwa na maji.
31 Mtu mwenye nguvu atatoweka kama majani makavu yawakayo moto,
na kazi yake kama cheche ya moto;
vyote vitaungua pamoja,
wala hakuna wa kuuzima huo moto.”
* 1:9 Bwana Mwenye Nguvu Zote hapa ni Yehova Sabaoth, yaani Bwana wa Majeshi; pia Warumi 9:29 na Yakobo 5:4.