36
Senakeribu Atishia Yerusalemu
(2 Wafalme 18:13-27; 2 Nyakati 32:1-19)
1 Katika mwaka wa kumi na nne wa utawala wa Mfalme Hezekia, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaishambulia miji yote ya Yuda yenye ngome na kuiteka.
2 Kisha mfalme wa Ashuru akamtuma jemadari wa jeshi pamoja na jeshi kubwa kutoka Lakishi hadi kwa Mfalme Hezekia huko Yerusalemu. Jemadari wa jeshi akasimama kwenye mfereji wa Bwawa la Juu, lililojengwa katika barabara iendayo kwenye Uwanja wa Dobi.
3 Eliakimu mwana wa Hilkia aliyekuwa msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna aliyekuwa katibu, na Yoa mwana wa Asafu mwandishi wakamwendea.
4 Jemadari wa jeshi akawaambia, “Mwambieni Hezekia,
“ ‘Hili ndilo asemalo mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru: Ni wapi unapoweka hili tumaini lako?
5 Unasema mnayo mikakati na nguvu za kijeshi, lakini unasema maneno matupu tu. Je, wewe unamtegemea nani, hata ukaniasi mimi?
6 Tazama sasa, unaitegemea Misri, fimbo ile ya mwanzi uliopasuka, ambayo huuchoma na kuujeruhi mkono wa mtu akiiegemea! Hivyo ndivyo alivyo Farao mfalme wa Misri, kwa wote wanaomtegemea.
7 Nawe kama ukiniambia, “Tunamtumainia Bwana Mungu wetu”: je, siyo yeye ambaye Hezekia aliondoa mahali pake pa juu pa kuabudia miungu na madhabahu zake, akiwaambia Yuda na Yerusalemu, “Ni lazima mwabudu mbele ya madhabahu haya”?
8 “ ‘Njooni sasa, fanyeni mapatano na bwana wangu, mfalme wa Ashuru: Nitakupa farasi elfu mbili, kama unaweza kuwapandisha waendesha farasi juu yao!
9 Utawezaje kumzuia hata afisa mmoja aliye mdogo kati ya maafisa wa bwana wangu, ijapo unategemea Misri kwa magari ya vita na wapanda farasi?
10 Zaidi ya hayo, je, nimekuja kushambulia na kuangamiza nchi hii bila Bwana? Bwana mwenyewe ndiye aliniambia niishambulie nchi hii na kuiangamiza.’ ”
11 Ndipo Eliakimu, Shebna na Yoa wakamwambia yule jemadari wa jeshi, “Tafadhali zungumza na watumishi wako kwa lugha ya Kiaramu, kwa kuwa tunaifahamu. Usiseme nasi kwa Kiebrania watu walioko juu ya ukuta wakiwa wanasikia.”
12 Lakini yule jemadari wa jeshi akajibu, “Je, bwana wangu amenituma kutoa ujumbe huu kwa bwana wenu na kwenu tu? Je, hakunituma pia kwa watu walioketi ukutani, ambao, kama ninyi, itawabidi kula mavi yao na kunywa mikojo yao wenyewe?”
13 Kisha yule jemadari wa jeshi akasimama na kuita kwa lugha ya Kiebrania, akasema: “Sikieni maneno ya mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru!
14 Hili ndilo asemalo mfalme: Msikubali Hezekia awadanganye. Hawezi kuwaokoa!
15 Msikubali Hezekia awashawishi kumtumaini Bwana kwa kuwaambia, ‘Hakika Bwana atatuokoa. Mji huu hautaangukia mikononi mwa mfalme wa Ashuru.’
16 “Msimsikilize Hezekia. Hili ndilo mfalme wa Ashuru asemalo: Fanyeni amani nami na mje kwangu. Kisha kila mmoja wenu atakula kutoka kwa mzabibu wake na mtini wake mwenyewe, na kunywa maji kutoka kisima chake mwenyewe,
17 mpaka nije nikawapeleke katika nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai mpya, nchi ya mkate na ya mashamba ya mizabibu.
18 “Msikubali Hezekia awapotoshe asemapo, ‘Bwana atatuokoa.’ Je, yuko mungu wa taifa lolote aliyewahi kuokoa nchi yake kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru?
19 Iko wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu? Je, imeokoa Samaria kutoka mkononi mwangu?
20 Ni yupi miongoni mwa miungu yote ya nchi hizi ameweza kuokoa nchi yake mkononi mwangu? Inawezekanaje basi Bwana aiokoe Yerusalemu mkononi mwangu?”
21 Lakini wale watu wakakaa kimya, wala hawakujibu lolote, kwa kuwa mfalme alikuwa amewaamuru, “Msimjibu lolote.”
22 Kisha Eliakimu mwana wa Hilkia msimamizi wa jumba la kifalme, Shebna katibu, na Yoa mwana wa Asafu, mwandishi wakamwendea Hezekia, nguo zao zikiwa zimeraruliwa, na kumwambia yale jemadari wa jeshi aliyoyasema.