16
Hotuba Ya Tano Ya Ayubu
Ayubu Anathibitisha Tena Hali Yake Ya Kutokuwa Na Hatia
Kisha Ayubu akajibu:
“Nimepata kusikia mambo mengi kama haya,
nanyi nyote ni wafariji wenye kutaabisha!
Je, maneno yenu mengi yasiyo na maana hayana mwisho?
Mna nini hata mwendelee kushindana kwa maneno?
Mimi pia ningeweza kuzungumza kama ninyi,
kama mngekuwa katika hali yangu;
ningeweza kutoa hotuba nzuri dhidi yenu,
na kuwatikisia ninyi kichwa changu.
Lakini kinywa changu kingewatia moyo;
faraja kutoka midomoni mwangu, ingewaletea nafuu.
 
“Lakini kama nikisema, maumivu yangu bado hayatulizwi;
nami kama nikijizuia, wala hayaondoki.
Ee Mungu, hakika umenichakaza;
umewaangamiza kabisa watu wa nyumbani mwangu wote.
Umenikunjakunja, nalo limekuwa ushahidi;
nako kukonda kwangu kumeongezeka sana na kushuhudia dhidi yangu.
Mungu amenishambulia na kunirarua katika hasira yake,
na kunisagia meno yake;
adui yangu hunikazia macho yake makali.
10 Watu wamenifumbulia vinywa vyao kunidhihaki;
hunipiga shavuni mwangu kwa dharau,
na kuungana pamoja dhidi yangu.
11 Mungu amenigeuzia kwa watu wabaya,
na kunitupa katika makucha ya waovu.
12 Mambo yote yalikuwa mazuri, lakini alinivunjavunja;
amenikamata shingo na kuniponda.
Amenifanya mimi kuwa shabaha yake;
13 wapiga upinde wake wananizunguka.
Bila huruma, huchoma figo zangu,
na kuimwaga nyongo yangu juu ya nchi.
14 Huniponda tena na tena;
hunishambulia kama shujaa wa vita.
 
15 “Nimejishonea nguo ya gunia juu ya mwili wangu
nami nimekizika kipaji cha uso wangu kwenye vumbi.
16 Uso wangu umekuwa mwekundu kwa kulia,
macho yangu yamepigwa na giza kuu.
17 Hata hivyo mikono yangu haijafanya jeuri,
na maombi yangu ni safi.
 
18 “Ee nchi, usiifunike damu yangu,
nacho kilio changu kisinyamazishwe kamwe.
19 Hata sasa shahidi wangu yuko mbinguni;
wakili wangu yuko juu.
20 Mwombezi wangu ni rafiki yangu
macho yangu yamwagapo machozi kwa Mungu;
21 kwa niaba ya mtu anamsihi Mungu
kama mtu anavyosihi kwa ajili ya rafiki yake.
 
22 “Ni miaka michache tu itapita
kabla sijaenda safari ambayo sitarudi.