Sehemu Ya Pili: Mazungumzo Ya Ayubu Na Rafiki Zake Watatu
3
(Ayubu 3–31)
Hotuba Ya Kwanza Ya Ayubu
Ayubu Anazungumza
Baada ya jambo hili, Ayubu akafumbua kinywa chake na kuilaani siku ya kuzaliwa kwake.
Kisha akasema:
“Siku ya kuzaliwa kwangu na ipotelee mbali,
nao usiku ule iliposemekana,
‘Mtoto wa kiume amezaliwa!’
Siku ile na iwe giza;
Mungu juu na asiiangalie;
nayo nuru isiiangazie.
Giza na kivuli kikuu kiikalie tena;
wingu na likae juu yake;
weusi na uifunike nuru yake.
Usiku ule na ushikwe na giza kuu;
usihesabiwe katika siku za mwaka,
wala usihesabiwe katika siku za mwezi wowote.
Usiku ule na uwe tasa;
sauti ya furaha na isisikike ndani yake.
Wale wazilaanio siku wailaani hiyo siku,
wale walio tayari kumwamsha Lewiathani.*
Nyota zake za alfajiri na ziwe giza;
nao ungojee mwanga bila mafanikio,
wala usiuone mwonzi wa kwanza
wa mapambazuko,
10 kwa sababu huo usiku haukunifungia
mlango wa tumbo la mama yangu,
ili kuyaficha macho yangu
kutokana na taabu.
 
11 “Kwa nini sikuangamia wakati wa kuzaliwa?
Kwa nini sikufa nilipokuwa ninatoka tumboni?
12 Kwa nini pakawa na magoti ya kunipokea
na matiti ili nipate kunyonyeshwa?
13 Kwa maana sasa ningekuwa nimepumzika kwa amani.
Ningekuwa nimelala na kupumzika
14 pamoja na wafalme na washauri wa dunia,
waliojijengea mahali ambapo sasa ni magofu,
15 pamoja na watawala waliokuwa na dhahabu,
waliozijaza nyumba zao kwa fedha.
16 Au kwa nini sikufichwa ardhini kama mtoto aliyezaliwa mfu,
kama mtoto mchanga ambaye kamwe hakuuona mwanga?
17 Huko waovu huacha kusumbua
na huko waliochoka hupumzika.
18 Wafungwa nao hufurahia utulivu wao,
hawasikii tena sauti ya kukemea ya kiongozi wa watumwa.
19 Wadogo na wakubwa wamo humo,
na mtumwa ameachiwa huru kutoka kwa bwana wake.
 
20 “Mbona nuru inawaangazia wale walio taabuni,
na hao wenye uchungu kupewa uhai,
21 wale wanaotamani kifo ambacho hakiji,
wale watafutao kufa zaidi ya kutafuta hazina iliyofichwa,
22 ambao hujawa na furaha,
na hushangilia wafikapo kaburini?
23 Kwa nini uhai hupewa mtu
ambaye njia yake imefichika,
ambaye Mungu amemzungushia boma?
24 Kwa maana kulia kwangu kwa uchungu kwanijia badala ya chakula;
kusononeka kwangu kunamwagika kama maji.
25 Lile nililokuwa naliogopa limenijia;
lile nililokuwa ninalihofia limenipata.
26 Sina amani, wala utulivu;
sina pumziko, bali taabu tu.”
* 3:8 Lewiathani ni mnyama mkubwa wa baharini mwenye magamba anayefanana na joka kubwa, mwenye umbo la kutisha, asiyeweza kuvuliwa.