Sehemu Ya Nne: Mungu Anazungumza
38
(Ayubu 38–41)
Bwana Anamjibu Ayubu
Kisha Bwana akamjibu Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli. Akasema:
“Nani huyu atiaye mashauri yangu giza
kwa maneno yasiyo na maarifa?
Jikaze kama mwanaume;
nitakuuliza swali,
nawe unijibu.
 
“Ulikuwa wapi nilipoweka misingi ya dunia?
Niambie, kama unafahamu.
Ni nani aliyeweka alama vipimo vyake?
Hakika wewe unajua!
Ni nani aliyenyoosha kamba ya kupimia juu yake?
Je, misingi yake iliwekwa juu ya nini,
au ni nani aliyeweka jiwe la pembeni,
wakati nyota za asubuhi zilipoimba pamoja,
na malaika wote walipokuwa wakipiga kelele kwa furaha?
 
“Ni nani aliyeifungia bahari milango
ilipopasuka kutoka tumbo,
nilipoyafanya mawingu kuwa vazi lake,
na kuyafungia katika giza nene,
10 nilipoamuru mipaka yake,
na kuiweka milango yake na makomeo mahali pake,
11 niliposema, ‘Unaweza kufika mpaka hapa wala si zaidi;
hapa ndipo mawimbi yako yenye kiburi yatakapokomea’?
 
12 “Umepata kuiamrisha asubuhi ipambazuke,
au kuyaonyesha mapambazuko mahali pake,
13 yapate kushika miisho ya dunia,
na kuwakungʼuta waovu waliomo?
14 Dunia hubadilika kama udongo wa mfinyanzi chini ya lakiri;
sura yake hukaa kama ile ya vazi.
15 Waovu huzuiliwa nuru yao,
nao mkono wao ulioinuliwa huvunjwa.
 
16 “Je, umepata kufika kwenye chemchemi za bahari?
Au kutembea mahali pa ndani pa vilindi?
17 Umewahi kuonyeshwa malango ya mauti?
Umewahi kuiona milango ya uvuli wa mauti?
18 Je, wewe unafahamu ukubwa wa dunia?
Niambie kama unajua haya yote.
 
19 “Njia ya kufika kwenye makao ya nuru ni ipi?
Nako maskani mwa giza ni wapi?
20 Je, unaweza kuvirudisha kwenye makao yake?
Unajua njia za kufika maskani mwake?
21 Hakika unajua, kwa kuwa ulikuwa umeshazaliwa!
Kwani umeishi miaka mingi!
 
22 “Je, umeshawahi kuingia katika ghala za theluji,
au kuona ghala za mvua ya mawe,
23 ambazo nimeziweka akiba kwa ajili ya wakati wa taabu,
na kwa ajili ya wakati wa vita na mapigano?
24 Ni ipi njia iendayo mahali umeme wa radi unapotawanyiwa,
au mahali upepo wa mashariki unaposambaziwa juu ya dunia?
25 Ni nani aliyepasua mifereji kwa ajili ya maji mengi ya mvua yaendayo kasi
na njia ya umeme wa radi,
26 ili kusababisha mvua kunyeshea mahali pasipokaliwa na mtu,
jangwa lisilo na yeyote ndani yake,
27 ili kuitosheleza nchi ya ukiwa na jangwa,
na majani yaanze kumea ndani yake?
28 Je, mvua ina baba?
Ni nani baba azaaye matone ya umande?
29 Barafu inatoka tumbo la nani?
Ni nani azaaye ukungu kutoka mbinguni,
30 wakati maji yawapo magumu kama jiwe,
wakati uso wa vilindi vya maji unapoganda?
 
31 “Je, waweza kuufunga mnyororo wa Kilimia?
Waweza kulegeza kamba za Orioni?
32 Waweza kuyaongoza makundi ya nyota kwa majira yake,
au kuongoza Dubu na watoto wake?
33 Je, unajua sheria zinazotawala mbingu?
Waweza kuweka utawala wa Mungu duniani?
 
34 “Waweza kuiinua sauti yako mpaka mawinguni,
na kujifunika mwenyewe na gharika ya maji?
35 Je, wewe hutuma umeme wa radi kwenye njia zake?
Je, hutoa taarifa kwako kukuambia, ‘Sisi tuko hapa’?
36 Ni nani aliyeujalia moyo hekima
au kuzipa akili ufahamu?
37 Nani mwenye hekima ya kuyahesabu mawingu?
Ni nani awezaye kuinamisha magudulia ya mbinguni
38 wakati mavumbi yawapo magumu,
na mabonge ya udongo kushikamana pamoja?
 
39 “Je, utamwindia simba jike mawindo,
na kuwashibisha simba wenye njaa
40 wakati wao wamejikunyata mapangoni mwao,
au wakivizia kichakani?
41 Ni nani ampaye kunguru chakula
wakati makinda yake yanamlilia Mungu,
yakizungukazunguka kwa ajili ya kukosa chakula?