40
Bwana akamwambia Ayubu:
“Je, mwenye kushindana na Mwenyezi aweza kumsahihisha?
Mwenye kumlaumu Mungu na ajibu.”
Ndipo Ayubu akamjibu Bwana:
“Mimi sistahili kabisa: ninawezaje kukujibu wewe?
Nauweka mkono wangu juu ya kinywa changu.
Nimesema mara moja, lakini sina jibu;
naam, nimesema mara mbili,
lakini sitasema tena.”
Ndipo Bwana akasema na Ayubu kutoka upepo wa kisulisuli:
“Jikaze kama mwanaume;
nitakuuliza maswali, nawe yakupasa unijibu.
 
“Je, utabatilisha hukumu yangu?
Utanilaumu mimi ili kujihesabia haki mwenyewe?
Je, una mkono kama wa Mungu,
nawe waweza kutoa sauti ya ngurumo kama yake?
10 Basi jivike mwenyewe utukufu na fahari,
nawe uvae heshima na enzi.
11 Fungulia ukali wa ghadhabu yako,
mtafute kila mwenye kiburi umshushe,
12 mwangalie kila mtu mwenye kiburi na umnyenyekeze,
waponde waovu mahali wasimamapo.
13 Wazike wote mavumbini pamoja;
wafunge nyuso zao kaburini.
14 Ndipo mimi mwenyewe nitakukubalia
kuwa mkono wako mwenyewe wa kuume unaweza kukuokoa.
 
15 “Mwangalie mnyama aitwaye Behemothi,*
niliyemuumba kama nilivyokuumba wewe,
anayekula majani kama ngʼombe.
16 Tazama basi nguvu alizo nazo kwenye viuno vyake,
uwezo alio nao kwenye misuli ya tumbo lake!
17 Mkia wake hutikisika kama mwerezi;
mishipa ya mapaja yake imesukwa pamoja.
18 Mifupa yake ni bomba za shaba,
maungo yake ni kama fito za chuma.
19 Yeye ni wa kwanza miongoni mwa kazi za Mungu,
lakini Muumba wake anaweza kumsogelea kwa upanga wake.
20 Vilima humletea yeye mazao yake,
nao wanyama wote wa porini hucheza karibu naye.
21 Hulala chini ya mimea ya yungiyungi,
katika maficho ya matete kwenye matope.
22 Hiyo mimea ya yungiyungi humficha kwenye vivuli vyake;
miti mirefu karibu na kijito humzunguka.
23 Wakati mto ufurikapo, yeye hapati mshtuko wa hofu;
yeye yu salama, hata kama Yordani ingefurika hadi kwenye kinywa chake.
24 Je, mtu yeyote anaweza kumkamata yeye akiwa macho,
au kumnasa kwa mtego na kutoboa pua yake?
 
* 40:15 Huyu alikuwa mnyama wa nyakati za zamani ambaye hajulikani hasa ni gani.