7
Ayubu: Mateso Yangu Hayana Mwisho
“Je, mwanadamu hana kazi ngumu duniani?
Siku zake si kama zile za mtu aliyeajiriwa?
Kama mtumwa anavyovionea shauku vivuli vya jioni,
au mtu aliyeajiriwa anavyoungojea mshahara wake,
ndivyo nilivyogawiwa miezi ya ubatili,
nami nimeandikiwa huzuni usiku hata usiku.
Wakati nilalapo ninawaza, ‘Itachukua muda gani kabla sijaamka?’
Usiku huwa mrefu, nami najigeuzageuza hadi mapambazuko.
Mwili wangu umevikwa mabuu na uchafu,
ngozi yangu imetumbuka na kutunga usaha.
Ayubu Anamlilia Mungu
“Siku zangu zinapita upesi kuliko mtande wa kufuma,
nazo zinafikia mwisho wake bila matumaini.
Kumbuka, Ee Mungu, maisha yangu ni kama pumzi;
macho yangu kamwe hayataona tena raha.
Lile jicho linaloniona sasa halitaniona tena;
utanitafuta, wala sitakuwepo.
Kama vile wingu liondokavyo na kutoweka,
vivyo hivyo yeye ashukaye kaburini* harudi tena.
10 Kamwe harudi tena nyumbani mwake;
wala mahali pake hapatamjua tena.
 
11 “Kwa hiyo sitanyamaza;
nitanena kutokana na maumivu makuu ya roho yangu,
nitalalama kwa uchungu wa nafsi yangu.
12 Je, mimi ni bahari, au mnyama mkubwa mno akaaye vilindini,
hata uniweke chini ya ulinzi?
13 Ninapofikiri kwamba kitanda changu kitanifariji,
nacho kiti changu cha fahari kitapunguza malalamiko yangu,
14 ndipo wanitisha kwa ndoto
na kunitia hofu kwa maono,
15 hivyo ninachagua kujinyonga na kufa,
kuliko huu mwili wangu.
16 Ninayachukia maisha yangu; nisingetamani kuendelea kuishi.
Niache; siku zangu ni ubatili.
 
17 “Mwanadamu ni kitu gani hata umjali kiasi hiki,
kwamba unamtia sana maanani,
18 kwamba unamwangalia kila asubuhi
na kumjaribu kila wakati?
19 Je, hutaacha kamwe kunitazama,
au kuniacha japo kwa kitambo kidogo tu?
20 Ikiwa nimetenda dhambi, nimekufanyia nini,
Ewe mlinzi wa wanadamu?
Kwa nini umeniweka niwe shabaha yako?
Je, nimekuwa mzigo kwako?
21 Kwa nini husamehi makosa yangu
na kuachilia dhambi zangu?
Kwa kuwa hivi karibuni nitalala mavumbini;
nawe utanitafuta, wala sitakuwepo.”
* 7:9 Kaburini hapa maana yake ni Kuzimu, kwa Kiebrania ni Sheol.