2
Maombi Ya Yona Katika Tumbo La Nyangumi
1 Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake.
2 Akasema:
“Katika shida yangu nalimwita Bwana,
naye akanijibu.
Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada,
nawe ukasikiliza kilio changu.
3 Ulinitupa kwenye kilindi,
ndani kabisa ya moyo wa bahari,
mikondo ya maji ilinizunguka,
mawimbi yako yote na viwimbi
vilipita juu yangu.
4 Nikasema, ‘Nimefukuziwa
mbali na uso wako,
hata hivyo nitatazama tena
kuelekea Hekalu lako takatifu.’
5 Maji yaliyonimeza yalinitisha,
kilindi kilinizunguka;
mwani ulijisokota kichwani pangu.
6 Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima,
makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele.
Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni,
Ee Bwana Mungu wangu.
7 “Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka,
nilikukumbuka wewe, Bwana,
nayo maombi yangu yalikufikia wewe,
katika Hekalu lako takatifu.
8 “Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa
hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao.
9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani,
nitakutolea dhabihu.
Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza.
Wokovu watoka kwa Bwana.”
10 Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.