15
Yesu Mbele Ya Pilato
(Mathayo 27:1-14; Luka 23:1-5; Yohana 18:28-38)
1 Asubuhi na mapema, viongozi wa makuhani, pamoja na wazee, walimu wa sheria na Baraza lote, wakafikia uamuzi. Wakamfunga Yesu, wakamchukua na kumkabidhi kwa Pilato.
2 Pilato akamuuliza, “Je, wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?”
Yesu akajibu, “Wewe umesema.”
3 Viongozi wa makuhani wakamshtaki kwa mambo mengi.
4 Pilato akamuuliza tena, “Je, huna la kujibu? Tazama ni mashtaka mangapi wanayaleta juu yako.”
5 Lakini Yesu hakujibu lolote, hivyo Pilato akashangaa.
Pilato Amtoa Yesu Asulubiwe
(Mathayo 27:15-26; Luka 23:13-25; Yohana 18:39–19:16)
6 Ilikuwa desturi wakati wa Sikukuu ya Pasaka kumfungulia mfungwa yeyote ambaye watu wangemtaka.
7 Wakati huo, mtu aliyeitwa Baraba alikuwa amefungwa gerezani pamoja na waasi wengine waliokuwa wametekeleza uuaji wakati wa maasi.
8 Ule umati wa watu ukamjia Pilato na kumwomba awafanyie kama ilivyokuwa desturi yake.
9 Pilato akawauliza, “Mnataka niwafungulie huyu Mfalme wa Wayahudi?”
10 Kwa maana yeye alitambua kuwa viongozi wa makuhani walikuwa wamemtia Yesu mikononi mwake kwa ajili ya wivu.
11 Lakini viongozi wa makuhani wakauchochea ule umati wa watu wamwombe awafungulie Baraba badala yake.
12 Pilato akawauliza tena, “Basi mnataka nifanye nini na huyu mtu mnayemwita Mfalme wa Wayahudi?”
13 Wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe!”
14 Pilato akawauliza, “Kwa nini? Amefanya kosa gani?”
Lakini wao wakapiga kelele kwa nguvu zaidi, wakisema, “Msulubishe!”
15 Pilato, akitaka kuuridhisha ule umati wa watu, akawafungulia Baraba. Naye baada ya kuamuru Yesu achapwe mijeledi, akamtoa ili asulubishwe.
Askari Wamdhihaki Yesu
(Mathayo 27:27-31; Yohana 19:2-3)
16 Askari wakampeleka Yesu hadi kwenye ukumbi wa ndani wa jumba la kifalme, ndio Praitorio, wakakusanya kikosi kizima cha askari.
17 Wakamvalisha Yesu joho la zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani.
18 Wakaanza kumsalimu kwa dhihaka, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!”
19 Wakampiga kwa fimbo ya mwanzi tena na tena kichwani na kumtemea mate. Wakapiga magoti mbele yake, wakamsujudia kwa kumdhihaki.
20 Walipokwisha kumdhihaki, wakamvua lile joho la zambarau, wakamvika tena nguo zake. Kisha wakamtoa nje ili wakamsulubishe.
Kusulubiwa Kwa Yesu
(Mathayo 27:32-44; Luka 23:26-43; Yohana 19:17-27)
21 Mtu mmoja kutoka Kirene, jina lake Simoni, baba yao Aleksanda na Rufo, alikuwa anapita zake kuingia mjini kutoka shamba, nao wakamlazimisha kuubeba ule msalaba.
22 Kisha wakampeleka Yesu mpaka mahali palipoitwa Golgotha (maana yake ni Mahali pa Fuvu la Kichwa).
23 Nao wakampa divai iliyochanganywa na manemane, lakini hakuinywa.
24 Basi wakamsulubisha, nazo nguo zake wakagawana miongoni mwao kwa kuzipigia kura ili kuamua ni gani kila mtu ataichukua.
25 Ilikuwa yapata saa tatu asubuhi walipomsulubisha.
26 Tangazo likaandikwa la mashtaka dhidi yake lenye maneno haya: “Mfalme wa Wayahudi.”
27 Pamoja naye walisulubiwa wanyangʼanyi wawili, mmoja upande wake wa kuume na mwingine upande wa kushoto. [
28 Nayo maandiko yakatimizwa, yale yasemayo, “Alihesabiwa pamoja na watenda dhambi.]”
29 Watu waliokuwa wakipita njiani wakamtukana huku wakitikisa vichwa vyao na kusema, “Aha! Wewe ambaye utalivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu,
30 basi shuka kutoka msalabani na ujiokoe mwenyewe!”
31 Vivyo hivyo, viongozi wa makuhani pamoja na walimu wa sheria wakamdhihaki miongoni mwao wakisema, “Aliwaokoa wengine, lakini hawezi kujiokoa mwenyewe!
32 Basi huyu Kristo, huyu Mfalme wa Israeli, ashuke sasa kutoka msalabani, ili tupate kuona na kuamini.” Wale waliosulubiwa pamoja naye pia wakamtukana.
Kifo Cha Yesu Msalabani
(Mathayo 27:45-56; Luka 23:44-49; Yohana 19:28-30)
33 Ilipofika saa sita, giza liliifunika nchi yote hadi saa tisa.
34 Mnamo saa tisa, Yesu akapaza sauti, akalia, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” (maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”)
35 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama karibu waliposikia hayo, wakasema, “Msikieni, anamwita Eliya.”
36 Mtu mmoja akaenda mbio, akachovya sifongo kwenye siki, akaiweka kwenye mwanzi na akampa Yesu ili anywe, akisema, “Basi mwacheni. Hebu tuone kama Eliya atakuja kumshusha kutoka hapo msalabani.”
37 Kisha Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho.
38 Pazia la Hekalu likachanika vipande viwili kuanzia juu hadi chini.
39 Basi yule jemadari aliyekuwa amesimama hapo mbele ya msalaba wa Yesu aliposikia ile sauti yake na kuona jinsi alivyokata roho, akasema, “Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu!”
40 Walikuwepo pia wanawake waliokuwa wakiangalia kwa mbali. Miongoni mwao walikuwepo Maria Magdalene, na Maria mama yao Yakobo mdogo na Yose, pia na Salome.
41 Hawa walifuatana na Yesu na kushughulikia mahitaji yake alipokuwa Galilaya. Pia walikuwepo wanawake wengine wengi waliokuwa wamekuja pamoja naye Yerusalemu.
Maziko Ya Yesu
(Mathayo 27:57-61; Luka 23:50-56; Yohana 19:38-42)
42 Ilipofika jioni, kwa kuwa ilikuwa Siku ya Maandalizi, yaani siku moja kabla ya Sabato,
43 Yosefu wa Arimathaya, mtu aliyeheshimiwa katika Baraza, na ambaye alikuwa anautarajia Ufalme wa Mungu, akamwendea Pilato kwa ujasiri na kumwomba mwili wa Yesu.
44 Pilato alikuwa akijiuliza kama Yesu alikuwa amekwisha kufa. Hivyo akamwita yule jemadari, akamuuliza iwapo Yesu alikuwa amekwisha kufa.
45 Baada ya kupata habari kutoka kwa yule jemadari kwamba kweli amekwisha kufa, Pilato akampa Yosefu ruhusa ya kuuchukua huo mwili.
46 Hivyo Yosefu akanunua kitambaa cha kitani safi, akaushusha mwili kutoka msalabani, akaufunga katika kile kitambaa cha kitani, na kuuweka ndani ya kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kwenye ingilio la kaburi.
47 Maria Magdalene na Maria mamaye Yose walipaona mahali pale alipolazwa.