Zaburi 115
Mungu Mmoja Wa Kweli
1 Sio kwetu sisi, Ee Bwana, sio kwetu sisi,
bali utukufu ni kwa jina lako,
kwa sababu ya upendo
na uaminifu wako.
2 Kwa nini mataifa waseme,
“Yuko wapi Mungu wao?”
3 Mungu wetu yuko mbinguni,
naye hufanya lolote limpendezalo.
4 Lakini sanamu zao ni za fedha na dhahabu,
zilizotengenezwa kwa mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa, lakini haziwezi kusema,
zina macho, lakini haziwezi kuona;
6 zina masikio, lakini haziwezi kusikia,
zina pua, lakini haziwezi kunusa;
7 zina mikono, lakini haziwezi kupapasa,
zina miguu, lakini haziwezi kutembea;
wala koo zao haziwezi kutoa sauti.
8 Wale wanaozitengeneza watafanana nazo,
vivyo hivyo wale wote wanaozitumainia.
9 Ee nyumba ya Israeli, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
10 Ee nyumba ya Aroni, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
11 Ninyi mnaomcha, mtumainini Bwana,
yeye ni msaada na ngao yao.
12 Bwana anatukumbuka na atatubariki:
ataibariki nyumba ya Israeli,
ataibariki nyumba ya Aroni,
13 atawabariki wale wanaomcha Bwana,
wadogo kwa wakubwa.
14 Bwana na awawezeshe kuongezeka,
ninyi na watoto wenu.
15 Mbarikiwe na Bwana
Muumba wa mbingu na dunia.
16 Mbingu zilizo juu sana ni mali ya Bwana,
lakini dunia amempa mwanadamu.
17 Sio wafu wanaomsifu Bwana,
wale washukao mahali pa kimya,
18 bali ni sisi tunaomtukuza Bwana,
sasa na hata milele.
Msifuni Bwana.