17
Yehoshafati Mfalme Wa Yuda
1 Yehoshafati mwanawe akawa mfalme baada yake na akajiimarisha dhidi ya Israeli.
2 Akaweka jeshi katika miji yote ya Yuda yenye ngome na kuweka askari walinzi katika Yuda na katika miji ya Efraimu ile ambayo baba yake Asa alikuwa ameiteka.
3 Bwana Mungu alikuwa na Yehoshafati kwa sababu katika miaka yake ya mwanzoni alienenda katika njia za Daudi baba yake. Hakutafuta Mabaali
4 bali alimtafuta Mungu wa baba yake na kuzifuata amri zake badala ya kufuata desturi za watu wa Israeli.
5 Kwa hiyo Bwana akauimarisha ufalme chini ya uongozi wake, nao Yuda wote wakamletea Yehoshafati zawadi, hivyo akawa na utajiri mwingi na heshima.
6 Moyo wake ukawa hodari katika njia za Bwana na zaidi ya yote, akaondoa mahali pa juu pa kuabudia miungu na nguzo za Maashera katika Yuda.
7 Katika mwaka wa tatu wa utawala wa akatuma maafisa wake ambao ni: Ben-Haili, Obadia, Zekaria, Nethaneli na Mikaya ili kufundisha katika miji ya Yuda.
8 Pamoja nao walikuwepo Walawi fulani nao ni: Shemaya, Nethania, Zebadia, Asaheli, Shemiramothi, Yehonathani, Adoniya, Tobia, Tob-Adonia, pamoja nao walikuwepo makuhani Elishama na Yehoramu.
9 Wakafundisha Yuda yote, wakiwa wamechukua Kitabu cha Sheria ya Bwana wakazunguka miji yote ya Yuda na kufundisha watu.
10 Hofu ya Bwana ikawa juu ya falme zote za nchi zilizozunguka Yuda, hivyo hawakufanya vita na Yehoshafati.
11 Baadhi ya Wafilisti wakamletea Yehoshafati zawadi na fedha kama ushuru, nao Waarabu wakamletea mifugo: kondoo dume 7,700 na mbuzi 7,700.
12 Yehoshafati akaendelea kupata nguvu zaidi na zaidi, akajenga ngome na miji ya hazina katika Yuda
13 na akawa na wingi mkubwa wa vitu katika miji ya Yuda. Pia aliweka askari wa vita wenye uzoefu huko Yerusalemu.
14 Wakaandikishwa katika jamaa zao kama ifuatavyo:
Kutoka Yuda, majemadari wa vikosi vya elfu:
Jemadari Adna akiwa na askari wa vita 300,000;
15 aliyefuata ni jemadari Yehohanani, akiwa na askari 280,000 walio tayari kwa vita;
16 aliyefuata ni Amasia mwana wa Zikri, ambaye alijitolea kwa ajili ya kazi ya Bwana, akiwa na askari 200,000.
17 Kutoka Benyamini:
Eliada, askari shujaa akiwa na watu 200,000 wenye silaha za nyuta na ngao;
18 aliyefuata ni Yehozabadi, akiwa na askari 180,000 wenye silaha za vita.
19 Hawa ndio waliomtumikia mfalme, mbali na wale mfalme aliweka katika miji yenye ngome huko Yuda yote.