27
Yothamu Mfalme Wa Yuda
(2 Wafalme 15:32-38)
1 Yothamu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita. Mama yake aliitwa Yerusha binti Sadoki.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana kama Uzia baba yake alivyokuwa amefanya, lakini tofauti na yeye, hakuingilia huduma za hekaluni mwa Bwana. Lakini hata hivyo, watu wakaendelea na desturi zao mbaya.
3 Yothamu akajenga upya Lango la Juu la Hekalu la Bwana na kufanya kazi kubwa kwenye ukuta katika kilima cha Ofeli.
4 Akajenga miji katika vilima vya Yuda pamoja na ngome na minara mwituni.
5 Yothamu akafanya vita na mfalme wa Waamoni na kumshinda. Mwaka ule Waamoni wakamlipa talanta 100 za fedha, kori 10,000 za ngano na kori 10,000 za shayiri. Waamoni wakamletea kiasi hicho hicho mwaka wa pili na wa tatu.
6 Yothamu akaendelea kuwa na nguvu kwa sababu alienenda kwa ukamilifu mbele za Bwana Mungu wake.
7 Matukio mengine ya utawala wa Yothamu, pamoja na vita vyake vyote na vitu vingine alivyofanya, vimeandikwa katika kitabu cha wafalme wa Israeli na Yuda.
8 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na sita.
9 Yothamu akalala na baba zake na akazikwa katika Mji wa Daudi. Naye Ahazi mwanawe akawa mfalme baada yake.