3
Solomoni Ajenga Hekalu
(1 Wafalme 6:1-38; 7:15-22)
Ndipo Solomoni akaanza kujenga Hekalu la Bwana katika Yerusalemu juu ya Mlima Moria, pale ambapo Bwana alikuwa amemtokea Daudi baba yake. Ilikuwa katika kiwanja cha kupuria cha Arauna,* Myebusi, mahali palipotolewa na Daudi. Alianza kujenga siku ya pili ya mwezi wa pili katika mwaka wa nne wa utawala wake.
Msingi aliouweka Solomoni kwa ajili ya kulijenga Hekalu la Mungu ulikuwa urefu wa dhiraa sitini na upana dhiraa ishirini. Ukumbi wa mbele wa Hekalu ulikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, yaani, kuanzia upande mmoja hadi upande mwingine wa upana wa nyumba hiyo na kimo chake dhiraa thelathini.§
Akaufunika ndani kwa dhahabu safi. Akaufunika ukumbi mkuu kwa mbao za miberoshi na kufunikwa kwa dhahabu safi na kuupamba kwa miti ya mitende na kuifanyizia kwa minyororo. Alilipamba Hekalu kwa vito vya thamani. Hiyo dhahabu aliyotumia ilikuwa dhahabu ya Parvaimu. Akazifunika boriti za dari, miimo na vizingiti vya milango, kuta na milango ya Hekalu kwa dhahabu, naye akatia nakshi ya makerubi kwenye kuta.
Akajenga Patakatifu pa Patakatifu, urefu na upana wake ulikuwa dhiraa ishirini, sawasawa na upana wa Hekalu. Alifunika ndani kwa talanta 120* za dhahabu safi. Misumari ya dhahabu ilikuwa na uzito wa shekeli hamsini. Alivifunika pia vyumba vya juu kwa dhahabu.
10 Katika sehemu ya Patakatifu pa Patakatifu akafanyiza jozi moja ya makerubi ya kuchongwa na kuyafunika kwa dhahabu. 11 Urefu wa mabawa ya hao makerubi ulikuwa jumla ya dhiraa ishirini. Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano, nalo liligusa ukuta wa Hekalu, bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano, ambalo liligusa bawa la kerubi lingine. 12 Vivyo hivyo bawa moja la kerubi wa pili lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na liligusa ukuta mwingine wa pili wa Hekalu na bawa lake lingine, lilikuwa pia na urefu wa dhiraa tano nalo liligusa bawa la kerubi wa kwanza. 13 Mabawa ya makerubi hawa yalitanda dhiraa ishirini. Walisimama kwa miguu yao, nyuso zao zikielekea ukumbi mkubwa.
14 Akatengeneza pazia la nyuzi za rangi ya buluu, zambarau na nyekundu, na za kitani safi, na kutarizi makerubi juu yake.
15 Mbele ya Hekalu Solomoni akatengeneza nguzo mbili, ambazo kwa pamoja zilikuwa na dhiraa thelathini na tano kwenda juu kwake, na urefu wa kila moja ilikuwa na taji juu yake yenye dhiraa tano. 16 Akatengeneza minyororo iliyosokotwa, na kuiweka juu ya zile nguzo. Pia akatengeneza makomamanga 100, na kuyashikamanisha kwenye minyororo. 17 Akazisimamisha hizo nguzo mbele ya Hekalu, moja upande wa kusini na nyingine upande wa kaskazini. Ile moja ya upande wa kusini akaiita Yakini,§ na ya upande wa kaskazini akaiita Boazi.*
* 3:1 Pia anaitwa Ornani kwa Kiebrania. 3:3 Dhiraa 60 ni sawa na mita 27. 3:3 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9. § 3:4 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5. * 3:8 Talanta 120 za dhahabu ni sawa na tani 23. 3:9 Shekeli 50 za dhahabu ni sawa na gramu 600. 3:11 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25. § 3:17 Yakini maana yake Atathibitisha. * 3:17 Boazi maana yake Imo nguvu.