20
Daudi Na Yonathani
1 Kisha Daudi akakimbia kutoka Nayothi huko Rama akamwendea Yonathani na kumuuliza, “Kwani nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemkosea baba yako kwa jinsi gani, hata kwamba anajaribu kuuondoa uhai wangu?”
2 Yonathani akajibu, “La hasha! Hutakufa! Tazama, baba yangu hafanyi kitu chochote, kikubwa au kidogo, bila kuniambia mimi. Kwa nini anifiche hili? Sivyo ilivyo!”
3 Lakini Daudi akaapa na kusema, “Baba yako anajua kabisa kwamba nimepata kibali mbele yako, naye amesema moyoni mwake, ‘Yonathani sharti asilijue hili, la sivyo atahuzunika.’ Lakini kweli kama Bwana aishivyo na kama uishivyo, kuna hatua moja tu kati yangu na mauti.”
4 Yonathani akamwambia Daudi, “Chochote unachotaka nifanye, nitakufanyia.”
5 Basi Daudi akamwambia, “Angalia, kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo, nami inanipasa kula chakula pamoja na mfalme; lakini niache niende kujificha shambani mpaka kesho kutwa.
6 Kama baba yako akiona ya kuwa sipo, mwambie, ‘Daudi aliniomba sana ruhusa kuwahi Bethlehemu, mji wake wa nyumbani, kwa sababu dhabihu ya mwaka inafanywa huko kwa ajili ya ukoo wake wote.’
7 Kama akisema, ‘Ni vyema sana,’ basi mtumishi wako yu salama. Lakini kama akikasirika, unaweza kuwa na hakika kwamba anakusudia kunidhuru.
8 Lakini kwa habari yako wewe, mtende wema mtumishi wako, kwa sababu mmeingia kwenye agano pamoja naye mbele za Bwana. Kama nina hatia, basi niue wewe mwenyewe! Kwa nini unikabidhi kwa baba yako?”
9 Yonathani akasema, “La hasha! Kama ningekuwa na kidokezo kidogo kwamba baba yangu amekusudia kukudhuru wewe, je, nisingekuambia?”
10 Daudi akamuuliza, “Je, nani atakayeniambia kama baba yako atakujibu kwa ukali?”
11 Yonathani akamwambia, “Njoo, twende shambani.” Basi wakaenda huko pamoja.
12 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Ninakuahidi kwa jina la Bwana, Mungu wa Israeli, hakika nitamchunguza baba yangu wakati kama huu kesho kutwa! Kama ameweka utaratibu wa kufaa kukuhusu wewe, je, sitakutumia ujumbe na kukufahamisha?
13 Lakini ikiwa baba yangu amenuia kukudhuru, Bwana na anishughulikie kwa ukali, iwapo sitakufahamisha na kukuaga uende salama. Bwana na awe pamoja nawe kama alivyokuwa pamoja na baba yangu.
14 Lakini nitendee wema usiokoma kama ule wa Bwana siku zote za maisha yangu, ili nisije nikauawa,
15 wala usiuondoe wema wako kwa jamaa yangu, hata kama ni wakati ule Bwana atakapokuwa amekatilia mbali kila adui wa Daudi kutoka kwenye uso wa dunia.”
16 Basi Yonathani akafanya agano na nyumba ya Daudi, akisema: “Bwana na awaangamize adui za Daudi.”
17 Naye Yonathani akamtaka Daudi athibitishe tena kiapo chake cha kumpenda, kwa sababu Yonathani alimpenda Daudi kama nafsi yake mwenyewe.
18 Kisha Yonathani akamwambia Daudi, “Kesho ni sikukuu ya Mwezi Mwandamo. Itajulikana kwamba haupo kwa kuwa kiti chako kitakuwa hakina mtu.
19 Kesho kutwa, inapokaribia jioni, nenda mahali pale ulipojificha wakati tatizo hili lilipoanza na usubiri karibu na jiwe la Ezeli.
20 Nitapiga mishale mitatu kando yake, kama kwamba nilikwenda kulenga shabaha.
21 Kisha nitamtuma mvulana na kumwambia, ‘Nenda ukaitafute mishale.’ Kama nikimwambia, ‘Tazama mishale iko upande huu wako! Uilete hapa,’ basi uje, kwa sababu hakika kama Bwana aishivyo, wewe ni salama, hakuna hatari.
22 Lakini kama nikimwambia huyo mvulana, ‘Angalia, mishale iko mbele yako,’ basi inakupasa uondoke, kwa sababu Bwana amekuruhusu uende zako.
23 Kuhusu yale tuliyozungumza wewe na mimi: kumbuka, Bwana ndiye shahidi kati yako wewe na mimi milele.”
24 Basi Daudi akajificha shambani, na sikukuu ya Mwezi Mwandamo ilipowadia, mfalme akaketi ili ale.
25 Akaketi mahali pake pa kawaida karibu na ukuta, kuelekeana na Yonathani, naye Abneri akaketi karibu na Mfalme Sauli, lakini kiti cha Daudi kilikuwa wazi.
26 Sauli hakusema chochote siku ile kwa kuwa alifikiri, “Kuna kitu cha lazima kimetokea kwa Daudi ambacho kimemfanya najisi asihudhurie karamuni, hakika yeye yu najisi.”
27 Lakini siku iliyofuata, siku ya pili ya mwezi, kiti cha Daudi kilikuwa wazi tena. Kisha Sauli akamwambia mwanawe Yonathani, “Kwa nini mwana wa Yese hajaja chakulani jana wala leo?”
28 Yonathani akamjibu, “Daudi alinisihi sana nimpe ruhusa aende Bethlehemu.
29 Alisema, ‘Niruhusu niende, kwa sababu jamaa yetu wana dhabihu mjini, na ndugu yangu ameniagiza niwepo huko. Kama nimepata kibali mbele yako, niruhusu niende kuona ndugu zangu.’ Hii ndiyo sababu hakuja mezani pa mfalme.”
30 Hasira ya Sauli ikawaka dhidi ya Yonathani na kumwambia, “Wewe mwana wa mwanamke mkaidi na mwasi! Je, sijui kuwa umekuwa upande wa mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe na kwa aibu ya mama yako aliyekuzaa?
31 Maadamu mwana wa Yese angali anaishi katika dunia hii wewe wala ufalme wako hautasimama. Sasa tuma aitwe umlete kwangu, kwa kuwa ni lazima afe!”
32 Yonathani akamuuliza baba yake, “Kwa nini auawe? Kwani amefanya nini?”
33 Lakini Sauli akamtupia Yonathani mkuki wake kwa nguvu ili amuue. Hapo ndipo Yonathani alipotambua kwamba baba yake alikusudia kumuua Daudi.
34 Yonathani akainuka kutoka mezani kwa hasira kali. Siku ile ya pili ya mwezi hakula chakula, kwa kuwa alikuwa amehuzunishwa na vitendo vya aibu ambavyo baba yake alikuwa anamtendea Daudi.
35 Kesho yake asubuhi Yonathani alikwenda shambani kukutana na Daudi. Alikuwa amefuatana na mvulana mdogo,
36 naye Yonathani akamwambia yule mvulana, “Kimbia ukatafute mishale nitakayorusha.” Mvulana alipokuwa akikimbia, akarusha mishale mbele yake.
37 Yule mvulana alipofika mahali pale ambapo mshale wa Yonathani ulipokuwa umeanguka, Yonathani akamwita, “Je, mshale hauko mbele yako?”
38 Yonathani akampigia kelele, “Harakisha, nenda haraka! Usisimame!” Mvulana akaokota mshale na kurudi kwa bwana wake.
39 (Mvulana hakujua chochote juu ya hayo yote; Yonathani na Daudi tu ndio waliojua.)
40 Basi Yonathani akampa yule mvulana silaha zake na kumwambia, “Nenda, zirudishe mjini.”
41 Baada ya mvulana kwenda, Daudi akainuka kutoka upande wa kusini wa lile jiwe, naye akasujudu uso wake mpaka nchi mara tatu mbele ya Yonathani. Kisha kila mmoja akambusu mwenzake, wakalia pamoja. Lakini Daudi akalia zaidi.
42 Yonathani akamwambia Daudi, “Nenda kwa amani, kwa kuwa tumeapiana kiapo cha urafiki kati yetu kwa jina la Bwana, tukisema, ‘Bwana ndiye shahidi kati yako na mimi, na kati ya wazao wako na wazao wangu milele.’ ” Kisha Daudi akaondoka, naye Yonathani akarudi mjini.