18
Kifo Cha Absalomu
1 Daudi akakusanya watu aliokuwa nao na kuweka majemadari wa maelfu na majemadari wa mamia.
2 Daudi akatuma vikosi vya askari: theluthi moja ilikuwa chini ya amri ya Yoabu, theluthi ya pili chini ya Abishai mwana wa Seruya nduguye Yoabu, na theluthi ya tatu chini ya Itai, Mgiti. Mfalme akaviambia vikosi, “Hakika mimi mwenyewe nitakwenda pamoja nanyi.”
3 Lakini watu wakasema, “Haikupasi kwenda, ikiwa sisi tutalazimika kukimbia, wao hawatatujali. Hata kama nusu yetu tukifa hawatajali, lakini wewe una thamani ya watu kama sisi kumi elfu. Ingekuwa bora zaidi kwako basi kutupatia msaada kutoka mjini.”
4 Mfalme akajibu, “Nitafanya lolote linaloonekana jema zaidi kwenu.”
Kwa hiyo mfalme akasimama kando ya lango wakati watu wote wakitoka nje kwa makundi ya mamia na maelfu.
5 Mfalme akawaamuru Yoabu, Abishai na Itai, “Kuweni wapole kwa kijana Absalomu kwa ajili yangu.” Vikosi vyote vikasikia mfalme akitoa amri kwa kila jemadari kumhusu Absalomu.
6 Jeshi likatoka kwenda kwenye uwanja wa vita kupigana na Israeli, hivyo vita vikapiganwa katika msitu wa Efraimu.
7 Huko jeshi la Israeli likashindwa na watu wa Daudi, siku hiyo majeruhi walikuwa wengi kiasi cha watu ishirini elfu.
8 Vita vikaenea nchi nzima, watu wengi zaidi wakifia msituni siku hiyo kuliko waliouawa kwa upanga.
9 Basi ikawa Absalomu alikutana na watu wa Daudi. Yeye alikuwa amepanda nyumbu wake, naye nyumbu alipopita chini ya matawi yaliyosongana ya mwaloni mkubwa, kichwa cha Absalomu kilinaswa kwenye mti. Akaachwa akiningʼinia hewani, wakati nyumbu aliyekuwa amempanda aliendelea kwenda.
10 Mmojawapo wa wale watu alipoona, akamwambia Yoabu, “Nimemwona Absalomu akiningʼinia kwenye mti wa mwaloni.”
11 Yoabu akamwambia huyo mtu, “Nini! Ulimwona Absalomu? Kwa nini hukumpiga papo hapo mpaka chini? Ndipo ningekupa shekeli kumi za fedha na mkanda wa askari shujaa.”
12 Lakini huyo mtu akamjibu Yoabu, “Hata kama ningepimiwa shekeli 1,000 mikononi mwangu, nisingeinua mkono wangu dhidi ya mwana wa mfalme. Tukiwa tunasikia, mfalme alikuagiza wewe na Abishai pamoja na Itai, akisema, ‘Mlindeni kijana Absalomu kwa ajili yangu.’
13 Nami kama ningekuwa nimemtendea kwa hila, na hakuna lolote linalofichika kwa mfalme, wewe mwenyewe ungejitenga nami.”
14 Yoabu akasema, “Mimi sitapoteza muda hapa pamoja nawe.” Hivyo akachukua mikuki mitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu nayo moyoni alipokuwa angali hai akiningʼinia katika ule mwaloni.
15 Nao wabeba silaha kumi wa Yoabu wakamzunguka Absalomu, wakampiga na kumuua.
16 Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, navyo vikosi vikaacha kuwafuata Israeli, kwa maana Yoabu aliwasimamisha.
17 Wakamchukua Absalomu, wakamtupa katika shimo kubwa huko msituni na kulundika lundo kubwa la mawe juu yake. Huko nyuma, Waisraeli wote wakakimbilia nyumbani kwao.
18 Wakati wa uhai wa Absalomu alikuwa amechukua nguzo na kuisimamisha katika Bonde la Mfalme, kwa maana alifikiri, “Sina mwana atakayeendeleza kumbukumbu ya jina langu.” Akaita nguzo hiyo kwa jina lake mwenyewe. Nayo inaitwa Mnara wa Ukumbusho wa Absalomu mpaka leo.
Daudi Aomboleza Kifo Cha Absalomu
19 Basi Ahimaasi mwana wa Sadoki akasema, “Niruhusu mimi nikimbie na kumpelekea mfalme habari kwamba Bwana amemwokoa mfalme kutoka mikononi mwa adui zake.”
20 Yoabu akamwambia Ahimaasi, “Leo si wewe utakayepeleka habari. Unaweza kupeleka habari wakati mwingine, lakini leo haikupasi kupeleka, kwa sababu mwana wa mfalme amekufa.”
21 Ndipo Yoabu akamwambia mtu mmoja Mkushi, “Nenda, ukamwambie mfalme kile ulichoona.” Mkushi akasujudu mbele ya Yoabu akaondoka mbio.
22 Ahimaasi mwana wa Sadoki akamwambia tena Yoabu, “Liwalo na liwe, tafadhali niruhusu nikimbie nyuma ya huyo Mkushi.”
Lakini Yoabu akajibu, “Mwanangu, mbona wataka kwenda? Wewe huna habari yoyote itakayokupa tuzo.”
23 Ahimaasi akasema, “Liwalo na liwe, nataka kukimbia.”
Kwa hiyo Yoabu akamwambia, “Haya, kimbia!” Ndipo Ahimaasi akakimbia kufuata njia ya kupitia tambarare, akafika kabla ya huyo Mkushi.
24 Wakati Daudi alipokuwa ameketi kati ya lango la ndani na la nje, mlinzi akapanda juu ya paa la lango kupitia ukutani. Alipotazama nje, akaona mtu mmoja akikimbia peke yake.
25 Mlinzi akampazia mfalme sauti na kumpa taarifa.
Mfalme akasema, “Ikiwa yuko peke yake, lazima atakuwa na habari njema.” Naye yule mtu akazidi kusogea karibu.
26 Kisha mlinzi akaona mtu mwingine anakuja akikimbia, akamwita bawabu, “Tazama, mtu mwingine anakuja akikimbia peke yake!”
Mfalme akasema, “Lazima atakuwa analeta habari njema pia.”
27 Mlinzi akasema, “Ninaona kuwa yule wa kwanza anakimbia kama Ahimaasi mwana wa Sadoki.”
Mfalme akasema, “Yeye ni mtu mwema. Analeta habari njema.”
28 Ndipo Ahimaasi akamwita mfalme, akasema, “Mambo yote ni mema!” Akasujudu mbele ya mfalme uso wake mpaka ardhini, akasema, “Ahimidiwe Bwana Mungu wako! Yeye aliyewatoa watu wale walioinua mikono yao dhidi ya mfalme bwana wangu.”
29 Mfalme akauliza, “Je, huyo kijana Absalomu yuko salama?”
Ahimaasi akajibu, “Kulikuwa na machafuko mengi mara tu Yoabu alipokuwa anataka kumtuma mtumishi wa mfalme pamoja nami mtumishi wako, lakini sijui ilikuwa nini?”
30 Mfalme akasema, “Simama kando na usubiri hapa.” Basi akasogea kando na kusimama hapo.
31 Ndipo huyo Mkushi akawasili na kusema, “Mfalme bwana wangu, sikia habari njema! Leo Bwana amekuokoa kutoka kwa wale wote walioinuka dhidi yako.”
32 Mfalme akamuuliza huyo Mkushi, “Je, kijana Absalomu yuko salama?”
Huyo Mkushi akajibu, “Adui wa mfalme bwana wangu na wote wale walioinuka kukudhuru na wawe kama huyo kijana.”
33 Mfalme akatetemeka. Akapanda chumbani juu kupitia langoni akilia. Alipokuwa akienda, akasema, “Ee mwanangu Absalomu! Mwanangu, mwanangu Absalomu! Laiti ningekufa badala yako: Ee Absalomu, mwanangu, mwanangu!”