20
Sheba Aasi Dhidi Ya Daudi
1 Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti,
“Hatuna fungu katika Daudi,
wala hatuna sehemu
katika mwana wa Yese!
Kila mtu aende hemani mwake,
enyi Israeli!”
2 Kwa hiyo watu wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini watu wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani mpaka Yerusalemu.
3 Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kuangalia jumba la kifalme na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane mpaka kifo chao.
4 Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite watu wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.”
5 Lakini Amasa alipokwenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
6 Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara zaidi kuliko alivyofanya Absalomu. Wachukue watu wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.”
7 Hivyo watu wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na wapiganaji mashujaa wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
8 Wakati walikuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kwenye kiuno wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka kwenye ala.
9 Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu.
10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!”
12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani mpaka kwenye shamba na kutupia nguo juu yake.
13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walijikusanya pamoja na kumfuata.
15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumhusuru Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wanagongagonga ukuta ili kuubomoa na kuuangusha chini,
16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.”
17 Yoabu alikwenda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?”
Akamjibu, “Ndiye mimi.”
Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri.
19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Bwana?”
20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu.
21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Nikabidhini mtu huyu mmoja, nami nitajiondoa katika mji huu.”
Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani kwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;
24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;
25 Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
26 na Ira, Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.