6
Marafiki
Mpenzi wako amekwenda wapi,
ewe mzuri kupita wanawake wote?
Mpenzi wako amegeukia njia ipi,
tupate kumtafuta pamoja nawe?
Mpendwa
Mpenzi wangu amekwenda bustanini mwake,
kwenye vitalu vya vikolezo,
kujilisha bustanini
na kukusanya yungiyungi.
Mimi ni wake mpenzi wangu,
na mpenzi wangu ni wangu;
yeye hujilisha katikati ya yungiyungi.
 
Shairi La Tano
Mpenzi
Wewe ni mzuri, mpenzi wangu, kama Tirsa,
upendezaye kama Yerusalemu,
umetukuka kama jeshi lenye bendera.
Uyageuze macho yako mbali nami,
yananigharikisha.
Nywele zako ni kama kundi la mbuzi
wanaoteremka kutoka Gileadi.
Meno yako ni kama kundi la kondoo
watokao kuogeshwa.
Kila mmoja ana pacha lake,
hakuna hata mmoja aliye peke yake.
Mashavu yako nyuma ya shela yako
ni kama vipande viwili vya komamanga.
Panaweza kuwepo malkia sitini,
masuria themanini
na mabikira wasiohesabika;
lakini hua wangu, mkamilifu wangu,
ni wa namna ya pekee,
binti pekee kwa mama yake,
kipenzi cha yeye aliyemzaa.
Wanawali walimwona na kumwita aliyebarikiwa;
malkia na masuria walimsifu.
Marafiki
10 Ni nani huyu atokeaye kama mapambazuko,
mzuri kama mwezi, mwangavu kama jua,
ametukuka kama nyota zifuatanazo?
Mpenzi
11 Niliteremka kwenye bustani ya miti ya milozi
ili kutazama machipuko ya bondeni,
kuona kama mizabibu imechipua
au kama mikomamanga imechanua maua.
12 Kabla sijangʼamua,
shauku yangu iliniweka
katikati ya magari ya kifalme ya kukokotwa na farasi ya watu wangu.
Marafiki
13 Rudi, rudi, ee Mshulami;
rudi, rudi ili tupate kukutazama!
Mpenzi
Kwa nini kumtazama Mshulami,
kama kutazama ngoma ya Mahanaimu?*
 
* 6:13 Mahanaimu hapa ina maana ya majeshi mawili.