6
Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako
1 Haya ndio maagizo, amri na sheria ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliniagiza niwafundishe ninyi ili mpate kuyashika katika nchi ambayo ninyi mnavuka Yordani kuimiliki,
2 ili ninyi, watoto wenu na watoto wao baada yao wamche Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, siku zote kwa kushika amri na maagizo yake yote ninayowapa, ili mweze kuyafurahia maisha marefu.
3 Sikia, ee Israeli, nawe uwe mwangalifu kutii ili upate kufanikiwa na kuongezeka sana katika nchi inayotiririka maziwa na asali, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu, alivyowaahidi ninyi.
4 Sikia, ee Israeli: Mwenyezi Mungu, Mungu wako, Mwenyezi Mungu ni mmoja.
5 Mpende Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote.
6 Amri hizi ninazokupa leo zitakuwa katika moyo wako.
7 Wafundishe watoto wako kwa bidii. Nena kuhusu amri hizi uketipo nyumbani na wakati utembeapo njiani, ulalapo na uamkapo.
8 Zifunge kama alama juu ya mkono wako, na uzifunge juu ya paji la uso wako.
9 Ziandike kwenye miimo ya milango ya nyumba yako na juu ya malango yako.
10 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapokuleta katika nchi aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, Isaka na Yakobo, kukupa wewe, nchi kubwa, yenye miji inayopendeza ambayo hukuijenga,
11 nyumba zilizojaa vitu vizuri vya aina nyingi ambavyo hukuvijaza, visima ambavyo hukuchimba, na mashamba ya mizabibu na mizeituni ambayo hukupanda wewe, basi, utakapokula na kushiba,
12 jihadhari usije ukamwacha Mwenyezi Mungu, aliyekutoa katika nchi ya Misri, kutoka nchi ya utumwa.
13 Utamcha Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na umtumikie yeye peke yake na kuapa kwa jina lake.
14 Usifuate miungu mingine, miungu ya mataifa yanayokuzunguka;
15 kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ambaye yuko katikati yako, ni Mungu mwenye wivu na hasira yake itawaka dhidi yako, naye atakuangamiza kutoka uso wa nchi.
16 Usimjaribu Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kama ulivyomjaribu huko Masa.
17 Utayashika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa bidii, na masharti na amri alizokupa.
18 Fanya lililo haki na jema mbele za Mwenyezi Mungu, ili upate kufanikiwa, uweze kuingia na kuimiliki nchi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu aliahidi kwa kiapo kwa baba zako,
19 kuwafukuza kwa nguvu adui zako mbele yako kama Mwenyezi Mungu alivyosema.
20 Siku zijazo, mtoto wako atakapokuuliza, “Ni nini maana ya masharti haya, amri na sheria hizi ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, alikuagiza wewe?”
21 Mwambie: “Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri, lakini Mwenyezi Mungu alitutoa sisi kutoka Misri kwa mkono wenye nguvu.
22 Machoni petu, Mwenyezi Mungu alitenda ishara za miujiza na maajabu makubwa na ya kutisha mno dhidi ya Misri, na dhidi ya Farao na nyumba yake yote.
23 Lakini Mungu akatutoa huko, akatuleta na kutupatia nchi hii ambayo aliwaahidi baba zetu kwa kiapo.
24 Mwenyezi Mungu akatuagiza tutii amri hizi zote na kumcha Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ili tupate kustawi na kuendelea kuwa hai kama ilivyo leo.
25 Tukizitii kwa bidii amri hizi zote mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kama alivyotuamuru sisi, hiyo itakuwa haki yetu.”