24
Isaka na Rebeka
Wakati huu Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, naye Mwenyezi Mungu alikuwa amembariki katika mambo yote. Ibrahimu akamwambia mtumishi wake mkuu katika nyumba yake, aliyekuwa msimamizi wa mali yake yote, “Weka mkono wako chini ya paja langu. Ninataka uape kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke kutoka binti za Wakanaani, ambao ninaishi miongoni mwao. Bali nenda katika nchi yangu na jamaa zangu umpatie Isaka mwanangu mke.”
Yule mtumishi akamuuliza, “Je, itakuwaje huyo mwanamke akikataa kuja nami katika nchi hii? Je, nimrudishe mwanao katika hiyo nchi uliyotoka?”
Ibrahimu akasema, “Hakikisha kwamba hutamrudisha mwanangu huko. Mwenyezi Mungu, Mungu wa mbingu, alinitoa nyumbani mwa baba yangu na nchi yangu niliyozaliwa. Ndiye alisema nami na akaniahidi kwa kiapo, akasema, ‘Nitawapa uzao wako nchi hii.’ Yeye atatuma malaika wake akutangulie ili umtwalie mwanangu mke kutoka huko. Huyo mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi utafunguliwa kutoka kiapo nilichokuapisha. Ila usimrudishe mwanangu huko.” Basi yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la bwana wake Ibrahimu, akamwapia kuhusu shauri hili.
10 Ndipo huyo mtumishi akachukua ngamia kumi miongoni mwa ngamia wa bwana wake, akaondoka, akiwa amechukua aina zote za vitu vizuri kutoka kwa bwana wake. Akaelekea Mesopotamia, akaenda hadi mji wa Nahori. 11 Akawapigisha ngamia magoti karibu na kisima cha maji nje ya mji; ilikuwa inaelekea jioni, wakati wanawake huteka maji.
12 Kisha akaomba, “Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nipatie ushindi leo, uoneshe ukarimu kwa bwana wangu Ibrahimu. 13 Tazama, nimesimama karibu na kisima hiki cha maji, nao binti za watu wa mji huu wanakuja kuteka maji. 14 Basi na iwe hivi, nitakapomwambia binti mmoja, ‘Tafadhali tua mtungi wako nipate kunywa maji’; naye akisema, ‘Kunywa, nitawanywesha na ngamia wako pia’: basi na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka. Kwa hili nitajua umemtendea bwana wangu ukarimu.”
15 Ikawa kabla hajamaliza kuomba, Rebeka akatokea akiwa na mtungi begani mwake. Alikuwa binti Bethueli. Bethueli alikuwa mwana wa Milka, aliyekuwa mke wa Nahori ndugu wa Ibrahimu. 16 Huyu msichana alikuwa mzuri sana wa sura, bikira, ambaye hakuna mwanaume aliyekuwa amekutana naye kimwili. Aliteremka kisimani, akajaza mtungi wake, tena akapanda juu.
17 Ndipo yule mtumishi akaharakisha kukutana naye, akamwambia, “Tafadhali nipe maji kidogo katika mtungi wako.”
18 Yule msichana akasema, “Kunywa, bwana wangu.” Akashusha kwa haraka mtungi mkononi mwake na akampa, akanywa.
19 Baada ya kumpa yule mtumishi yale maji, akamwambia, “Nitawatekea ngamia wako maji pia hadi wote watosheke.” 20 Akafanya haraka kumimina maji kwenye birika ya kunyweshea wanyama, akakimbia kisimani kuteka maji mengine, na akateka ya kuwatosha ngamia wake wote. 21 Pasipo kusema neno, yule mtumishi akamtazama kwa makini aone kama Mwenyezi Mungu ameifanikisha safari yake, au la.
22 Ikawa ngamia walipokwisha kunywa wote, yule mtumishi akampa huyo msichana pete ya puani ya dhahabu yenye uzito wa beka moja*, na bangili mbili za dhahabu zenye uzito wa shekeli kumi. 23 Kisha akamuuliza, “Wewe ni binti ya nani? Tafadhali niambie. Je, kuna nafasi katika nyumba ya baba yako tunapoweza kulala?”
24 Yule msichana akamjibu, “Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Milka aliyemzalia Nahori.” 25 Akaendelea kusema, “Kwetu kuna majani mengi na malisho, tena kuna nafasi kwa ajili yenu kulala.”
26 Yule mtumishi akasujudu na kumwabudu Mwenyezi Mungu, 27 akisema, “Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuondoa wema na uaminifu wake kwa bwana wangu. Mimi nami, Mwenyezi Mungu ameniongoza safarini, akanifikisha nyumbani kwa jamaa za bwana wangu.”
28 Yule msichana akakimbia, akawaeleza watu wa nyumbani mwa mama yake kuhusu mambo haya. 29 Rebeka alikuwa na kaka aliyeitwa Labani; huyo akaharakisha kukutana na yule mtumishi kule kisimani. 30 Mara alipoiona ile pete puani, na bangili mikononi mwa dada yake, na kusikia yale maneno Rebeka aliyoambiwa na huyo mtumishi, alimwendea huyo mtumishi, akamkuta amesimama karibu na ngamia wake pale karibu na kisima. 31 Akamwambia, “Karibu nyumbani wewe uliyebarikiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa nini unasimama huko nje? Mimi nimekuandalia nyumba na mahali kwa ajili ya ngamia.”
32 Hivyo yule mtumishi akaingia nyumbani, nayo mizigo ikaondolewa juu ya ngamia. Majani na malisho yakaletwa kwa ajili ya ngamia, na maji kwa ajili yake na watu wake ili kunawa miguu. 33 Ndipo chakula kikaandaliwa kwa ajili yake, lakini akasema, “Sitakula hadi niwe nimewaambia yale niliyo nayo ya kusema.”
Labani akasema, “Basi tuambie.”
34 Hivyo akasema, “Mimi ni mtumishi wa Ibrahimu. 35 Mwenyezi Mungu amembariki sana bwana wangu, amekuwa tajiri. Amempa kondoo na ng’ombe, fedha na dhahabu, watumishi wa kiume na wa kike, ngamia na punda. 36 Sara mkewe bwana wangu amemzalia mwana katika uzee wake, naye amempa kila kitu alichokuwa nacho. 37 Naye bwana wangu ameniapisha na akasema, ‘Kamwe usimtwalie mwanangu mke katika binti za Wakanaani, ambao ninaishi katika nchi yao, 38 ila uende hadi kwa jamaa ya baba yangu na ukoo wangu mwenyewe, ukamtwalie mwanangu mke huko.’
39 “Kisha nikamuuliza bwana wangu, ‘Je, kama huyo mwanamke hatakubali kurudi nami?’
40 “Akanijibu, ‘Mwenyezi Mungu, ambaye nimetembea mbele zake, atatuma malaika wake pamoja nawe, na kuifanikisha safari yako, ili uweze kupata mke kwa ajili ya mwanangu katika ukoo wangu na kutoka jamaa ya baba yangu. 41 Kisha, utakapoenda kwenye ukoo wangu, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu. Hata wakikataa kukupa huyo binti, utakuwa umefunguliwa kutoka kiapo changu.’
42 “Nilipokuja kisimani leo nilisema, ‘Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ikikupendeza, naomba uifanikishe safari niliyoijia. 43 Tazama, ninasimama kando ya kisima hiki. Mwanamwali akija kuteka maji, nami nikimwambia: Tafadhali niruhusu ninywe maji kidogo kutoka mtungi wako. 44 Naye akiniambia, “Kunywa, nami nitawatekea ngamia wako maji pia,” basi huyo awe ndiye mke Mwenyezi Mungu amemchagulia mwana wa bwana wangu.’
45 “Kabla sijamaliza kuomba moyoni mwangu, Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani, akateka maji, nami nikamwambia, ‘Tafadhali nipe maji ninywe.’
46 “Akafanya haraka kushusha mtungi wake begani na kusema, ‘Kunywa, na nitawanywesha ngamia wako pia.’ Basi nikanywa, naye akawanywesha na ngamia pia.
47 “Nikamuuliza, ‘Wewe ni binti ya nani?’
“Akasema, ‘Mimi ni binti ya Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia.’
“Ndipo nilipotia pete puani mwake na bangili mikononi mwake, 48 nikasujudu na nikamwabudu Mwenyezi Mungu. Nikamtukuza Mwenyezi Mungu, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza katika njia sahihi ili nimtwalie mwana na bwana wangu mke katika jamaa zake. 49 Ikiwa mtaonesha wema na uaminifu kwa bwana wangu, mniambie; la sivyo, mniambie, ili niweze kujua njia ya kugeukia.”
50 Labani na Bethueli wakajibu, “Jambo hili limetoka kwa Mwenyezi Mungu; hatuwezi kukuambia jambo lolote baya au jema. 51 Rebeka yuko hapa, mchukue na uende, awe mke wa mwana wa bwana wako, sawasawa na Mwenyezi Mungu alivyoongoza.”
52 Ikawa huyo mtumishi wa Ibrahimu aliposikia waliyosema, alisujudu, uso wake ukagusa chini mbele za Mwenyezi Mungu. 53 Ndipo huyo mtumishi akatoa vitu vilivyotengenezwa kwa dhahabu na kwa fedha, pamoja na mavazi, akampa Rebeka; pia akawapa zawadi za thamani kubwa nduguye na mamaye. 54 Kisha yeye na wale watu waliokuwa pamoja naye wakala, wakanywa na kulala palepale.
Walipoamka asubuhi, yule mtumishi akasema, “Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
55 Lakini ndugu yake Rebeka pamoja na mama yake wakajibu, “Acha binti akae kwetu siku kumi au zaidi, ndipo mwondoke.”
56 Lakini yule mtumishi akawaambia, “Msinicheleweshe, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amefanikisha safari yangu. Nipeni ruhusa nirudi kwa bwana wangu.”
57 Ndipo wakasema, “Acha tumwite huyo binti tumuulize, tusikie atakavyosema.” 58 Kwa hiyo wakamwita Rebeka na kumuuliza, “Je, utaenda na mtu huyu?”
Akasema, “Nitaenda.”
59 Hivyo wakamwaga ndugu yao Rebeka aondoke, pamoja na mjakazi wake, na mtumishi wa Ibrahimu na watu wake. 60 Wakambariki Rebeka, wakamwambia,
“Ndugu yetu, uwe wewe kumi elfu,
mara elfu nyingi;
nao wazao wako wamiliki
malango ya adui zao.”
61 Rebeka na vijakazi wake wakajiandaa, wakapanda ngamia wao, wakafuatana na yule mtu. Hivyo yule mtumishi akamchukua Rebeka, wakaondoka.
62 Basi Isaka alikuwa ametoka Beer-Lahai-Roi, kwa kuwa alikuwa akiishi nchi ya Negebu. 63 Isaka akaenda shambani kutafakari wakati wa jioni; alipoinua macho yake, akaona ngamia wanakuja. 64 Rebeka pia akainua macho, akamwona Isaka. Akashuka kutoka ngamia wake, 65 akamuuliza yule mtumishi, “Ni nani mtu yule kule shambani anayekuja kutulaki?”
Yule mtumishi akajibu, “Huyu ndiye bwana wangu.” Hivyo Rebeka akachukua shela yake, akajifunika.
66 Kisha yule mtumishi akamweleza Isaka mambo yote aliyoyatenda. 67 Isaka akamwingiza Rebeka katika hema la Sara mama yake. Isaka akamchukua Rebeka, hivyo akawa mke wake. Isaka akampenda; akafarijika baada ya kifo cha mama yake.
* 24:22 Beka moja ya dhahabu ni sawa na gramu 5.5. 24:22 Shekeli 10 za dhahabu ni sawa na gramu 110.