41
Ndoto za Farao
1 Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto. Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Naili,
2 wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye matete.
3 Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea Mto Naili, wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto.
4 Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.
5 Farao akaingia usingizini tena, akaota ndoto ya pili. Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja.
6 Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyokaushwa na upepo wa mashariki.
7 Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, na kumbe ilikuwa ndoto.
8 Kesho yake asubuhi, alifadhaika akilini. Hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.
9 Ndipo mnyweshaji mkuu alimwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kosa langu.
10 Farao alipowakasirikia watumishi wake, alinifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa walinzi.
11 Katika usiku mmoja, kila mmoja wetu aliota ndoto, na kila ndoto ilikuwa na maana yake.
12 Basi kuna kijana Mwebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, mtumishi wa mkuu wa walinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupatia kila mtu tafsiri ya ndoto yake.
13 Nayo mambo yakawa jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu, naye huyo mwingine akaangikwa.”
14 Basi, Farao akatuma Yusufu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake, akaenda mbele ya Farao.
15 Farao akamwambia Yusufu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia habari yako kwamba unapoelezwa ndoto unaweza kuifasiri.”
16 Yusufu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”
17 Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Naili.
18 Nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni, wakaja kujilisha kwenye matete.
19 Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri.
20 Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza.
21 Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.
22 “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja.
23 Baada ya hayo, masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki.
24 Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna yeyote aliyeweza kunifasiria.”
25 Ndipo Yusufu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto hiyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.
26 Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba; ni ndoto hiyo hiyo moja.
27 Ng’ombe saba waliokonda na wabaya waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki: Ni miaka saba ya njaa.
28 “Ni kama nilivyomwambia Farao. Mungu amemwonesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.
29 Miaka saba ya shibe inakuja katika nchi yote ya Misri,
30 lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo shibe yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.
31 “Shibe iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.
32 Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.
33 “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri.
34 Farao na aweke wasimamizi nchini kote, wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya shibe.
35 Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji.
36 Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”
Yusufu afanywa msimamizi wa Misri
37 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote.
38 Hivyo Farao akawauliza, “Je, tunaweza kumpata yeyote kama mtu huyu, aliye na Roho wa Mungu ndani yake?”
39 Ndipo Farao akamwambia Yusufu, “Maadamu Mungu amekufunulia haya yote, hakuna yeyote mwenye akili na hekima kama wewe.
40 Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”
41 Kwa hiyo Farao akamwambia Yusufu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.”
42 Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yusufu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43 Akampandisha katika gari lake la vita kama msaidizi wake; watu wakamtangulia wakipaza sauti na kusema, “Fungueni njia!” Ndivyo Farao alimweka Yusufu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.
44 Kisha Farao akamwambia Yusufu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.”
45 Farao akamwita Yusufu jina Safenath-Panea; pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yusufu akaitembelea nchi yote ya Misri.
46 Yusufu alikuwa na umri wa miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao, mfalme wa Misri. Naye Yusufu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri.
47 Katika ile miaka saba ya shibe nchi ilizaa mazao kwa wingi sana.
48 Yusufu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya shibe nchini Misri, akakihifadhi katika miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo.
49 Yusufu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari; ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi kipimo.
50 Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yusufu wana wawili wa kiume.
51 Yusufu akamwita mzaliwa wake wa kwanza jina Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.”
52 Mwana wa pili akamwita jina Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”
53 Ile miaka saba ya shibe huko Misri ikaisha,
54 nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yusufu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula.
55 Nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao aliwaagiza Wamisri wote, “Nendeni kwa Yusufu, nanyi mfanye anachowaambia.”
56 Njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yusufu akafungua maghala ya vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri.
57 Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yusufu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.