35
Furaha ya waliokombolewa
Jangwa na nchi kame vitafurahi;
nyika itashangilia na kuchanua maua.
Kama waridi, litachanua maua,
litashangilia sana na kupaza sauti kwa furaha.
Litapewa utukufu wa Lebanoni,
fahari ya Karmeli na Sharoni;
wataona utukufu wa Mwenyezi Mungu,
fahari ya Mungu wetu.
 
Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu,
yafanyeni imara magoti yaliyolegea,
waambieni wale wenye mioyo ya hofu,
“Kuweni hodari, msiogope;
tazama, Mungu wenu atakuja kulipa kisasi,
pamoja na ujira wake,
atakuja na kuwaokoa.”
 
Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa
na masikio ya viziwi yatazibuliwa.
Ndipo kilema atarukaruka kama kulungu,
nao ulimi wa aliye bubu utapaza sauti kwa shangwe.
Maji yatatiririka kwa kasi katika nyika,
na vijito katika jangwa.
Mchanga wa moto utakuwa bwawa la maji,
ardhi yenye kiu itabubujika chemchemi.
Maskani ya mbweha walikolala hapo awali
patamea nyasi, matete na mafunjo.
 
Nako kutakuwa na njia kuu,
nayo itaitwa Njia ya Utakatifu.
Wasio safi hawatapita juu yake;
itakuwa ya wale wanaotembea katika Njia Ile;
yeye asafiriye juu yake,
ajapokuwa mjinga, hatapotea.
Huko hakutakuwa na simba,
wala mnyama mkali hatapita njia hiyo;
hawatapatikana humo.
Ila waliokombolewa tu ndio watakaopita huko,
10 waliokombolewa na Mwenyezi Mungu watarudi.
Wataingia Sayuni wakiimba;
furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao.
Watapata furaha na shangwe;
huzuni na majonzi vitakimbia.