62
Jina jipya la Sayuni
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza,
kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia,
hadi haki yake itakapoangaza kama mapambazuko,
wokovu wake kama mwanga wa moto.
Mataifa wataona haki yako,
nao wafalme wote wataona utukufu wako;
wewe utaitwa kwa jina jipya
lile ambalo kinywa cha Mwenyezi Mungu kitatamka.
Utakuwa taji la fahari mkononi mwa Mwenyezi Mungu,
taji la kifalme mkononi mwa Mungu wako.
Hawatakuita tena Aliyeachwa,
wala nchi yako kuiita Ukiwa.
Bali utaitwa Hefsiba*,
nayo nchi yako itaitwa Beula,
kwa maana Mwenyezi Mungu atakufurahia,
nayo nchi yako itaolewa.
Kama vile kijana aoavyo mwanamwali,
ndivyo Mwashi wako atakavyokuoa;
kama bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi wake,
ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.
 
Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu,
hawatanyamaza mchana wala usiku.
Ninyi wenye kumwita Mwenyezi Mungu,
msitulie,
msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu
na kuufanya uwe sifa ya dunia.
 
Mwenyezi Mungu ameapa kwa mkono wake wa kuume
na kwa mkono wake wenye nguvu:
“Kamwe sitawapa tena adui zenu
nafaka zenu kama chakula chao;
kamwe wageni hawatakunywa tena
divai mpya ambayo mmeitaabikia,
lakini wale waivunao nafaka wataila
na kumsifu Mwenyezi Mungu,
nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake
katika nyua za patakatifu pangu.”
 
10 Piteni, piteni katika malango!
Tengenezeni njia kwa ajili ya watu.
Jengeni, jengeni njia kuu!
Ondoeni mawe.
Inueni bendera kwa ajili ya mataifa.
 
11 Mwenyezi Mungu ametoa tangazo
hadi miisho ya dunia:
“Mwambie Binti Sayuni,
‘Tazama, mwokozi wako anakuja!
Tazama ujira wake uko pamoja naye,
na malipo yake yanafuatana naye!’ ”
12 Wataitwa Watu Watakatifu,
Waliokombolewa na Mwenyezi Mungu;
nawe utaitwa Aliyetafutwa,
Mji Usioachwa Tena.
* 62:4 maana yake Yeye ninayemfurahia 62:4 maana yake Aliyeolewa 62:5 au ndivyo wanao watakavyokuoa wewe