49
Ujumbe kuhusu Amoni
Kuhusu Waamoni:
 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Je, Israeli hana wana?
Je, hana warithi?
Kwa nini basi Moleki amechukua milki ya Gadi?
Kwa nini watu wake wanaishi katika miji yake?
Lakini siku zinakuja,”
asema Mwenyezi Mungu,
“nitakapopiga ukelele wa vita
dhidi ya Raba, mji wa Waamoni;
utakuwa kilima cha magofu,
navyo vijiji vinavyouzunguka
vitateketezwa kwa moto.
Kisha Israeli atawafukuza
wale waliomfukuza,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Lia kwa huzuni, ee Heshboni, kwa kuwa Ai umeangamizwa!
Pigeni kelele, enyi wakazi wa Raba!
Vaeni gunia na kuomboleza,
kimbieni hapa na pale ndani ya kuta,
kwa kuwa Moleki ataenda uhamishoni,
yeye pamoja na makuhani na maafisa wake.
Kwa nini unajivunia mabonde yako,
kujivunia mabonde yako yaliyozaa sana?
Ee binti usiye mwaminifu,
unayeutumainia utajiri wako na kusema,
‘Ni nani atakayenishambulia?’
Nitaleta hofu kuu juu yako
kutoka kwa wale wote wanaokuzunguka,”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
“Kila mmoja wenu ataondolewa,
wala hakuna hata mmoja atakayekusanya wakimbizi.
 
“Lakini hatimaye,
nitarudisha mateka wa Waamoni,”
asema Mwenyezi Mungu.
Ujumbe kuhusu Edomu
Kuhusu Edomu:
 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Je, hakuna tena hekima katika Temani?
Je, shauri limewapotea wenye busara?
Je, hekima yao imechakaa?
Geuka na ukimbie, jifiche katika mapango marefu kabisa,
wewe uishiye Dedani,
kwa kuwa nitaleta maafa juu ya Esau
wakati nitakapomwadhibu.
Je, kama wachuma zabibu wangekuja kwako,
wasingebakiza zabibu chache?
Kama wezi wangekujia usiku,
je, si wangeiba tu kiasi ambacho wangehitaji?
10 Lakini nitamvua Esau nguo abaki uchi,
nitayafunua maficho yake,
ili asiweze kujificha.
Watoto wake, jamaa na majirani wataangamia,
naye hatakuwepo tena.
11 Waache yatima wako; nitayalinda maisha yao.
Wajane wako pia
wanaweza kunitumaini mimi.”
12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: “Kama wasiostahili kukinywea kikombe ni lazima wakinywe, kwa nini wewe usiadhibiwe? Hutakwepa kuadhibiwa, ni lazima ukinywe. 13 Ninaapa kwa nafsi yangu,” asema Mwenyezi Mungu, “kwamba Bosra utakuwa magofu na kitu cha kutisha, cha aibu na cha kulaania; miji yake yote itakuwa magofu milele.”
14 Nimesikia ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu:
Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,
“Jikusanyeni ili kuushambulia!
Inukeni kwa ajili ya vita!”
 
15 “Sasa nitakufanya mdogo miongoni mwa mataifa,
uliyedharauliwa miongoni mwa watu.
16 Vitisho vyako na kiburi cha moyo wako
vimekudanganya,
wewe unayeishi katika majabali ya miamba,
wewe unayedumu katika miinuko ya kilima.
Ujapojenga kiota chako juu sana kama cha tai,
nitakushusha chini kutoka huko,”
asema Mwenyezi Mungu.
17 “Edomu atakuwa kitu cha kutisha;
wote wapitao karibu
watashangaa na kuzomea
kwa sababu ya majeraha yake yote.
18 Kama vile Sodoma na Gomora zilivyoangamizwa,
pamoja na miji iliyokuwa jirani nayo,”
asema Mwenyezi Mungu,
“vivyo hivyo hakuna mtu yeyote atakayeishi humo.
Naam, hakuna mtu yeyote atakayekaa humo.
 
19 “Kama simba anayepanda kutoka vichaka vya Yordani
kuja kwenye nchi ya malisho mengi,
ndivyo nitakavyomfukuza Edomu kutoka nchi yake ghafula.
Ni nani aliye mteule nitakayemweka kwa ajili ya jambo hili?
Ni nani aliye kama mimi,
na ni nani awezaye kunipinga?
Tena ni mchungaji yupi awezaye
kusimama kinyume nami?”
20 Kwa hiyo, sikia kile Mwenyezi Mungu alichokipanga dhidi ya Edomu,
kile alichokusudia dhidi ya wale wanaoishi Temani:
Aliye mchanga katika kundi ataburutwa mbali;
yeye ataharibu kabisa malisho yao kwa sababu yao.
21 Kwa sauti ya anguko lao, dunia itatetemeka.
Kilio chao kitasikika hadi Bahari ya Shamu*.
22 Tazama! Tai atapaa juu angani na kuruka chini kwa ghafula,
akitandaza mabawa yake juu ya Bosra.
Katika siku hiyo, mioyo ya mashujaa wa Edomu
itakuwa kama moyo wa mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
Ujumbe kuhusu Dameski
23 Kuhusu Dameski:
“Hamathi na Arpadi imetahayarika,
kwa kuwa wamesikia habari mbaya.
Wamevunjika moyo na wametaabika
kama bahari iliyochafuka.
24 Dameski amedhoofika,
amegeuka na kukimbia,
hofu ya ghafula imemkamata sana;
amepatwa na uchungu na maumivu,
maumivu kama ya mwanamke katika uchungu wa kuzaa.
25 Kwa nini mji unaosifika haujaachwa,
mji wenye sifa, na wa furaha yangu?
26 Hakika, vijana wake wanaume wataanguka barabarani;
askari wake wote watanyamazishwa siku hiyo,”
asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.
27 “Nitatia moto kuta za Dameski;
utaangamiza ngome za Ben-Hadadi.”
Ujumbe kuhusu Kedari na Hazori
28 Kuhusu Kedari na falme za Hazori, ambazo Nebukadneza mfalme wa Babeli alizishambulia:
 
Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:
“Inuka, ushambulie Kedari
na kuwaangamiza watu wa mashariki.
29 Mahema yao na makundi yao ya kondoo yatachukuliwa;
vibanda vyao vitatwaliwa,
pamoja na mali yao yote na ngamia wao.
Watu watawapigia kelele,
‘Hofu kuu iko kila upande!’
 
30 “Kimbieni haraka!
Kaeni kwenye mapango marefu sana, ninyi mnaoishi Hazori,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Nebukadneza, mfalme wa Babeli amepanga njama dhidi yenu;
amebuni hila dhidi yenu.
 
31 “Inuka na ulishambulie taifa lililostarehe,
linaloishi kwa kujiamini,”
asema Mwenyezi Mungu,
“taifa lisilo na malango wala makomeo;
watu wake wanaishi peke yao.
32 Ngamia wao watakuwa nyara,
nayo mifugo yao itatekwa.
Walio maeneo ya mbali
nitawatawanya pande zote,
nami nitaleta maafa juu yao
kutoka kila upande,”
asema Mwenyezi Mungu.
33 “Hazori itakuwa makao ya mbweha,
mahali pa ukiwa milele.
Hakuna atakayeishi humo;
hakuna mtu atakayekaa ndani yake.”
Ujumbe kuhusu Elamu
34 Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu lililomjia nabii Yeremia kuhusu Elamu, mapema katika utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda:
 
35 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni:
“Tazama, nitavunja upinde wa Elamu,
ulio tegemeo la nguvu zao.
36 Nitaleta pepo nne dhidi ya Elamu
toka pande nne za mbingu,
nitawatawanya katika hizo pande nne,
wala hapatakuwa na taifa
ambalo watu wa Elamu waliofukuzwa
hawataenda.
37 Nitamfadhaisha Elamu mbele ya adui zao,
mbele yao wanaoutafuta uhai wao;
nitaleta maafa juu yao,
naam, hasira yangu kali,”
asema Mwenyezi Mungu.
“Nitawafuatia kwa upanga
hadi nitakapowamaliza.
38 Nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu
na kumwangamiza mfalme wake na maafisa wake,”
asema Mwenyezi Mungu.
 
39 “Lakini nitarudisha mateka wa Elamu
katika siku zijazo,”
asema Mwenyezi Mungu.
* 49:21 au Bahari ya Mafunjo