10
Wale waliotia muhuri walikuwa:
 
Nehemia mtawala, mwana wa Hakalia.
 
Sedekia, Seraya, Azaria, Yeremia,
Pashuri, Amaria, Malkiya,
Hatushi, Shebania, Maluki,
Harimu, Meremothi, Obadia,
Danieli, Ginethoni, Baruku,
Meshulamu, Abiya, Miyamini,
Maazia, Bilgai na Shemaya.
Hao walikuwa makuhani.
 
Walawi:
Yeshua mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadmieli,
10 na wenzao: Shebania,
Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani,
11 Mika, Rehobu, Hashabia,
12 Zakuri, Sherebia, Shebania,
13 Hodia, Bani na Beninu.
 
14 Viongozi wa watu:
Paroshi, Pahath-Moabu, Elamu, Zatu, Bani,
15 Buni, Azgadi, Bebai,
16 Adoniya, Bigwai, Adini,
17 Ateri, Hezekia, Azuri,
18 Hodia, Hashumu, Besai,
19 Harifu, Anathothi, Nebai,
20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri,
21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua,
22 Pelatia, Hanani, Anaya,
23 Hoshea, Hanania, Hashubu,
24 Haloheshi, Pilha, Shobeki,
25 Rehumu, Hashabna, Maaseya,
26 Ahia, Hanani, Anani,
27 Maluki, Harimu na Baana.
 
28 “Watu wengine wote, wakiwa ni makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji, watumishi wa Hekalu*, na wale wote waliojitenga na mataifa jirani kwa ajili ya Torati ya Mungu, pamoja na wake zao na wana wao wote wa kiume na wa kike waliokuwa na uwezo wa kufahamu, 29 basi hawa wote wanajiunga na ndugu zao na wakuu wao, na kujifunga kwa laana na kwa kiapo kufuata Torati ya Mungu iliyotolewa kupitia kwa Musa mtumishi wa Mungu, na kutii kwa uangalifu amri zote, maagizo na sheria za Mwenyezi Mungu, Bwana wetu.
30 “Tunaahidi kutowaoza binti zetu kwa watu wanaotuzunguka, wala kuwaoza wana wetu binti zao.
31 “Mataifa jirani wanapoleta bidhaa zao au nafaka kuuza siku ya Sabato, hatutazinunua kutoka kwao siku ya Sabato, wala siku nyingine yoyote takatifu. Kila mwaka wa saba, tutaacha kuilima ardhi na tutafuta madeni yote.
32 “Tunakubali wajibu wa kutimiza amri za kutoa theluthi ya shekeli kila mwaka kwa ajili ya utumishi wa nyumba ya Mungu: 33 Kwa ajili ya mikate ya Wonesho, kwa ajili ya sadaka za kawaida za nafaka na sadaka za kuteketezwa, kwa ajili ya sadaka za siku za Sabato, Sikukuu za Mwandamo wa Mwezi na sikukuu nyingine zilizoamriwa, kwa ajili ya sadaka takatifu, kwa ajili ya sadaka za dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli, na kwa ajili ya kazi zote za nyumba ya Mungu wetu.
34 “Sisi makuhani, Walawi na watu, tumepiga kura kuamua kuwa kila mmoja wa jamaa zetu lazima alete katika nyumba ya Mungu wetu kwa nyakati maalum kila mwaka mchango wa kuni za kukokea moto katika madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika Torati.
35 “Pia tunachukua wajibu wa kuleta malimbuko ya mazao yetu na matunda ya kwanza ya kila mti wa matunda katika nyumba ya Mwenyezi Mungu kila mwaka.
36 “Kama pia ilivyoandikwa katika Torati, tutawaleta wazaliwa wetu wa kwanza wa kiume, na wa mifugo yetu, yaani wa ng’ombe wetu na wa makundi yetu ya kondoo na mbuzi, katika nyumba ya Mungu wetu, kwa ajili ya makuhani wanaohudumu huko.
37 “Zaidi ya hayo, tutaleta katika maghala ya nyumba ya Mungu wetu, kwa makuhani, vyakula vya kwanza vya mashamba yetu, sadaka zetu za nafaka, matunda ya miti yetu yote, divai yetu mpya na mafuta. Nasi tutaleta zaka za mazao yetu kwa Walawi, kwa kuwa Walawi ndio ambao hukusanya zaka katika miji yote tunakofanya kazi. 38 Kuhani aliye wa uzao wa Haruni atashirikiana na Walawi wanapopokea zaka. Nao Walawi watapaswa kuleta sehemu ya kumi ya zaka katika maghala ya hazina yaliyo katika nyumba ya Mungu wetu. 39 Watu wa Israeli pamoja na Walawi itawapasa kuleta michango yao ya nafaka, divai mpya na mafuta katika vyumba vya ghala, mahali vifaa vya mahali patakatifu vinapohifadhiwa, na wanapokaa makuhani wanaohudumu, na mabawabu na waimbaji.
“Hatutaacha kuijali nyumba ya Mungu wetu.”
* 10:28 yaani Wanethini. 10:32 Theluthi ya shekeli hapa ni kama gramu 4.