32
Makabila ng’ambo ya Yordani
(Kumbukumbu 3:12-22)
1 Basi Wareubeni na Wagadi, waliokuwa na makundi makubwa ya ng’ombe, kondoo na mbuzi, waliona kuwa nchi ya Yazeri na nchi ya Gileadi ni nzuri kwa mifugo.
2 Hivyo walimjia Musa, na kuhani Eleazari na viongozi wa jumuiya, na kuwaambia,
3 “Atarothi, Diboni, Yazeri, Nimra, Heshboni, Eleale, Sebamu, Nebo na Beoni,
4 nchi ambayo Mwenyezi Mungu ameishinda mbele ya Waisraeli, inafaa kwa mifugo, nao watumishi wako wana mifugo.
5 Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, nchi hii na ipewe watumishi wako kama milki yetu. Usitufanye tuvuke Yordani.”
6 Musa akawaambia Wagadi na Wareubeni, “Je, watu wa nchi yenu wataenda vitani wakati ninyi mmeketi hapa?
7 Kwa nini mmewakatisha Waisraeli tamaa wasivuke katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu amewapa?
8 Hivi ndivyo baba zenu walivyofanya wakati nilipowatuma kutoka Kadesh-Barnea kuipeleleza nchi.
9 Baada ya kufika kwenye Bonde la Eshkoli na kuitazama nchi, waliwakatisha tamaa Waisraeli wasiingie katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amewapa.
10 Siku ile hasira ya Mwenyezi Mungu iliwaka naye akaapa kiapo hiki:
11 ‘Kwa kuwa hawakunifuata kwa moyo wote, hakuna mtu yeyote mwenye miaka ishirini au zaidi ambaye alikuja kutoka Misri atakayeona nchi niliyoahidi kwa kiapo kwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo;
12 hakuna hata mmoja isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni, kwa sababu walimfuata Mwenyezi Mungu kwa moyo wote.’
13 Hasira ya Mwenyezi Mungu iliwaka dhidi ya Waisraeli na akawafanya watangetange katika jangwa kwa miaka arobaini, hadi kizazi chote cha wale waliofanya maovu mbele yake kimeangamia.
14 “Nanyi mko hapa, uzao wa wenye dhambi, mkisimamia mahali pa baba zenu na mkimfanya Mwenyezi Mungu kuwakasirikia Waisraeli hata zaidi.
15 Mkigeuka na kuacha kumfuata, atawaacha tena watu hawa wote jangwani, na mtakuwa sababu ya maangamizi yao.”
16 Ndipo wakamjia Musa na kumwambia, “Tungetaka kujenga mazizi hapa kwa ajili ya mifugo yetu na miji kwa ajili ya wanawake wetu na watoto.
17 Lakini sisi tuko tayari kuchukua silaha zetu na kutangulia mbele ya Waisraeli hadi tutakapowaleta mahali pao. Wakati huo wanawake wetu na watoto wataishi katika miji yenye ngome, kwa ajili ya ulinzi dhidi ya wenyeji wa nchi.
18 Hatutarudi nyumbani mwetu hadi kila Mwisraeli apokee urithi wake.
19 Hatutapokea urithi wowote pamoja nao ng’ambo ya Yordani, kwa sababu urithi wetu umekuja kwetu upande wa mashariki mwa Yordani.”
20 Kisha Musa akawaambia, “Kama mtafanya jambo hili, kama mtajivika silaha mbele za Mwenyezi Mungu kwa ajili ya vita,
21 na kama ninyi nyote mtaenda mmejivika silaha ng’ambo ya Yordani mbele za Mwenyezi Mungu hadi awe amewafukuza adui zake mbele zake,
22 hadi wakati nchi itakapokuwa imeshindwa mbele za Mwenyezi Mungu, ndipo mtaweza kurudi na kuwa huru kutoka masharti yenu kwa Mwenyezi Mungu na Israeli. Nayo nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Mwenyezi Mungu.
23 “Lakini mkishindwa kufanya hili, mtakuwa mnatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu; nanyi kuweni na hakika kuwa dhambi yenu itawapata.
24 Jengeni miji kwa ajili ya wanawake na watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya mbuzi na kondoo wenu, lakini fanyeni yale mliyoahidi.”
25 Wagadi na Wareubeni wakamwambia Musa, “Sisi watumishi wako tutafanya kama bwana wetu anavyotuagiza.
26 Watoto na wake zetu, makundi ya mbuzi na kondoo, na makundi ya ng’ombe wetu, watabaki hapa katika miji ya Gileadi.
27 Lakini watumishi wenu, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, watavuka ng’ambo kupigana mbele za Mwenyezi Mungu, sawa kama bwana wetu asemavyo.”
28 Kisha Musa akatoa amri kuwahusu kwa kuhani Eleazari, na Yoshua mwana wa Nuni, na viongozi wa jamaa za makabila ya Israeli.
29 Musa akawaambia, “Ikiwa Wagadi na Wareubeni, kila mwanaume aliyevaa silaha za vita, atavuka Yordani pamoja nanyi mbele za Mwenyezi Mungu, basi mtakapoishinda nchi iliyo mbele yenu, wapeni nchi ya Gileadi kama milki yao.
30 Lakini kama hawatavuka pamoja nanyi wakiwa wamevaa silaha za vita, lazima wakubali kupokea milki yao pamoja nanyi katika nchi ya Kanaani.”
31 Wagadi na Wareubeni wakajibu, “Watumishi wako watafanya lile Mwenyezi Mungu alilosema.
32 Tutavuka mbele za Mwenyezi Mungu kuingia Kanaani tukiwa tumevaa silaha za vita, lakini mali tutakayoirithi itakuwa ng’ambo hii ya Yordani.”
33 Kisha Musa akawapa Wagadi, Wareubeni, na nusu ya kabila la Manase mwana wa Yusufu ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, nchi yote pamoja na miji yake, na nchi inayowazunguka.
34 Wagadi wakajenga Diboni, Atarothi, Aroeri,
35 Atroth-Shofani, Yazeri, Yogbeha,
36 Beth-Nimra na Beth-Harani kama miji iliyozungushiwa ngome, tena wakajenga mazizi kwa ajili ya makundi yao ya mbuzi na kondoo.
37 Nao Wareubeni wakajenga upya miji ya Heshboni, Eleale na Kiriathaimu,
38 pia Nebo na Baal-Meoni (majina ya hiyo miji yalibadilishwa) na Sibma. Miji waliyoijenga upya waliipa majina.
39 Wazao wa Makiri mwana wa Manase walienda Gileadi, wakaiteka nchi na kuwafukuza Waamori waliokuwa huko.
40 Kwa hiyo Musa akawapa Wamakiri, wazao wa Manase, nchi ya Gileadi, nao wakakaa huko.
41 Yairi, mzao wa Manase, akateka makazi yao, akayaita Hawoth-Yairi.
42 Naye Noba akateka Kenathi na makazi yaliyoizunguka, akayaita Noba kwa jina lake.