Zaburi 111
Sifa za Mwenyezi Mungu kwa matendo ya ajabu
1 Msifuni Mwenyezi Mungu.
Nitamtukuza Mwenyezi Mungu kwa moyo wangu wote,
katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.
2 Kazi za Mwenyezi Mungu ni kuu,
wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.
3 Kazi zake zimejaa fahari na utukufu,
haki yake hudumu daima.
4 Amefanya maajabu yake yakumbukwe,
Mwenyezi Mungu ni mwenye neema na huruma.
5 Huwapa chakula wale wanaomcha,
hulikumbuka agano lake milele.
6 Amewaonesha watu wake uwezo wa kazi zake,
akiwapa nchi za mataifa mengine.
7 Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki,
mausia yake yote ni ya kuaminika.
8 Zinadumu milele na milele,
zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.
9 Aliwapa watu wake ukombozi,
aliamuru agano lake milele:
jina lake ni takatifu na la kuogopwa.
10 Kumcha Mwenyezi Mungu ndicho chanzo cha hekima,
wote wanaozifuata amri zake wana busara.
Sifa zake zadumu milele.