Zaburi 12
Kuomba msaada
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa sheminithi. Zaburi ya Daudi.
1 Mwenyezi Mungu tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka;
waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.
2 Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;
midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.
3 Mwenyezi Mungu na akatilie mbali midomo yote ya hila
na kila ulimi uliojaa majivuno,
4 ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;
midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”
5 “Kwa sababu wanyonge wanaonewa,
na wahitaji wanalia kwa uchungu,
nitainuka sasa,” asema Mwenyezi Mungu.
“Nitawalinda kutokana na wale
wenye nia mbaya juu yao.”
6 Maneno ya Mwenyezi Mungu ni safi,
kama fedha iliyosafishwa katika tanuru,
iliyosafishwa mara saba.
7 Ee Mwenyezi Mungu, utatuweka salama
na kutulinda na kizazi hiki milele.
8 Watu waovu huenda wakiringa kila mahali
wakati yule aliye mbaya sana
ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.