Zaburi 99
Mwenyezi Mungu Mfalme mtakatifu
Mwenyezi Mungu anatawala,
mataifa na yatetemeke;
anakalia kiti cha enzi katikati ya makerubi,
dunia na itikisike.
Mwenyezi Mungu ni mkuu katika Sayuni;
ametukuzwa juu ya mataifa yote.
Wanalisifu jina lako ambalo ni kuu na la kuogopwa:
yeye ni mtakatifu!
 
Mfalme ni mwenye nguvu na hupenda haki,
wewe umethibitisha adili;
katika Yakobo umefanya
yaliyo haki na sawa.
Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
na mkaabudu katika mahali pa kuwekea miguu yake;
yeye ni mtakatifu.
 
Musa na Haruni walikuwa miongoni mwa makuhani wake,
Samweli alikuwa miongoni mwa walioliitia jina lake;
walimwita Mwenyezi Mungu,
naye aliwajibu.
Alizungumza nao kutoka nguzo ya wingu;
walizishika sheria zake na amri alizowapa.
 
Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
ndiwe uliyewajibu,
kwa Israeli ulikuwa Mungu mwenye kusamehe,
ingawa uliadhibu matendo yao mabaya.
Mtukuzeni Mwenyezi Mungu, Mungu wetu,
mwabuduni kwenye mlima wake mtakatifu,
kwa maana Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, ni mtakatifu.