18
Mikaya atabiri dhidi ya Ahabu
(1 Wafalme 22:1-28)
1 Basi, Yehoshafati alikuwa na mali nyingi sana na heshima. Naye akafanya urafiki na Ahabu kwa uhusiano wa ndoa.
2 Baada ya miaka kadhaa akateremka kumtembelea Ahabu huko Samaria. Ahabu akachinja ng’ombe na kondoo wengi kwa ajili yake na watu aliokuwa amefuatana nao. Kisha Ahabu akamshawishi Yehoshafati kukwea pamoja naye ili kuishambulia Ramoth-Gileadi.
3 Ahabu mfalme wa Israeli akamuuliza Yehoshafati mfalme wa Yuda, “Je, utaenda pamoja nami kupigana dhidi ya Ramoth-Gileadi?”
Yehoshafati akamjibu mfalme wa Israeli, “Mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi wangu ni kama farasi wako. Tutakuwa pamoja nawe vitani.”
4 Lakini Yehoshafati pia akamwambia mfalme wa Israeli, “Kwanza tafuta ushauri wa Mwenyezi Mungu.”
5 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akawaleta pamoja manabii, wanaume wapatao mia nne, akawauliza, “Je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi, au niache?”
Wakajibu, “Naam, nenda kwa kuwa Mungu ataiweka Ramoth-Gileadi mkononi mwa mfalme.”
6 Lakini Yehoshafati akauliza, “Je, hayuko nabii wa Mwenyezi Mungu hapa ambaye tunaweza kumuuliza?”
7 Mfalme wa Israeli akamjibu Yehoshafati, “Bado yupo mtu mmoja ambaye kupitia kwake twaweza kuuliza ushauri wa Mwenyezi Mungu, lakini namchukia kwa sababu hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila hunitabiria mabaya kila mara. Yeye ni Mikaya mwana wa Imla.”
Yehoshafati akajibu, “Mfalme hapaswi kusema hivyo.”
8 Kwa hiyo mfalme wa Israeli akamwita mmoja wa maafisa wake na kusema, “Mlete Mikaya mwana wa Imla mara moja.”
9 Wakiwa wamevalia majoho yao ya kifalme, mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wameketi juu ya viti vyao vya kifalme katika sakafu ya kupuria, kwenye ingilio la lango la Samaria, huku manabii wote wakitabiri mbele yao.
10 Wakati huu Sedekia mwana wa Kenaana alikuwa ametengeneza pembe za chuma. Naye akatangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, ‘Kwa hizi pembe utawapiga Waaramu hadi waangamizwe.’ ”
11 Manabii wengine wote walikuwa wanatabiri kitu hicho hicho, wakisema, “Ishambulie Ramoth-Gileadi na uwe mshindi. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ataitia mkononi mwa mfalme.”
12 Mjumbe aliyekuwa ameenda kumwita Mikaya akamwambia, “Tazama, manabii wote kama mtu mmoja wanatabiri ushindi kwa mfalme. Neno lako na likubaliane na lao, nawe unene mema kuhusu mfalme.”
13 Lakini Mikaya akasema, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo, nitamwambia kile tu Mwenyezi Mungu atakachoniambia.”
14 Alipofika, mfalme akamuuliza, “Mikaya, je, twende vitani dhidi ya Ramoth-Gileadi au niache?”
Akamjibu, “Shambulia na ushinde, kwa kuwa watatiwa mkononi mwako.”
15 Mfalme akamwambia, “Je, ni mara ngapi nitakuapisha ili usiniambie kitu chochote ila kweli tu kwa jina la Mwenyezi Mungu?”
16 Ndipo Mikaya akajibu, “Niliona Israeli wote wametawanyika vilimani kama kondoo wasio na mchungaji, naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Watu hawa hawana kiongozi. Mwache kila mmoja aende nyumbani kwa amani.’ ”
17 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Sikukuambia kwamba huwa hatabiri jambo lolote jema kunihusu, ila mabaya tu?”
18 Mikaya akaendelea, “Kwa hiyo lisikie neno la Mwenyezi Mungu: Nilimwona Mwenyezi Mungu ameketi kwenye kiti chake cha enzi pamoja na jeshi lote la mbinguni likiwa limesimama upande wa kulia na wa kushoto.
19 Naye Mwenyezi Mungu akasema, ‘Ni nani atakayemshawishi Ahabu, mfalme wa Israeli, ili aishambulie Ramoth-Gileadi na kukiendea kifo chake huko?’
“Mmoja akapendekeza hili na mwingine lile.
20 Hatimaye, roho akajitokeza, akasimama mbele za Mwenyezi Mungu na kusema, ‘Nitamshawishi.’
“Mwenyezi Mungu akauliza, ‘Kwa njia gani?’
21 “Akasema, ‘Nitaenda na kuwa roho ya uongo katika vinywa vya manabii wake wote.’
“Mwenyezi Mungu akasema, ‘Utafanikiwa katika kumshawishi. Nenda ukafanye hivyo.’
22 “Kwa hiyo sasa Mwenyezi Mungu ameweka roho ya kudanganya ndani ya vinywa vya hawa manabii wako wote. Mwenyezi Mungu ameamuru maafa kwa ajili yako.”
23 Kisha Sedekia mwana wa Kenaana akatoka na kumpiga Mikaya kofi usoni. Akauliza, “Huyo Roho kutoka kwa Mwenyezi Mungu alipita njia gani alipotoka kwangu ili kusema nawe?”
24 Mikaya akajibu, “Utagundua siku hiyo utakapoenda kujificha kwenye chumba cha ndani.”
25 Kisha mfalme wa Israeli akaagiza, “Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mtawala wa mji, na kwa Yoashi mwana wa mfalme.
26 Mkaseme, ‘Hivi ndivyo asemavyo mfalme: Mwekeni mtu huyu gerezani na asipewe chochote ila mkate na maji hadi nitakaporudi salama.’ ”
27 Mikaya akasema, “Kama utarudi salama, basi Mwenyezi Mungu hajanena kupitia kwangu.” Kisha akaongeza kusema, “Zingatieni maneno yangu, enyi watu wote!”
Ahabu anauawa huko Ramoth-Gileadi
(1 Wafalme 22:29-35)
28 Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakaenda Ramoth-Gileadi.
29 Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, “Nitaingia vitani nikiwa nimejibadilisha, lakini wewe uvae majoho yako ya kifalme.” Kwa hiyo mfalme wa Israeli akajibadilisha na kwenda vitani.
30 Wakati huu, mfalme wa Aramu alikuwa amewaagiza majemadari thelathini na wawili wa magari ya vita, “Msipigane na yeyote, mdogo au mkubwa, isipokuwa mfalme wa Israeli.”
31 Wale majemadari wa magari ya vita walipomwona Yehoshafati, wakafikiri, “Hakika huyu ndiye mfalme wa Israeli.” Kwa hiyo wakageuka ili wamshambulie, lakini Yehoshafati akapiga kelele, naye Mwenyezi Mungu akamsaidia. Mungu akawaondoa kwake,
32 wale majemadari wakaona kwamba hakuwa mfalme wa Israeli nao wakaacha kumfuatilia.
33 Lakini mtu fulani akavuta upinde pasipo lengo na kumpiga mfalme wa Israeli katikati ya kiungio cha mavazi yake ya chuma. Mfalme akamwambia mwendesha gari lake la vita, “Geuza gari na uniondoe katika mapigano, nimejeruhiwa.”
34 Vita vikaendelea mchana kutwa, naye mfalme wa Israeli akajitegemeza ndani ya gari lake kuwaelekea Waaramu hadi jioni. Basi jioni yake akafa.