26
Uzia mfalme wa Yuda
(2 Wafalme 14:21-22; 15:1-7)
1 Kisha watu wote wa Yuda wakamchukua Uzia, aliyekuwa na umri wa miaka kumi na sita, nao wakamfanya mfalme mahali pa Amazia baba yake.
2 Ndiye aliijenga upya Elathi na kuirudisha kwa Yuda baada ya Amazia kulala na baba zake.
3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka hamsini na mbili. Mama yake aliitwa Yekolia, kutoka Yerusalemu.
4 Akatenda yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu, vile Amazia baba yake alivyofanya.
5 Akamtafuta Mungu katika siku za Zekaria, aliyemwelekeza kumcha Mungu. Wakati wote alipomtafuta Mwenyezi Mungu, Mungu alimfanikisha.
6 Alipigana vita dhidi ya Wafilisti na kubomoa kuta za Gathi, Yabne na Ashdodi. Kisha akajenga upya miji karibu na Ashdodi, na mahali pengine katikati ya Wafilisti.
7 Mungu akamsaidia dhidi ya Wafilisti na dhidi ya Waarabu walioishi Gur-Baali na dhidi ya Wameuni.
8 Waamoni wakamletea Uzia ushuru, na umaarufu wake ukaenea hadi mpaka wa Misri, kwa sababu alikuwa na nguvu sana.
9 Uzia akajenga minara huko Yerusalemu katika Lango la Pembeni, katika Lango la Bondeni na katika pembe, mahali kuta zikutanapo, kisha akaijengea ngome.
10 Akajenga pia minara jangwani na kuchimba visima vingi vya maji, kwa sababu alikuwa na mifugo mingi chini ya vilima na katika nchi tambarare. Alikuwa na watu waliofanya kazi katika mashamba yake, na kwenye mashamba yake ya mizabibu huko vilimani na katika ardhi zenye rutuba, kwa kuwa aliupenda udongo.
11 Zaidi ya hayo, Uzia alikuwa na jeshi lililofunzwa vizuri, lililokuwa tayari kwenda vitani kwa vikosi kufuatana na idadi yao kama walivyokusanywa na Yeieli mwandishi na Maaseya msimamizi chini ya maelekezo ya Hanania, mmoja wa maafisa wa mfalme.
12 Idadi yote ya viongozi wa jamaa waliowaongoza wapiganaji walikuwa elfu mbili na mia sita.
13 Chini ya uongozi wao kulikuwa na jeshi la watu elfu mia tatu na saba na mia tano waliofundishwa kwa ajili ya vita, jeshi lenye nguvu la kumsaidia mfalme dhidi ya adui zake.
14 Uzia akalipatia jeshi lote ngao, mikuki, chapeo, dirii, pinde na mawe ya kombeo.
15 Huko Yerusalemu watu wenye utaalamu mkubwa wakatengeneza mitambo iliyotumika katika minara na kwenye pembe za ulinzi ili kurusha mishale na kuvurumisha mawe makubwa. Sifa zake zikaenea mbali sana kwa sababu alisaidiwa mno hadi akawa na nguvu sana.
16 Lakini baada ya Uzia kuwa na nguvu sana, majivuno yake yakamsababishia kuanguka. Alikosa uaminifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wake, naye akaingia hekaluni mwa Mwenyezi Mungu ili afukize uvumba kwenye madhabahu ya kufukizia uvumba.
17 Azaria kuhani akiwa pamoja na makuhani wengine themanini wa Mwenyezi Mungu wenye ujasiri wakamfuata ndani.
18 Wakamkabili na kumwambia, “Siyo sawa kwako, Uzia, kumfukizia Mwenyezi Mungu uvumba. Hiyo ni kazi ya makuhani, wazao wa Haruni, ambao wamewekwa wakfu ili kufukiza uvumba. Ondoka mahali patakatifu, kwa kuwa umekosa uaminifu nawe hutaheshimiwa na Bwana Mwenyezi Mungu.”
19 Uzia, aliyekuwa na chetezo mkononi mwake tayari kufukiza uvumba, akakasirika. Alipokuwa anawaghadhibikia makuhani mbele ya madhabahu ya kufukizia uvumba katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ukoma ukamtokea kwenye paji la uso wake.
20 Azaria kuhani mkuu pamoja na makuhani wengine wote walipomtazama wakaona kwamba alikuwa na ukoma pajini lake, wakaharakisha kumtoa nje. Naam, hata yeye mwenyewe alitamani kuondoka kwa sababu Mwenyezi Mungu alikuwa amempiga.
21 Mfalme Uzia alikuwa na ukoma hadi siku ya kufa kwake. Akatengwa katika nyumba ya pekee akiwa mwenye ukoma, naye akawa ametengwa kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu. Yothamu mwanawe akawa msimamizi wa jumba la mfalme, pia akawaongoza watu wa nchi.
22 Matukio mengine ya utawala wa Uzia, kuanzia mwanzo hadi mwisho, yameandikwa na nabii Isaya mwana wa Amozi.
23 Uzia akalala na baba zake, akazikwa karibu nao katika shamba la kuzikia lililokuwa mali ya wafalme, kwa kuwa watu walisema, “Alikuwa na ukoma.” Yothamu mwanawe akawa mfalme baada yake.