4
Maagizo ya mwisho
Nakuagiza mbele za Mungu na mbele za Al-Masihi Isa, atakayewahukumu watu walio hai na waliokufa wakati wa kuja kwake na ufalme wake, kwamba: Hubiri Neno; kuwa tayari wakati ufaao na wakati usiofaa; karipia, kemea na utie moyo kwa uvumilivu wote na kwa mafundisho mazuri. Maana wakati utakuja watu watakapokataa kuyakubali mafundisho yenye uzima. Badala yake, ili kutimiza tamaa zao wenyewe, watajikusanyia idadi kubwa ya walimu watakaowaambia yale masikio yao yanatamani kusikia. Watakataa kusikiliza kweli na kuzigeukia hadithi za uongo. Bali wewe, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza wajibu wote wa huduma yako.
Kwa maana mimi sasa ni tayari kumiminwa kama sadaka ya kinywaji, nayo saa yangu ya kuondoka imetimia. Nimevipiga vita vizuri, mashindano nimeyamaliza, imani nimeilinda. Sasa nimewekewa taji la haki ambalo Bwana, Mwamuzi wa haki, atanitunukia siku ile: wala si mimi tu, bali pia wote ambao wamengoja kwa shauku kudhihirishwa kwake.
Maelekezo ya binafsi
Jitahidi kuja kwangu upesi 10 kwa sababu Dema, kwa kuupenda ulimwengu, ameniacha na ameenda Thesalonike. Kreske ameenda Galatia, na Tito ameenda Dalmatia. 11 Ni Luka pekee aliye hapa nami. Mtafute Marko uje naye, kwa sababu ananifaa sana katika huduma yangu. 12 Nimemtuma Tikiko huko Efeso. 13 Utakapokuja, niletee lile joho nililoliacha kwa Karpo huko Troa, na vile vitabu vyangu, hasa vile vya ngozi.
14 Iskanda yule mfua chuma alinitendea ubaya mkubwa. Bwana Isa atamlipa kwa ajili ya yale aliyotenda. 15 Wewe pia ujihadhari naye kwa sababu aliyapinga maneno yetu vikali.
16 Katika utetezi wangu wa mara ya kwanza, hakuna hata mmoja aliyeniunga mkono, bali kila mmoja aliniacha. Naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. 17 Lakini Bwana Isa alisimama upande wangu akanitia nguvu, ili kupitia kwangu lile Neno lihubiriwe kwa ukamilifu, watu wote Mataifa wapate kulisikia. Mimi niliokolewa kutoka kinywa cha simba. 18 Bwana Isa ataniokoa katika kila shambulio baya na kunileta salama katika ufalme wake wa mbinguni. Atukuzwe milele na milele. Amen.
 
Salamu za mwisho
19 Wasalimu Prisila* na Akila, na wote wa nyumbani mwa Onesiforo.
 
20 Erasto alibaki Korintho, nami nikamwacha Trofimo huko Mileto akiwa mgonjwa. 21 Jitahidi ufike huku kabla ya majira ya baridi.
 
Eubulo anakusalimu, vivyo hivyo Pude, Lino, Klaudia na ndugu wote.
 
22 Bwana Isa awe pamoja na roho yako. Neema iwe pamoja nanyi.
* 4:19 kwa Kiyunani ni Priska