5
1 Hivyo, mtu mmoja aliyeitwa Anania, na Safira mkewe, waliuza sehemu ya mali,
2 na akaficha sehemu ya fedha waliyouza (mke wake pia alilijua hili), na akaleta sehemu iliyobakia na kuiweka kwenye miguu ya mitume.
3 Lakini Petro akasema, “Anania, kwa nini shetani ameujaza moyo wako kusema uongo kwa Roho Mtakatifu na kuficha sehemu ya mali ya shamba?
4 Wakati lilipokuwa halijauzwa, halikuwa ni mali yako? Na baada ya kuuzwa, halikuwa chini ya uamuzi wako? Ilikuwaje uwaze jambo hili moyoni mwako? Hujawadanganya wanadamu, bali umemdanganya Mungu.”
5 Katika kusikia maneno haya, Anania alidondoka chini na akakata roho. Na hofu kubwa iliwajia wote waliolisikia hili.
6 Vijana wakaja mbele na kumtia katika sanda, na kumpeleka nje na kumzika.
7 Baada ya masaa matatu hivi, mke wake aliingia ndani, asijue ni nini kilichokuwa kimetokea.
8 Petro akamwambia, “Niambie, kama mliuza shamba kwa thamani hiyo.” Akasema, “Ndiyo, kwa thamani hiyo.”
9 Kisha Petro akamwambia, “Inakuwaje kwamba mmepatana kwa pamoja kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu ya wale waliomzika mme wako iko mlangoni, na watakubeba na kukupeleka nje.”
10 Ghafla akadondoka miguuni pa Petro, akakata roho, na wale vijana wakaja ndani wakamkuta ameshakufa. Wakambeba kumpeleka nje, na kumzika karibu na mmewe.
11 Hofu kubwa ikaja juu ya kanisa zima, na juu ya wote walioyasikia mambo haya.
12 Ishara nyingi na maajabu vilikuwa vinatokea miongoni mwa watu kupitia mikono ya mitume. Walikuwa pamoja katika ukumbi wa Sulemani.
13 Lakini, hakuna mtu mwingine tofauti aliyekuwa na ujasiri wa kuambatana nao; hata hivyo, walipewa heshima ya juu na watu.
14 Na pia, waamini wengi walikuwa wakiongezeka kwa Bwana, idadi kubwa ya wanaume na wanawake,
15 kiasi kwamba hata waliwabeba wagonjwa mitaani, na kuwalaza vitandani na kwenye makochi, ili kwamba Petro akiwa anapita, kivuli chake kiweze kushuka juu yao.
16 Hapo pia, idadi kubwa ya watu walikuja kutoka miji iliyozunguka Yerusalem, wakiwaleta wagonjwa na wote waliopagawa na roho wachafu, na wote waliponywa.
17 Lakini kuhani mkuu aliinuka, na wote waliokuwa pamoja naye (ambao ni wa dhehebu la masadukayo); na walijawa na wivu
18 wakanyosha mikono yao kuwakamata mitume na kuwaweka ndani ya gereza la jumla.
19 Na wakati wa usiku malaika wa Bwana akaifungua milango ya gereza na kuwaongoza nje na kusema,
20 “Nendeni, mkasimame hekaluni na kuwaambia watu maneno yote ya Uzima huu.”
21 Waliposikia hili, waliingia hekaluni wakati wa kupambazuka na kufundisha. Lakini, kuhani mkuu alikuja na wote waliokuwa naye, na kuitisha baraza lote kwa pamoja, na wazee wote wa watu wa Israeli, na kuwatuma gerezani ili kuwaleta mitume.
22 Lakini watumishi waliokwenda, hawakuwakuta gerezani, walirudi na kutoa taarifa,
23 “Tumekuta gereza limefungwa vizuri salama, na walinzi wamesimama langoni, lakini tulipokuwa tukifungua, hatukuona mtu ndani.”
24 Sasa wakati jemedari wa hekalu na makuhani wakuu waliposikia maneno haya, waliingiwa na shaka kubwa kwa ajili yao wakiwaza litakuwaje jambo hili.
25 Kisha mmoja akaja na kuwaambia, “Watu mliowaweka gerezani wamesimama hekaluni na wanafundisha watu.”
26 Hivyo jemedari alienda pamoja na watumishi, na wakawaleta, lakini bila ya kufanya vurugu, kwa sababu waliwaogopa watu wangeweza kuwapiga kwa mawe.
27 Walipokwisha kuwaleta, waliwaweka mbele ya baraza. Kuhani mkuu aliwahoji
28 akisema, “Tuliwaamuru msifundishe kwa jina hili, na bado mmeijaza Yerusalemu kwa fundisho lenu, na kutamani kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”
29 Lakini Petro na mitume wakajibu, “Lazima tumtii Mungu kuliko watu.
30 Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, mliyemuua, kwa kumtundika juu ya mti.
31 Mungu alimtukuza katika mkono wake wa kuume, na kumfanya kuwa Mkuu na mwokozi, kutoa toba kwa Israeli, na msamaha wa dhambi.
32 Sisi ni mashahidi wa mambo haya, na Roho Mtakatifu, ambaye Mungu amemtoa kwa wale wanaomtii.”
33 Wajumbe wa baraza waliposikia hivi, walishikwa na hasira wakataka kuwaua mitume.
34 Lakini pharisayo aliyeitwa Gamalieli, mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, alisimama na kuwaamuru mitume wachukuliwe nje kwa muda mfupi.
35 Kisha akawaambia, “Wanaume wa Israeli, iweni makini sana na kile mnachopendekeza kuwafanyia watu hawa.
36 Kwa sababu, zamani zilizopita, Theuda aliinuka na kujidai kuwa mtu mkuu, na idadi ya watu, wapata mia nne walimfuata. Aliuawa, na wote waliokuwa wanamtii walitawanyika na kupotea.
37 Baada ya mtu huyu, Yuda mgalilaya, aliinuka siku zile za kuandikwa sensa, akavuta watu wengi nyuma yake. Naye pia alipotea na wote waliokuwa wakimtii walitawanyika.
38 Sasa nawaambia, jiepusheni na watu hawa na muwaache wenyewe, kwa sababu, kama mpango huu au kazi hii ni ya watu itatupwa.
39 Lakini kama ni ya Mungu, hamtaweza kuwazuia; mnaweza mkajikuta hata mnashindana na Mungu.” Hivyo, walishawishika na maneno yake.
40 Kisha, waliwaita mitume ndani na kuwachapa na kuwaamuru wasinene kwa jina la Yesu, na wakawaacha waende zao.
41 Waliondoka mbele ya baraza wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuteseka na kutoheshimiwa kwa ajili ya Jina hilo.
42 Kwa hiyo, kila siku, ndani ya hekalu na kutoka nyumba hadi nyumba waliendelea kufundisha na kuhubiri Yesu kuwa ni Masihi.