6
1 Mmoja wenu anapokuwa na tatizo na mwenzake, anathubutu kwenda kwa mahakama ya wasio haki kuliko mbele ya waumini?
2 Hamjui kuwa waumini watauhukumu ulimwengu? Na kama mtauhukumu ulimwengu, hamuwezi kuamua mambo yasiyo muhimu?
3 Hamjui kuwa tutawahukumu malaika? Kwa kiasi gani zaidi, tunaweza kuamua mambo ya maisha haya?
4 Kama tunaweza kuhukumu mambo ya maisha haya, kwa nini mnathubutu kupeleka mashitaka mbele ya wasiosimama kanisani?
5 Nasema haya kwa aibu yenu. Hakuna mwenye busara miongoni mwenu wa kutosha kuweka mambo sawa kati ya ndugu na ndugu?
6 Lakini kama ilivyo sasa, mwamini mmoja huenda mahakamani dhidi ya muumini mwingine, na mashitaka hayo huwekwa mbele ya hakimu asiyeamini!
7 Ukweli ni kwamba kuna matatizo katikati ya Wakristo yaliyoleta tayari usumbufu kwenu. Kwanini msiteseke kwa mabaya? Kwanini mnakubali kudanganywa?
8 Lakini mmetenda uovu na kudanganya wengine, na hao ni kaka na dada zenu!
9 Hamjui kwamba wasio haki hawataurithi ufalme wa Mungu? Msiamini uongo. Waasherati, waabudu sanamu, wazinzi, wafiraji, walawiti,
10 wevi, wachoyo, walevi, wanyang'anyi, watukanaji-hakuna miongoni mwao atakayeurithi ufalme wa Mungu.
11 Na hao walikuwa baadhi yao ni ninyi. Lakini mmekwisha kutakaswa, lakini mmekwisha kuoshwa, lakini mmekwisha kutengwa kwa Mungu, lakini mmefanywa haki mbele za Mungu katika jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.
12 “Vitu vyote ni halali kwangu”, lakini si kila kitu kina faida. “Vitu vyote ni halali kwangu,” lakini sitatawaliwa na kimoja cha hivyo.
13 “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula,” lakini Mungu atavitowesha vyote. Mwili haujaumbwa kwa ajili ya ukahaba, badala yake, mwili ni kwa ajili ya Bwana, na Bwana atauhudumia mwili.
14 Mungu alimfufua Bwana na sisi pia atatufufua kwa nguvu zake.
15 Hamjui kwamba miili yenu ina muunganiko na Kristo? Mwawezaje kuvitoa viungo vya Kristo na kwenda kuviunganisha na kahaba? Haiwezekani!
16 Hamjui kwamba anayeungana na kahaba amekuwa mwili mmoja naye? Kama andiko lisemavyo, “Wawili watakuwa mwili mmoja.”
17 Lakini anayeungana na Bwana anakuwa roho moja pamoja naye.
18 Ikimbieni zinaa! “Kila dhambi aifanyayo mtu ni nje na mwili wake. Lakini zinaa, mtu hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
19 Hamjui kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu, akaaye ndani yenu, yule ambaye mlipewa kutoka kwa Mungu? Hamjui kwamba si ninyi wenyewe?
20 Kwamba mlinunuliwa kwa thamani. Kwa hiyo mtukuzeni Mungu kwa miili yenu.