9
1 Mimi si huru? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Yesu Bwana wetu? Ninyi si matunda ya kazi yangu katika Bwana?
2 Ikiwa mimi si mtume kwa wengine, angalau ni mtume kwenu ninyi. Kwa maana ninyi ni uthibitisho wa utume wangu katika Bwana.
3 Huu ndio utetezi wangu kwa wale wanaonichunguza mimi.
4 Je hatuna haki ya kula na kunywa?
5 Hatuna haki kuchukua mke aliye amini kama wafanyavyo mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa?
6 Au ni mimi peke yangu na Barnaba ambao tunapaswa kufanya kazi?
7 Ni nani afanyaye kazi kama askari kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mzabibu na asile matunda yake? Au ni nani achungaye kundi asiyekunywa maziwa yake?
8 Je ninasema haya kwa mamlaka ya kibinadamu? Sheria nayo haisemi haya?
9 Kwa kuwa imeandikwa katika sheria ya Musa, “usimfunge ng'ombe kinywa apulapo nafaka.” Ni kweli kwamba hapa Mungu anajali ng'ombe?
10 Au je hasemi hayo kwa ajili yetu? imeandikwa kwa ajili yetu, kwa sababu yeye alimaye nafaka inampasa kulima kwa matumaini, naye avunaye inampasa avune kwa matarajio ya kushiriki katika mavuno.
11 Ikiwa tulipanda vitu vya rohoni miongoni mwenu, Je! Ni neno kubwa kwetu tukivuna vitu vya mwilini kutoka kwenu?
12 Ikiwa wengine walipata haki hii kutoka kwenu, Je! Sisi si zaidi? Hata hivyo, hatukuidai haki hii. Badala yake, tulivumilia mambo yote badala ya kuwa kikwazo cha injili ya Kristo.
13 Hamjui ya kuwa wote wafanyao kazi hekaluni hupata chakula chao kutoka hekaluni? Hamjui ya kuwa wote watendao kazi madhabahuni hupata sehemu ya kile kilichotolewa madhabahuni?
14 Kwa jinsi iyo hiyo, Bwana aliagiza ya kuwa wote wanaoitangaza injili sharti wapate kuishi kutokana na hiyo injili.
15 Lakini sijawadai haki zote hizi. Na siandiki haya ili jambo lolote lifanyike kwa ajili yangu. Ni heri mimi nife kuliko mtu yeyote kubatilisha huku kujisifu kwangu.
16 Maana ikiwa naihubiri injili, sina sababu ya kujisifu, kwa sababu ni lazima nifanye hivi. Na ole wangu nisipoihubiri injili!
17 Kwa maana nikifanya hivi kwa hiari yangu, nina thawabu. Lakini ikiwa si kwa hiari, bado nina jukumu nililopewa kuwa wakili.
18 Basi thawabu yangu ni nini? Ya kuwa nihubiripo, nitaitoa injili pasipo gharama na bila kutumia kwa utimilifu wa haki yangu niliyonayo katika Injili.
19 Maana japo nimekuwa huru kwa wote, nilifanyika mtumwa wa wote, ili kwamba niweze kuwapata wengi zaidi.
20 Kwa Wayahudi nilikuwa kama Myahudi, ili niwapate Wayahudi. Kwa wale walio chini ya sheria, nilikuwa kama mmoja wao aliye chini ya sheria ili niwapate wale walio chini ya sheria. Nilifanya hivyo ingawa mimi binafsi sikuwa chini ya sheria.
21 Kwa wale walio nje ya sheria, nilikuwa kama mmoja wao nje ya sheria, ingawa mimi binafsi sikuwa nje ya sheria ya Mungu, bali chini ya sheria ya Kristo. Nilifanya hivyo ili niwapate wale walio nje ya sheria.
22 Kwa walio wanyonge nilikuwa mnyonge, ili niwapate walio wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa baadhi.
23 Nami nafanya mambo yote kwa ajili ya injili, ili nipate kushiriki katika baraka.
24 Hamjui ya kuwa katika mbio wote washindanao hupiga mbio, lakini apokeaye tuzo ni mmoja? Hivyo pigeni mbio ili mpate tuzo.
25 Mwana michezo hujizuia katika yote awapo katika mafunzo. Hao hufanya hivyo ili wapokee taji iharibikayo, lakini sisi tunakimbia ili tupate taji isiyoharibika.
26 Kwa hiyo mimi sikimbii bila sababu au napigana ngumi kama kupiga hewa.
27 Lakini nautesa mwili wangu na kuufanya kama mtumwa, ili kwamba nijapokwisha kuwahubiri wengine, mimi mwenyewe nisiwe wa kukataliwa.