Kutoka
1
1 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli waliokuja Misri pamoja na Yakobo kila moja na familia yake:
2 Rubeni, Simioni, Lawi, na Yuda,
3 Isakari, Zebuluni, na Benjamini,
4 Dani, Naftali, Gadi, na Asheri.
5 Jumla ya watu wa ukoo wa Yakobo walikuwa sabini. Yusufu alikuwa Misri tayari.
6 Ndipo Yusufu, pamoja na kaka zake wote, na kizazi chote wakafa.
7 Waisraeli walifanikiwa sana, wakaongezeka sana idadi yao, na wakawa na nguvu maana nchi ilijazwa na wao.
8 Wakati huu sasa mfalme mpya asiyemjua Yusufu aliinuka katika Misri.
9 Akawaambia watu wake, “Tazama, hawa Waisraeli ni wengi na wenye nguvu kuliko sisi.
10 Njooni na tukae nao kwa akili, ama sivyo wataendelea kuongezeka na kama vita ikiibuka, wataungana na adui zetu, watapigana nasi, na kisha wataondoka.”
11 Hivyo wakawekea walinzi ambao waliwatesa kwa kuwatumikisha kazi ngumu. Waisraeli walijenga maghala ya miji kwa ajili ya Farao: Pishoni na Ramsei.
12 Lakini kadiri Wamisri walivyowatesa, ndivyo Waisraeli waliendelea kuongezeka na kusambaa. Hivyo Wamisri wakaanza kuwaogopa Waisraeli.
13 Wamisri waliwafanya Waisraeli wafanye kazi kwa nguvu nyingi.
14 Waliyafanya maisha yao kuwa machungu kwa kuwafanyisha kazi ngumu kwa vinu na matofali na kwa kila aina ya kazi za shambani. Kazi zao zote zilikuwa ngumu.
15 Kisha mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Kiebrania; mmoja wao aliitwa jina lake Shifra, na mwingine aliitwa Puha.
16 Akasema, “Wakati mnapowasaidia wanawake wa Kiebrania wanapojifungua, chunguzeni wanapozaa. Ikiwa ni mtoto wa kiume, basi muueni; bali ikiwa ni mtoto wa kike, basi mwacheni aishi.”
17 Lakini wale Wakunga walimwogopa Mungu na hawakufanya kama mfalme wa Misri alivyowaagiza; badala yake waliwaacha watoto wa kiume waishi.
18 Mfalme wa Misri akawaita Wakunga na kuwaambia, “Kwanini mmefanya haya, na kuwaacha watoto wa kiume wakaishi?”
19 Wale Wakunga wakamjibu Farao, “Hawa wanawake wa Kiebrania siyo kama wanawake wa Kimisri. Hawa wana nguvu na jasiri sana maana wao humaliza kuzaa kabla hata mkunga hajafika.”
20 Mungu aliwalinda hawa Wakunga. Watu waliongezeka kwa idadi na kuwa na nguvu sana.
21 Kwa sababu wale Wakunga walimwogopa Mungu, aliwapa familia.
22 Farao akawaagiza watu wote, “Lazima mmutupe kila mtoto wa kiume anayezaliwa katika mto, lakini kila mtoto wa kike wamwache aishi.”