31
1 Yahweh akasema na Musa,
2 “Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda
3 Nami nimemjaza Bezaleli na roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina,
4 ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba,
5 na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.
6 Tena, nimemchagua, awe pamoja naye Oholiabu, mwana wa Ahisamaki, wa kabila ya Dani. Nami nimetia hekima katika mioyo ya wote wenye moyo wa hekima, ili wapate kufanya vyote nilivyokuagiza. Hii ni,
7 hema ya kukutania na sanduku la ushuhuda, na kiti cha rehema kilicho juu yake, na vyombo vyote vya Hema;
8 na meza, na vyombo vyake, na kinara cha taa safi pamoja na vyombo vyake vyote,
9 na madhabahu ya kufukizia uvumba; na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake.
10 Pia mavazi yenye kufumwa kwa uzuri, na mavazi matakatifu ya Haruni kuhani, na mavazi ya wanawe, ili kutumika katika kazi ya ukuhani.
11 Pia mafuta ya kutiwa, na uvumba wa manukato mazuri, kwa ajili ya mahali patakatifu; sawasawa na yote niliyokuagiza ndivyo watakavyofanya wao.
12 akasema na Musa,
13 “Waambie wana wa Israeli, 'Hakika mtazishika Sabato zangu, kwa kuwa ni ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi BWANA niwatakasaye ninyi.
14 Basi mtaishika hiyo Sabato; kwa kuwa ni takatifu kwenu; kila mtu atakayeitia unajisi hakika yake atauawa; kwa kuwa kila mtu afanyaye kazi katika siku hiyo, nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
15 Kazi itafanywa siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, takatifu kwa BWANA; kila mtu atakayefanya kazi yo yote katika siku ya Sabato, hakika yake atauawa.
16 Kwa ajili ya hayo wana wa Israeli wataishika Sabato. Kuiangalia sana hiyo Sabato katika vizazi vyao vyote, ni agano la milele.
17 Ni ishara kati ya mimi na wana wa Israeli milele; kwani kwa siku sita Yahweh alifanya mbingu na nchi, akastarehe kwa siku ya saba na kupumzika.
18 Hapo Mungu alipokuwa amekwisha zungumza na Musa katika mlima wa Sinai, akampa hizo mbao mbili za ushuhuda, mbao mbili za mawe, zilizoandikwa kwa mkono wake.