6
1 Ndugu, ikiwa mtu amekamatwa katika uovu, ninyi mlio wa kiroho, mnawiwa kumrejesha huyo ndugu katika roho ya upole. Huku mkijiangalia wenyewe ili msijaribiwe.
2 Mchukuliane mizigo, na kwa hiyo mtaikamilisha sheria ya Kristo.
3 Ikiwa mtu yeyote anajiona ni bora wakati si kitu, anajidanganya mwenyewe.
4 Kila mmoja na aipime kazi yake. Kisha atakuwa na kitu mwenyewe peke yake cha kujisifu, bila kujilinganisha mwenyewe na mtu yeyote.
5 Maana kila mtu atachukua mzigo wake mwenyewe.
6 Mtu aliyefundishwa neno lazima amshirikishe mazuri yote mwalimu wake.
7 Msidanganyike. Mungu hadhihakiwi. Kila apandacho mtu, ndicho atakachovuna pia.
8 Kila apandaye mbegu katika asili yake ya dhambi atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye mbegu katika Roho, atavuna uzima wa milele kutoka kwa Roho.
9 Tusichoke katika kutenda mema, maana kwa wakati wake tutavuna ikiwa hatutakata tamaa.
10 Hivyo basi, wakati tutakapokuwa na nafasi, tutende mema kwa kila mmoja. Tutende mema zaidi hasa kwa walio ndani ya imani.
11 Angalieni ukubwa wa barua nilizowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe.
12 Wale wanaotaka kufanya mema kwa mtazamo wa mwili ndiyo wenye kuwalazimisha mtahiriwe. Wanafanya hivyo kwa sababu wasiingie kwenye mateso ya msalaba wa Kristo.
13 Maana hata hao waliotahiriwa wenyewe hawaishiki sheria. Badala yake wanataka ninyi mtahiriwe ili waweze kujivunia miili yenu.
14 Isitokee nikajivuna isipokuwa kwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni katika yeye ulimwengu umesulubiwa kwangu na mimi katika ulimwengu.
15 Kwa kuwa haijalishi kutahiriwa au kutokutahiriwa kuwa ni kitu. Badala yake uzao mpya ni muhimu.
16 Kwa wote wenye kuishi kwa kanuni hii, wawe na amani na rehema iwe juu yao wote, na juu ya Israel ya Mungu.
17 Tangu sasa mtu yeyote asinitaabishe, maana nimebeba chapa za Yesu mwilini mwangu.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe na roho zenu, ndugu. Amina.