18
1 Yahwe alimtokea Abraham katika Mialoni ya Mamre, alipokua ameketi mlangoni pa hema wakati wa jua.
2 Akatazama juu na, tazama, akaona wanaume watatu wamesimama mbele yake. Alipo waona, alikimbia kupitia mlango wa hema kuwalaki na kuinama chini hadi ardhini.
3 Akasema, “Bwana, kama nimepata upendelea machoni pako, nakuomba usinipite na kuniacha mtumishi wako.
4 Naomba maji kidogo yaletwe, mnawe miguu yenu, na mjipumzishe chini ya mti.
5 Nami acha nilete chakula kidogo, ili kwamba mjiburudishe wenyewe. Ndipo baadae mwaweza kwenda zenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.” Nao wakasema, “Fanya kama ulivyo sema.”
6 Kisha Abraham akaenda upesi hemani kwa Sara, na akasema, “Harakisha, chukua vipimo vitatu vya unga safi, uukande, na fanya mkate.”
7 Kisha Abraham akakimbia kundini, akachukua ndama wa ng'ombe aliye laini na mzuri, na akampatia mtumishi na kwa haraka akamwandaa.
8 Akatwaa siagi na maziwa na ndama aliye kwisha andaliwa, na akaweka chakula mbele yao, naye akasimama karibu nao chini ya mti wakati wanakula.
9 Wakamwambia, “Mke wako Sara yuko wapi?” akajibu. “pale hemani.”
10 akasema, “Hakika nitarejea kwako majira ya machipuko, na tazama Sara mkeo atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa akisikiliza mlangoni pa hema iliyokuwa nyuma yake.
11 Abraham na Sara walikuwa wazee, umri wao ulikuwa umeendelea sana, na Sara alikuwa amepita umri ambao mwanamke anaweza kuzaa watoto.
12 Kwa hiyo Sara akajicheka mwenyewe, akijisemesha mwenyewe, “baada ya kuwa nimechakaa na bwana wangu ni mzee, je ni tapata furaha hii?”
13 Yahwe akamwambia Abraham, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, Je ni kweli nitazaa mtoto, nikiwa mzee'?
14 Je kuna jambo lolote gumu sana kwa Yahwe? Itakuwa katika wakati nilioweka mimi majira ya machipuko, nitarejea kwako. Majira haya mwakani Sara atakuwa na mtoto wa kiume.”
15 Kisha Sara akakataa na kusema, “sikucheka,” kwa kuwa aliogopa. Yahwe akasema, “hapana ulicheka.”
16 Kisha wale wanaume walisimama kuondoka na wakatazama chini kuelekea Sodoma. Abraham akafuatana nao kuona njia yao.
17 Lakini Yahwe akasema, Je ni mfiche Abraham kile ninacho kusudia kufanya,
18 Ikiwa kwa hakika Abraham atakuwa mkuu na taifa lenye nguvu, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa?
19 Kwa kuwa nimemchagua ili awaelekeze wanawe na nyumba yake baada yake waishike njia ya Yahwe, watende utakatifu na haki, ili kwamba Yahwe ampatie Abraham yale aliyo yasema kwake.”
20 Kisha Yahwe akasema, “Kwa sababu kilio cha Sodoma na Gomora ni kikuu, na kwa kuwa dhambi yao ni kubwa,
21 sasa nitashuka pale na kuona kilio kilicho nifikia dhidi yake, ikiwa kweli wamefanya au hawakufanya, nitajua.”
22 Kwa hiyo wale wanaume wakageuka toka pale, na kuelekea Sodoma, lakini Abraham akabaki amesimama mbele ya Yahwe.
23 Kisha Abraham alikaribia na kusema, “Je utawafutilia mbali watakatifu pamoja na waovu?
24 Huenda wakawepo wenye haki hamsini katika mji. Je utawakatilia mbali na usiuache mji kwa ajili ya hao watakatifu hamsini walioko hapo?
25 Hasha usifanye hivyo, kuwauwa watakatifu pamoja na waovu, ili kwamba watakatifu watendewe sawa na waovu. Hasha! Je muhukumu wa ulimwengu wote hatatenda haki?”
26 Yahwe akasema, “Katika Sodoma nikipata watakatifu hamsini kwenye mji, nita uacha mji wote kwa ajili ya hao.”
27 Abraham akajibu na kusema, “Tazama, Nimeshika kusema na Bwana wangu, hata kama mimi ni mavumbi na majivu!
28 Itakuwaje ikiwa kuna watano pungufu katika idadi ya hao watakatifu hamsini? Je utaangamiza mji wote kwa upungufu wa hao watano?” Akasema, “Sitaangamiza, ikiwa nitapata watu arobaini na watano pale.”
29 Akaongea naye tena, na kusema, “Itakuwaje ikiwa arobaini watapatikana pale?” Akajibu, “Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini.”
30 Akasema, Tafadhali usikasirike, Bwana, nikiongea. Pengine thelathini watapatikana pale.” Akajibu, 'Sitafanya, ikiwa nitapata thelathini pale.”
31 Akasema, Tazama, Nimeshika kusema na Bwana wangu! Pengine ishirini watapatikana pale.” Akajibu, “Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini.”
32 Akasema, “Tafadhali usikasirike, Bwana, na nitasema jambo hili kwa mara ya mwisho. Huenda kumi wakaonekana kule.” Na akasema, sitaangamiza kwa ajili ya hao kumi.”
33 Yahwe akaendelea na njia yake mara tu baada ya kumaliza kuongea na Abraham, na Abraham akarudi nyumbani.